Entertainment
Wasanii wa Kuimba Wanatabia Nyingi za Kihuni Kuliko wa Hip Hop asema Roma Mkatoliki

Msanii wa hip hop kutoka Tanzania anayeishi Marekani, Roma Mkatoliki, amevunja kimya kuhusu kile alichokitaja kuwa dhana potofu inayoambatanishwa na muziki wa hip hop.
Kupitia mitandao yake ya kijamii, Roma alisisitiza kuwa kwa miaka mingi, jamii imekuwa ikiwaona marapa kama wahuni na waasi wa maadili bila sababu ya msingi. Kauli yake imezua mjadala mzito kuhusu mitazamo ya kijamii, hususan tofauti ya namna jamii inavyowaona wasanii wa hip hop na waimbaji wa nyimbo laini.
Roma alisema marapa ni wastaarabu.
“Na sijui ni nani aliwakaririsha hiki kitu. Ukweli ni kwamba tabia nyingi za kihuni wanazo wasanii wa kuimba. Wasanii wa hiphop wengi ni wastaarabu mno,” alisema.
Roma ameeleza kuwa wasanii wengi wa kuimba wanavuta bangi, kunywa pombe, kubadilisha wapenzi kila mara, na kuimba nyimbo zilizojaa matusi na mafumbo ya ngono.
Kwa mujibu wa Roma Mkatoliki ni kuwa wasanii wengi wa hip hop wanaishi maisha yenye misingi ya familia, heshima, na maadili. Wengi wao hawatumii pombe wala bangi.
Roma alitoa mfano wa Nay wa Mitego, Nikki wa Pili, Kala Jeremiah, na Gnako. Zaidi ya hayo, Roma alisema wasanii wa hip hop ndio wanaoongoza kushika nafasi za uongozi ndani ya tasnia ya muziki na hata katika harakati za kijamii.
“Wasanii wengi wa kuimba wanakunywa pombe, tofauti na wasanii wa hiphop. Mtu kama Nay, Nikki wa Pili, Kala I guess na G-Nako hawali tungi kabisa. Wasanii wa kuimba, wengi nyimbo zao zimejaa matusi, ” Roma alisema.
Entertainment
Mboga Imejileta; Arrow Bwoy Aitisha Pigano Dhidi ya Shakib

Msanii maarufu wa Kenya, Arrow Bwoy, amezua gumzo mtandaoni baada ya kumualika wazi wazi mfanyabiashara kutoka Uganda, Shakib Cham, kwenye pambano la ndondi.
Hii imekuja baada ya kipigo cha hadharani ambacho Shakib alipokea kutoka kwa msanii mwenzake wa Uganda, Rickman, hali iliyoacha mashabiki wengi wakisema: “Sasa ata Arrow Bwoy anaweza!”
Kupitia video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Arrow Bwoy, anayefahamika kwa vibao kama Digi Digi, hakuonyesha woga wowote. Kwa ucheshi, alisema amekuwa akisubiri nafasi kama hii kwa muda mrefu.
“Mboga imejileta,” alisema kwa kujiamini, akimaanisha kuwa Shakib amejileta mwenyewe kwenye kipigo.
“Chakula kiko tayari. Niko tayari kwa pambano hili.”
Arrow Bwoy pia hakusita kumtaja mke wa Shakib, Zari Hassan, akimtaka akae mbali na ulingo siku ya pambano hilo kwa usalama wake binafsi.
“Zari, usijisumbue kuja. Hii si sehemu ya wanawake. Usije ukazimia tukapata janga la pili,” alisema kwa kejeli.
Hata hivyo, wakosoaji wake walikumbusha jamii kuhusu video za awali zinazoonyesha Arrow Bwoy akichapwa na polisi wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha. Swali likabaki: Je, kweli ana uwezo wa kumpiga Shakib au ni porojo za mitandaoni?
Kwa jina la Zari kuingizwa kwenye sakata hili, mvutano umeongezeka na mashabiki kote Afrika Mashariki wanasubiri kuona kama Shakib atakubali changamoto hii ya kihistoria.
“Zari, kama unasikia, mtume tu kijana wako aje achukue kichapo — kichapo cha kimataifa,” Arrow Bwoy alimalizia kwa msisitizo.
Kwa sasa, macho yote yako kwa Shakib. Je, atakubali changamoto hii na kuweka historia mpya ya burudani Afrika Mashariki?
Entertainment
#CHAN2024: Savara, Zuchu na Eddy Kenzo Kutumbuiza Fainali ya CHAN 2024 Nairobi

Mashindano ya CHAN 2024 yakielekea ukingoni, mashabiki wanatarajiwa kupata burudani ya aina yake kutoka kwa baadhi ya nyota wakubwa wa muziki Afrika Mashariki.
Kenya, Uganda na Tanzania zitawakilishwa vilivyo kupitia majina makubwa matatu: Savara wa Kenya (mwanachama wa zamani wa kundi maarufu Sauti Sol), Eddy Kenzo wa Uganda, na Zuchu kutoka Tanzania, anayejulikana kwa jina halisi Zuhura Othman.
Onyesho hili la kufunga pazia litafanyika sambamba na mechi ya fainali Jumamosi, likitarajiwa kuhamasisha na kuburudisha maelfu ya mashabiki watakaofurika uwanja wa Kasarani. Shoo hiyo inalenga kumaliza mashindano haya ya kihistoria kwa upekee na kiwango cha juu cha burudani.
Mbali na kusubiriwa kwa hamu jukwaani, Savara pia amekuwa na mchango mkubwa nyuma ya pazia. Yeye ndiye mtunzi na mtayarishaji wa wimbo rasmi wa CHAN 2024 unaoitwa “Pamoja”.
Wimbo huo unashirikisha nyota kutoka kanda hii: Elijah Kitaka wa Uganda na Phina wa Tanzania. Uliimbwa kwa mara ya kwanza katika sherehe za ufunguzi na uliweka ladha na hamasa ya mashindano haya.
Ingawa wenyeji wa mashindano haya—Kenya, Uganda na Tanzania—waliishia katika hatua ya robo fainali, fainali za mwaka huu zinaahidi kuwa kilele cha msisimko.
Burudani kutoka kwa Zuchu, Savara na Eddy Kenzo itakuwa chachu ya kuhitimisha mashindano yaliyojaa matukio na hisia.
Kwa upande mwingine, kumekuwa na malumbano mitandaoni kati ya mashabiki wa Kenya na Tanzania, hususan baada ya timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, kudondoshwa nje ya michuano hiyo katika robo fainali.
Mashabiki wa Tanzania hawakusita kuchokoza wenzao kwa kejeli, jambo lililoongeza ladha ya ushindani wa nje ya uwanja.