News
Wakaazi wa Magarini wanalalamikia uhaba wa maji

Wakaazi wa Magarini kaunti ya Kilifi wanalalamikia kukithiri kwa changamoto ya uhaba wa maji inayoendelea kushughudiwa katika eneo hilo.
Wakiongozwa na Joseph Kithi, wakaazi hao walielezea kusikitishwa na jinsi eneo hilo limesalia bila huduma za maji kwa kipindi kirefu.
Aidha walisema maeneo mengine ya kaunti ya Kilifi yakipata maji kwa urahisi, itakuwa jambo mwafaka katika kufanikisha miradi mbalimbali ya kimaendeleo lakini suala hilo limekosa kuangizwa na kuchangia wanawake wengi kupitia changamoto.
Kithi alidokeza kwamba kwa sasa eneo hilo limebaki bila huduma za maji kwa takriban miezi miwili, akiilaumu serikali kwa kutoangazia mikakati ya kusuluhisha changamoto hiyo.
“Sisi wakaazi wa Magarini tumekuwa tukipita changamoto nyingi sana za ukosefu wa maji, jambo la kusitisha ni kwamba maji yanatoka hapa karibu na maeneo yetu LangoBaya lakini ichukua mda mrefu bila maji, kwani haya maji yanaenda wapi kwani shinda ya maji imekuwa miaka nenda miaka rudi inachukua mda mrefu bila maji”, alisema Kithi.
Wakaazi hao waliiomba serikali kuhakikisha kwamba huduma za maji zinarudishwa haraka iwezekanavyo la sivyo wataandamana hadi pale changamoto hiyo itakapoangaziwa kikamilifu na wananchi kupata maji.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Wachungaji 85 Adu, Kilifi wapokea mafunzo ya kukabili itikadi kali

Jumla ya wachungaji 85 kutoka wadi ya Adu eneo bunge la Magarini kaunti ya kilifi wanaendelea kupokea mafunzo ya kidini kuhusu sheria zinazoambatana na utoaji wa mafunzo ya dini katika makanisa.
Wakiongozwa na Johnson Kaingu mchungaji wa kanisa la PGM Ramada, wachungaji hao walisema kuwa mafunzo hayo yatasaidia pakubwa kudhibiti makanisa yanayoendeleza mafunzo ya imani potofu.
Wachungaji hao aidha walipongeza mpango huo wakisema utatoa mwelekeo wa jinsi wachungaji wanavyostahili kuhudumu pasi na kupotosha waumini.
“Tuliposikia habari zile za Shakahola tuliona si vizuri tubaki hivyo ila tupate mafundisho maalum kama wachungaji, ili tuweze kudhibiti makanisa yetu yasiangukie mtego ule wa Shakahola. Ufahamu huu ambao umeletwa huku kwetu Adu umetufanya sisi tutakuwa hata tukisimama tutakuwa hata tukisimama tunajua tunafundisha nini ili watu wa Mungu tujue tutawaelekeza katika njia ambayo inafaa”,walisema wachungaji.
Kwa upande wake Elizabeth Dama mmoja wa wachungaji hao ameupongeza mpango huo akisema utawasaidia kutoa mafunzo ya kweli kwa waumini.
“Tuko wachungaji 85 kupitia Christian Pass ambao wametushika mkono ndio wanatufadhili tufundishwe ndio wanalipa walimu”,alisema mchungaji Dama.
Mafunzo hayo yanayofadhiliwa na shirika la Christian Pass yanajiri baada ya kushuhudiwa kwa idadi kubwa ya maafa ya watu katika msitu wa Shakahola sawa na eneo la Kwa Binzaro kupitia mafunzo ya dini potofu.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Mackenzie yuko salama, wasema maafisa gerezani Shimo la tewa

Afisa anayesimamia gereza la Shimo la Tewa, Abdi Willy Adan amekanusha madai yalioibuliwa na mhubiri tata Paul Mackenzie kwamba maisha yake yako hatarini akiwa katika gerezani hilo.
Akizungumza mbele ya mahakama ya watoto ya Tononoka, Adan alisema hakuna vitu vya kutiliwa shaka vilivyowekwa kwenye chumba cha Mackenzie katika gereza hilo la Shimo la Tewa, na kwamba usalama wa gereza uko imara.
Mackenzie, anayekabiliwa na mashtaka yanayohusiana na mauaji ya Shakahola, alikuwa ameomba kuhamishwa hadi Gereza la Manyani lakini Adan alikataa, akisema uzito wa mashtaka unahitaji asalie katika gereza la usalama wa juu.
Adan Pia alisema madai ya Mackenzie ya mgomo wa njaa hayana msingi wowote kwani rekodi zinaonyesha wazi kwamba yeye na washukiwa wengine wanaendelea kula chakula wakiwa gerezani.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Jami Yamina, ulipinga ombi la kuahirisha kwa kesi hiyo kwa sababu ya mgomo wa njaa, na kuutaja kama jaribio la kuchelewesha haki ya waathiriwa.
Hata hivyo Hakimu Nelly Chepchirchir alikataa ombi la kuahirisha kwa kesi hiyo, akisema mgomo wa njaa wa kujiletea sio sababu ya kusimamisha kesi, na akaagiza washukiwa wapewe nafasi ya kuwasiliana na mawakili wao.
Mackenzie na wenzake 34 wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya watoto katika msitu wa Shakahola kaunti ya Kilifi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu