News
Viongozi wahofia kulegea kwa kasi ya ujenzi wa barabara, Jaribuni

Viongozi wa kijamii katika eneo la Jaribuni kaunti ya Kilifi wamekashifu vikali hatua ya kufunguliwa kwa barabaraza kuelekea katika timbo za mawe katika eneo la Jaribuni ili kuwawezesha wawekezaji kuendelea na shughuli zao.
Wakiongozwa na Emmanuel Chai maarufu Bwenyenye viongozi hao walisema kuwa huenda ujenzi wa barabara ya Dzitsoni–Jaribuni ukachukua muda mrefu zaidi kutokana na suala hilo.
“Hali ikiendelea jinsi ilivyo basi tutaanzisha mchakato wa kutaka kusimamishwa kwa shughuli za timboni hadi pale ujenzi wa barabara utakapotamatika”, alisema Emmanuel.
Naye Mwenyekiti wa baraza la Wazee wa jamii ya Kauma Samson Mwakudza amepongeza juhudi za wakaazi na viongozi kuwashinikiza wawekezaji kujenga barabara hiyo ya takriban kilomita 14 ambayo imewafaidisha kwa kiwango kikubwa.
Hata hivyo aliwataka wakaazi kushirikiana na mkandarasi wa barabara hiyo ili kufanikisha kukamilika kwa barabara hiyo kwa wakati.
Taarifa ya Hamis Kombe
News
Joho atangaza kuwania urais siku zijazo

Waziri wa madini na masuala ya bahari nchini Hassan Ali Joho, alidokeza kwamba katika siku zijazo eneo la Pwani litatoa rais wa taifa la Kenya.
Waziri Joho aliwataka wakaazi wa Pwani kutojiingiza katika mivutano ya kisiasa na mirengo mingine ya kisiasa nchini, akisema ni wakati mwafaka wa wapwani kuungana na kujipanga kisiasa.
Waziri Joho alisema mtu ambaye alikuwa na nafasi nzuri ya kushikilia wadhfa huo wa kitaifa aliyekuwa ni Marehemu Karisa Maitha lakini ndoto hiyo bado ipo, akiweka wazi kwamba anamezea mate kiti hicho katika siku zijazo.
“Mara ya kwanza nilifikia kama kuna mpwani anaweza kuwa rais ilikuwa ni marehemu Karisa, lakini mimi hiyo ndoto bado niko nayo na nina imani iko siku bado hapa Pwani kuzaa rais. Siku moja wataskia rais Hassan na nikujipanga”, alisema Joho.
Joho alisisitiza haja ya wapwani kujipanga kisiasa ili kuwa katika nafasi nzuri ya kuvuna kwenye ngazi ya kitaifa pamoja na kuwa rahisi kwa eneo la Pwani kuwania kiti hicho na kutangaza rais wa Kenya katika siku zijazo.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Waziri Joho na Mvurya waonya wanyakuzi wa ardhi.

Waziri wa madini na uchumi wa bahari nchini Ali Hassan Joho alisema serikali haitaruhusu tena wakaazi kufurushwa katika ardhi wanayoishi.
Akizungumza katika maeneo ya Mzambarauni mjini Mtwapa eneo bunge la Kilifi Kusini kaunti ya Kilifi, Joho alionya kwamba mabwenyenye wenye hulka ya kufurusha wananchi kwenye ardhi za umma kamwe hawataruhusiwa.
Joho alisema wananchi hawafai kuhangaishwa kwenye ardhi zao huku akiwatahadharisha maafisa wa serikali dhidi ya kushirikiana na mabwenyenye kuhangaisha raia kwenye ardhi zao.
Hii ni baada ya kuibuka malalamishi ya mabwenyenye kutaka kuwafurusha wakaazi wa Utange Kaunti ya Mombasa.
Kwa upande wake Waziri wa michezo na Sanaa nchini Salim Mvurya alidokeza kuwa serikali inapanga kununua mashamba ambayo hayatumiki ili kuyakabidhi ya wananchi.
Taarifa ya Joseph Jira