News
Wakaazi wa Lamu Waandamana Kupinga Mradi wa Kawi ya Mawe

Wakaazi wa kaunti ya Lamu kwa ushirikiano na Shirika la kijamii la Save Lamu wamefanya maandamano ya amani kupinga mradi wa uzalishaji wa Kawi ya Mawe yaani Coal Plant katika kaunti hiyo.
Wakaazi hao wamesema baada ya kufanya utafiti kuhusu mradi huo wamebaini kwamba una madhara mengi kwa afya ya jamii, wakishikilia kwamba wataendelea kuupinga mradi huo wa serikali.
Wakaazi hao aidha wameitaka Mahakama ya kuu ya Malindi ambayo inatarajiwa kutoa uamuzi wake kuhusu mradi huo kusikiliza kilio cha wakaazi wa kaunti ya Lamu na kupiga marufuku ujenzi wa mradi huo.
Hata hivyo Wawekezaji wa mradi huo ambao ni Lamu Coal Power Plant wamewasilisha rufaa Mahakamani kabla ya uamuzi wa Mahakama siku ya Alhamis.
News
Mwanaharakati Mwabili Mwagodi apatikana

Mwanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu Mwabili Mwagodi ambaye alidaiwa kutekwa nyara akiwa nchini Tanzania sasa amepatikana.
Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za kibinamu nchini la VOCAL Africa Hussein Khalid, alisema Mwabili alipatikana katika msitu wa Kinondo eneo bunge la Msambweni kaunti ya Kwale mwendo wa saa tisa usiku akitembea kuelekea Diani.
Khalid alisema Mwabili, anaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Pandya mjini Mombasa kisha baadaye atasafirishwa kwa ndege hadi jijini Nairobi kuungana na familia yake.
“Tunashukuru Mwabili amepatikana akiwa hai japo amedhohofika na anaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Pandya na kisha atarudi Nairobi kukutana na familia yake lakini tunaiambia serikali ya Kenya na Tanzania ni lazima wahusika kukomesha tabia hii ya kuwateka watu nyara kuna sheria kama mtu amekosea apelekwe Mahakamani”, alisema Khalid.
Hata hivyo Wanaharakati hao wa kutetea haki za kibinadamu waliishtumu serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuwanyanyasa wanaharakati wa kijamii wa taifa la Tanzania na wale wanaoingia Tanzania kutoka mataifa mengine ili kuendeleza hamasa za haki za kijamii.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Herman yahairishwa

Kesi ya mauaji ya mfanyabiashara ambaye ni raia wa Uholanzi, Rowenhorst Herman na mlinzi wake Evans Bokoro imeahirishwa hadi mwezi Oktoba mwaka huu kufuatia Mahakama kuingia kwenye mapumziko rasmi ya majaji.
Mke wa Marehemu, Riziki Cherono pamoja na mshukiwa mwenza Timothy Omondi wanakabiliwa na mashtaka ya kupanga na kutekeleza mauaji hayo yaliyotokea Juni 4 mwaka 2021 katika eneo la Shanzu kaunti ya Mombasa.
Katika kikao cha awali cha Mahakama, Afisa wa Polisi Koplo Richard Cheruiyot alieleza mbele ya Jaji Wendy Micheni kwamba Cherono alijaribu kuonekana kama mwathirika kwa madai ya kutekwa nyara na majambazi waliodaiwa kuvamia nyumba yao.
Afisa huyo alieleza kwamba walimkuta Cherono akiwa amefungwa kwenye usukani wa gari lake, huku akidai kwamba alivamiwa na kulazimishwa kuondoka nyumbani kwao akiwa chini ya tishio la bunduki.
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa ulibaini kwamba Marehemu Herman alipatikana amefariki nyumbani kwake akiwa amefungwa mikono na miguu huku mlinzi wao, Evans Bokoro, alikutwa akiwa hai kwa taabu karibu na bwawa la kuogelea lakini baadaye alifariki akipelekwa hospitalini.
Mashahidi wa upande wa mashtaka pamoja na polisi, wanaamini kwamba Cherono ndiye mshukiwa mkuu wakidai kwamba alipanga na kufanikisha mauaji hayo kwa kushirikiana na watu wengine, wakiwemo waliotajwa kuwa sehemu ya genge lililovamia nyumba hiyo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu