Entertainment
Wakili George Kithi na Mbosso Khan Waanzisha Ushirikiano wa Kimkakati kuinua Muziki wa Africa Mashariki

Wakili na mwanasiasa maarufu kutoka Kilifi, George Kithi, ameweka wazi azma yake ya kuendelea kukuza sekta ya muziki na ubunifu katika ukanda wa Pwani ya Kenya kwa njia za kimkakati na kimataifa.
Wakili Kithi aliyasema haya Jijini Dar es salaam Tanzania alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwanamuziki nyota wa Bongo flavor, Mbosso Khan, katika mazungumzo yaliyolenga kuleta mageuzi ya kweli katika Sekta ya muziki wa Pwani na Kenya kwa ujumla.
“Nilifanya kikao chenye mafanikio na msanii maarufu kutoka Tanzania, Mbosso Khan, jijini Dar es Salaam, ambapo tulijadili mbinu za kimkakati katika kuboresha muziki na kukuza wasanii hususan kutoka Kaunti ya Kilifi na eneo zima la Pwani.,” Kithi alisema.
Mkutano huu ni hatua Moja wapo ya kuendeleza uhusiano kati ya Kiongozi huyo na Mwanamuziki Mbosso baada ya ziara ya Mwanamuziki huyo Mjini Kilifi mnamo Desemba 31, 2023, ilitia fora na kuweka Msingi mahusiano bora.
Ziara ya Mbosso mjini Kilifi ilizua gumzo Kwa jinsi ilivyoshabikiwa kufuatia show yake ya kukata na shoka katika eneo la Old Fery Kilifi, na kuwavutia maelfu ya mashabiki.
Tukio hilo liliangazia kiwango cha hamasa na kiu ya burudani ambayo Pwani inayo na huenda ndicho Kithi anataka kuendeleza kwa vitendo.
Miongoni mwa mambo wanayolengwa katika usjirikiano huu pia ni kuleta mshikamano na ushirikiano wa karibu baina ya wasanii wa Africa Mashariki Kwa lengo ya kukuza sekta na muziki Kwa kutumia teknolojia ya kisasa, vifaa bora, na ubadilishanaji wa maarifa kutoka pande zote mbili za mipaka.
Zaidi ya hayo, walitathmini njia za kuwasaidia wasanii kibiashara kwa kuwapatia mafunzo kuhusu jinsi ya kutumia teknolojia kupata mapato kupitia majukwaa mbali mbali ya kidijitali mfano mapato ya muziki kupitia mtandaoni (streaming royalties), uuzaji wa maudhui (content monetization), ushirikiano na chapa mbalimbali (brand partnerships), pamoja na mbinu za kujenga hadhira kupitia mitandao ya kijamii. Lengo kuu likiwa ni kuhakikisha kuwa kipaji kinaweza kubadilishwa kuwa taaluma, na muziki kuwa chanzo halisi cha mapato.
Kwa mujibu wa Kithi, mafunzo haya yatasaidia sana kubadilisha fikra za muziki kuwa kipaji tu, hadi kuwa chanzo cha mapato na ajirankwa vijana wa Pwani.
Huenda hii ikawa hatua kubwa kuelekea kuinua uchumi wa kijamii kupitia sekta ya ubunifu.
“Maarifa katika eneo hili yanaweza kubadilisha ari kuwa taaluma na kipaji kuwa chanzo cha mapato,” alisema Kithi.
“Tumejikita katika kukuza vipaji, kujenga ushirikiano, na kuunda fursa zitakazoinua vijana wetu na kuiweka kanda yetu kwenye ramani ya dunia” aliongezea.
George Kithi ametangaza kuwa kuna mengine mengi yanakuja, ikiwa ni pamoja na miradi mipya ya ushirikiano, mafunzo ya ubunifu, na kuibua vipaji vijijini.
Entertainment
Mboga Imejileta; Arrow Bwoy Aitisha Pigano Dhidi ya Shakib

Msanii maarufu wa Kenya, Arrow Bwoy, amezua gumzo mtandaoni baada ya kumualika wazi wazi mfanyabiashara kutoka Uganda, Shakib Cham, kwenye pambano la ndondi.
Hii imekuja baada ya kipigo cha hadharani ambacho Shakib alipokea kutoka kwa msanii mwenzake wa Uganda, Rickman, hali iliyoacha mashabiki wengi wakisema: “Sasa ata Arrow Bwoy anaweza!”
Kupitia video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Arrow Bwoy, anayefahamika kwa vibao kama Digi Digi, hakuonyesha woga wowote. Kwa ucheshi, alisema amekuwa akisubiri nafasi kama hii kwa muda mrefu.
“Mboga imejileta,” alisema kwa kujiamini, akimaanisha kuwa Shakib amejileta mwenyewe kwenye kipigo.
“Chakula kiko tayari. Niko tayari kwa pambano hili.”
Arrow Bwoy pia hakusita kumtaja mke wa Shakib, Zari Hassan, akimtaka akae mbali na ulingo siku ya pambano hilo kwa usalama wake binafsi.
“Zari, usijisumbue kuja. Hii si sehemu ya wanawake. Usije ukazimia tukapata janga la pili,” alisema kwa kejeli.
Hata hivyo, wakosoaji wake walikumbusha jamii kuhusu video za awali zinazoonyesha Arrow Bwoy akichapwa na polisi wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha. Swali likabaki: Je, kweli ana uwezo wa kumpiga Shakib au ni porojo za mitandaoni?
Kwa jina la Zari kuingizwa kwenye sakata hili, mvutano umeongezeka na mashabiki kote Afrika Mashariki wanasubiri kuona kama Shakib atakubali changamoto hii ya kihistoria.
“Zari, kama unasikia, mtume tu kijana wako aje achukue kichapo — kichapo cha kimataifa,” Arrow Bwoy alimalizia kwa msisitizo.
Kwa sasa, macho yote yako kwa Shakib. Je, atakubali changamoto hii na kuweka historia mpya ya burudani Afrika Mashariki?
Entertainment
#CHAN2024: Savara, Zuchu na Eddy Kenzo Kutumbuiza Fainali ya CHAN 2024 Nairobi

Mashindano ya CHAN 2024 yakielekea ukingoni, mashabiki wanatarajiwa kupata burudani ya aina yake kutoka kwa baadhi ya nyota wakubwa wa muziki Afrika Mashariki.
Kenya, Uganda na Tanzania zitawakilishwa vilivyo kupitia majina makubwa matatu: Savara wa Kenya (mwanachama wa zamani wa kundi maarufu Sauti Sol), Eddy Kenzo wa Uganda, na Zuchu kutoka Tanzania, anayejulikana kwa jina halisi Zuhura Othman.
Onyesho hili la kufunga pazia litafanyika sambamba na mechi ya fainali Jumamosi, likitarajiwa kuhamasisha na kuburudisha maelfu ya mashabiki watakaofurika uwanja wa Kasarani. Shoo hiyo inalenga kumaliza mashindano haya ya kihistoria kwa upekee na kiwango cha juu cha burudani.
Mbali na kusubiriwa kwa hamu jukwaani, Savara pia amekuwa na mchango mkubwa nyuma ya pazia. Yeye ndiye mtunzi na mtayarishaji wa wimbo rasmi wa CHAN 2024 unaoitwa “Pamoja”.
Wimbo huo unashirikisha nyota kutoka kanda hii: Elijah Kitaka wa Uganda na Phina wa Tanzania. Uliimbwa kwa mara ya kwanza katika sherehe za ufunguzi na uliweka ladha na hamasa ya mashindano haya.
Ingawa wenyeji wa mashindano haya—Kenya, Uganda na Tanzania—waliishia katika hatua ya robo fainali, fainali za mwaka huu zinaahidi kuwa kilele cha msisimko.
Burudani kutoka kwa Zuchu, Savara na Eddy Kenzo itakuwa chachu ya kuhitimisha mashindano yaliyojaa matukio na hisia.
Kwa upande mwingine, kumekuwa na malumbano mitandaoni kati ya mashabiki wa Kenya na Tanzania, hususan baada ya timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, kudondoshwa nje ya michuano hiyo katika robo fainali.
Mashabiki wa Tanzania hawakusita kuchokoza wenzao kwa kejeli, jambo lililoongeza ladha ya ushindani wa nje ya uwanja.
-
News21 hours ago
Mahakama ya Kilifi imetoa hukumu kwa wanaume 6 wanaokabiliwa na mashtaka ya unajisi
-
Sports19 hours ago
Kocha wa Uingereza Thomas Tuchel akataa madai ya “laana” huku akilenga kuvunja ukame wa miaka 60 wa mataji makubwa
-
News22 hours ago
Thoya: Serikali kuu iongeze mgao wa fedha kwa sekta ya Afya