News
Waislam Waadhimisha Sikukuu ya Eid-Ul-Adha

Waislam kote duniani wanaadhimisha Sikukuu ya Eid-Ul-Adha, inayojulikana pia kama sikukuu ya sadaka, ambayo huadhimishwa katika mwezi wa Dhul Hijjah katika kalenda ya Kiislam.
Sikukuu hii ni moja ya nyakati tukufu zaidi katika Uislamu, ikiashiria kilele cha Hijja na kuadhimisha utiifu wa Nabii Ibrahimu aliyekuwa tayari kumtoa mwanawe Ismail kama sadaka kwa amri ya Mwenyezi Mungu.
Siku kumi za mwanzo za Dhul Hijjah zinahesabiwa kuwa siku takatifu zaidi, zikiwa zimejawa na ibada, kufunga, na dua.
Mwaka huu, zaidi ya mahujaji milioni 2 wanahudhuria Hijja katika mji mtakatifu wa Makkah nchini Saudi Arabia, Kenya ikipeleka wahujaji 4,500, kuhijji, ikiwa ni mojawapo ya idadi kubwa zaidi katika historia ya hivi karibuni.
Viongozi mbalimbali wa dini ya kiislam waliwahimiza waumini wa dini ya kiislam kuhakikisha wanasheherekea sikukuu ya Eid-ul-Adha pamoja na wale wasiojiweza kwa kuchinja mifugo na kugawa na watu wengine wasiobahati katika jamii.
Taarifa ya Lolani Kalu
News
Wakaazi wa Voi waonywa dhidi ya ugonjwa wa MPOX

Daktari wa magonjwa ya kuambukiza katika hospitali ya rufaa ya Moi mjini Voi katika kaunti ya Taita Taveta Urbanius Kioko amewataka wenyeji wa kaunti hiyo kuzingatia maagizo ya Wizara ya Afya ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Mpox.
Akiongea kwenye warsha ya Wanahabari iliyofadhiliwa na Shirika la Stawisha Pwani, Daktari Kioko alisema wananchi wanapaswa kujikinga ili kudhibiti ugonjwa huo kuenea.
Kioko pia aliwataka wale ambao wana dalili za ugonjwa huo kufika kwenye vituo vya afya ili kutibiwa.
“Huu ugonjwa huwa unaenezwa kupitia kutangamana, kuvaa nguo za mwenzako na kupitia hewa wakati wa kuongea’’, alisema Kioko.

Wadau wa sekta ya Afya katika kikao na Wanahabari mjini Voi
Vilevile, Kioko alitaja kisa cha mgonjwa mmoja wa Mpox kilichothibitishwa siku ya Jumanne wiki hii mjini Voi huku visa vingi vikishamiri katika kaunti Mombasa.
Haya yanajiri huku Wizara ya Afya nchini ikishinikiza wananchi kujiepusha kula nyama za Wanyamapori miongoni mwa tahadhari zingine kama njia mojawapo ya kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Mpox.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Mzozo kati ya Kenye na Tanzania waendelea kutokota

Serikali ya Kenya imeiandikia barua jumuiya ya afrika mashariki kupinga vikwazo vilivyowekwa na Tanzania kuhusu kufanya biashara katika taifa hilo.
Katibu mkuu katika idara ya EAC Daktari Caroline Karugu, alisema kenya imebaini kuwa agizo hilo haliambatani kamwe na masharti muhimu ya itifaki ya soko la pamoja la EAC, ambayo inahakikisha uruhu wa watu kusafiri, kuhudumu na haki ya kuanzishwa kwa biashara na raia wa mataifa ya afrika mashariki.
Aidha Kenya iliasema imeandika rasmi barua kwa EAC kuiarifu rasmi jamhuri ya muungano wa Tanzania kuangazia upya agizo hilo ili kuhakikisha inafuata kikamilifu mkataba wa EAC na sheria za Jumuia.
Maafisa wa EAC kwa sasa wanafanya uchambuzi wa hatua hiyo na itawasilisha hatua zozote zilizokiukwa pamoja na kaununi zilizopo katika mkutano ujao wa baraza la kisekta la biashara, viwanda na uekezaji.
Taarifa ya Joseph Jira