News
Wanaharakati na vijana wa Gen -z wazua purukushani kwenye majengo ya bunge la Mombasa

Wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu na vijana wa Gen – Z katika kaunti ya Mombasa wemezuiwa kuingia katika bunge la kaunti ya Mombasa kuwasilisha malalamishi yao kuhusiana na bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2025/26.
Vijana hao pamoja na wanaharakati hao waliojawa na hasira wanasema wenyeji wa Mombasa hawajahusishwa kiukamilifu Katika mchakato huo tofauti na inavyofanyika kwenye kaunti zingine nchini.
Wanadai hali ya kutokuwa na uwazi katika utekelezaji wa miswada ya fedha kwenye kaunti hiyo kunachangia kwa shughuli mbalimbali kaunti ya Mombasa kukosa kutekelezwa ipasavyo
Hatahivyo baadae Karani wa bunge la kaunti ya Mombasa salim Juma alipokea malalamishi yao na kuahidi kutoa mwelekeo ufaao Jumanne wiki ijao huku vijana hao wakitishia kurudi tena iwapo malalamishi yao hayatatiliwa maanani.

Bunge la kaunti ya Mombasa/Picha kwa hisani
News
Anselim, ashutumu utovu wa usalama Taita Taveta

Kaimu Spika katika bunge la kaunti ya Taita Taveta Anselim Mwadime alieleza kusikitishwa na mauaji ya mhudumu mmoja wa bodaboda aliyeuliwa na kisha pikipiki yake kuchukuliwa katika eneo la chuo kikuu cha Taita Taveta.
Mwadime alisema kuna baadhi ya abiria ambao ni wahuni hubebwa na kisha kuwashambulia wahudumu wa pikipiki hadi kuwaua au hata kutoweka na pikipiki.
Aidha, Mwadime alisema kama viongozi wa kaunti ya Taita Taveta hawataruhusu visa hivyo kuendelezwa katika kaunti hiyo.
Vilevile, Mwadime aliishinikiza idara ya usalama kwenye kaunti ya Taita Taveta kuwajibika ipasavyo ili kudhibiti visa vya utovu wa usalama katika sekta ya bodaboda na wanaohusika wakabiliwe kisheria.
“Hili jambo linafaa kufuatiliwa kwa undani. Na tunalilaani vikali sisi kama viongozi wa Taita Taveta’’ alisema Mwadime.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Viongozi wahimizwa kushirikiana kubuni ajira kwa vijana

Mwakilishi wa wadi ya Sabaki eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi Rose Baraka alitoa wito kwa viongozi wa kaunti ya Kilifi kushirikiana na mashirika ya kijamii pamoja na wawekezaji katika kaunti ya Kilifi ili kudhibiti changamoto za ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.
Rose alisema hatua hiyo itasaidia pakubwa kuwaepusha vijana kujiingiza kwenye utumizi wa mihadarati sawa na uhalifu.
Akizungumza wakati wa kikao kilichowaleta pamoja maafisa wa shirika la SHOFCO pamoja na wakaazi wa Sabaki, Rose aliahidi kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kijamii katika juhudi za kuwasadia wananchi kujiendeleza kupitia mpango wa ajira.
“Vijana ni wengi, kazi ni kidogo. Sisi kama viongozi tunastahili kutia bidii kutafuta haya mashirika ili tuangalie vijana wetu wasaidika vipi’’ alisema Rose Baraka.
Kwa upande wake Afisa wa Shirika la SHOFCO eneo la Magarini Kelvin Mtawali Karisa aliupongeza ushirikiano wa mwakilishi wa wadi huyo na shirika hilo na kuwataka vijana kujiunga kwenye makundi mbalimbali ili waweze kupata mikopo ya kujiendeleza kimaisha.
Taarifa ya Janet Mumbi