Business
Wafanyabiashara wa Soko la Mtwapa Walalamikia Ukosefu wa Maji Kwenye Soko Hilo

Wafanyabiashara wa Soko la Mtwapa kaunti ya Kilifi wamelalamikia ukosefu wa maji kwenye Soko hilo ambapo wafanyibiashara wengi wanalitegemea kuendeleza shughuli zao za kila siku.
Kulingana na mwenyekiti wa Soko hilo Millicent Mbodze ukosefu wa maji katika soko hilo limeathiri biashara zao kwani maji yanatumiwa kuonsha bishaa nyingi kama vile matunda, mboga na hata samaki kwa wanaouza samaki katika soko hilo.
Aidha amesema wateja wengi wanalalamikia hali mbaya ya ya soko hilo kwani kumejaa uchafu kila mahali hali inayowasababishia kuhofia afya yao.
Amesema tayari wateja wengi wanasusia maeneo hayo jambo ambalo liewasababishishia hasara kubwa kwani bidhaa nyingi huozea sokoni.
Wakati huo huo Mbodze amesema licha ya kuwasilisha swala hilo kwa kwa wahusika sawa na serikali ya kaunti ya Kilifi,bado halijatatuliwa.
Anasema imekuwa changamoto kwa wafanyabiashara kwani imekuwa shida kutumia hata sehemu za kujisaidia sokoni humo huku ikiwalazimu kutafuta bidhaa hiyo kwenye kituo kimoja cha mafuta kilichoko eneo hilo.
Huku hayo yakijiri benki ya dunia imetenga shilingi bilioni 2.58 kuimarisha mpango wa usabasazaji maji katika kaunti ya kilifi.
Mradi huo unalenga miji ya malindi , kilifi na mtwapa na utahusisha kubadilishwa kwa mabomba makuku ya maji na kuweka mabomba mapya.
Ikumbukwe Gavana wa kilifi Gedion Mung’aro alisema miradi hiyo itahakikisha kuwa kaunti hiyo iko na maji safi na yakutosha.
Business
KEMFRI kuanzisha mradi maalum wa kuzalisha mbegu za samaki

Taasisi ya utafiti wa bahari na uvuvi nchini, KEMFRI, imeanzisha mradi maalum wa kuzalisha mbegu za samaki, ili kuongeza upatikanaji wao na kuinua sekta ya uvuvi nchini.
Akizungumza jijini Mombasa, kaimu mkurugenzi mkuu wa KEMFRI, Dkt. James Mwaluma, alisema kuwa mradi huo unatekelezwa katika eneo la Shimoni kaunti ya Kwale na unalenga kuzalisha samaki wa thamani kubwa kama vile kamba, matiko, na aina nyingine ambazo upatikanaji wake ni nadra.
Dkt. Mwaluma alisema kuwa mbegu zitakazozalishwa kupitia mradi huo zitasambazwa kwa vikundi vya vijana na wanawake wanaojihusisha na shughuli za ufugaji wa samaki, ili kuwawezesha kujitegemea kiuchumi.
Aidha, aliwahimiza vijana kote nchini wakumbatie fursa zilizopo kwenye uchumi wa baharini akisema ni njia mojawapo ya kujikwamua kimaisha na kupambana na ukosefu wa ajira.
Taarifa ya Pauline Mwango
Business
Kaunti ya Kilifi yaendeleza mikakati ya kuimarisha sekta ya uvuvi

Mkurugenzi wa masuala ya uvuvi kaunti ya Kilifi Mwangi Gachuru amesema serikali ya kaunti ya Kilifi inaendeleza mikakati katika kuimarisha sekta ya uvuvi kwenye kaunti hii ya Kilifi.
Gachuru alisema wanashirikiana na wasimamizi wa fuo za bahari katika kaunti ya Kilifi katika kuhakikisha wavuvi wananufaika kupitia raslimali za baharini.
Aidha, Gachuru aliwahimiza wavuvi na wenyeji wa kaunti ya Kilifi kushirikiana ipasavyo kuhakikisha raslimali hizo zinawafaidi ipasavyo.
“Ni kupitia ushirikiano pekee ndipo mtaweza kuendeleza uvuvi wenu vizuri’’, alisema Gachuru
Akizungumzia mzozo baina ya wavuvi, Gachuru aliwataka kuzingatia sheria zilizopo kwa mujibu wa sheria za uvuvi ili kupatikane mwafaka na sio kuchukua sheria mkononi na kuahidi kuwa watawakabili kisheria wale ambao wanatumia nyavu ambazo zilipigwa marufuku kutumika baharini kuvua samaki.
“Panapotokea ugomvi miongoni mwenu, zingatieni sheria na sio kuchukua sheria mkononi’’ Aliongeza Gichuru.
Taarifa ya Janet Mumbi