News
Viongozi wahofia kulegea kwa kasi ya ujenzi wa barabara, Jaribuni

Viongozi wa kijamii katika eneo la Jaribuni kaunti ya Kilifi wamekashifu vikali hatua ya kufunguliwa kwa barabaraza kuelekea katika timbo za mawe katika eneo la Jaribuni ili kuwawezesha wawekezaji kuendelea na shughuli zao.
Wakiongozwa na Emmanuel Chai maarufu Bwenyenye viongozi hao walisema kuwa huenda ujenzi wa barabara ya Dzitsoni–Jaribuni ukachukua muda mrefu zaidi kutokana na suala hilo.
“Hali ikiendelea jinsi ilivyo basi tutaanzisha mchakato wa kutaka kusimamishwa kwa shughuli za timboni hadi pale ujenzi wa barabara utakapotamatika”, alisema Emmanuel.
Naye Mwenyekiti wa baraza la Wazee wa jamii ya Kauma Samson Mwakudza amepongeza juhudi za wakaazi na viongozi kuwashinikiza wawekezaji kujenga barabara hiyo ya takriban kilomita 14 ambayo imewafaidisha kwa kiwango kikubwa.
Hata hivyo aliwataka wakaazi kushirikiana na mkandarasi wa barabara hiyo ili kufanikisha kukamilika kwa barabara hiyo kwa wakati.
Taarifa ya Hamis Kombe
News
Waziri Joho na Mvurya waonya wanyakuzi wa ardhi.

Waziri wa madini na uchumi wa bahari nchini Ali Hassan Joho alisema serikali haitaruhusu tena wakaazi kufurushwa katika ardhi wanayoishi.
Akizungumza katika maeneo ya Mzambarauni mjini Mtwapa eneo bunge la Kilifi Kusini kaunti ya Kilifi, Joho alionya kwamba mabwenyenye wenye hulka ya kufurusha wananchi kwenye ardhi za umma kamwe hawataruhusiwa.
Joho alisema wananchi hawafai kuhangaishwa kwenye ardhi zao huku akiwatahadharisha maafisa wa serikali dhidi ya kushirikiana na mabwenyenye kuhangaisha raia kwenye ardhi zao.
Hii ni baada ya kuibuka malalamishi ya mabwenyenye kutaka kuwafurusha wakaazi wa Utange Kaunti ya Mombasa.
Kwa upande wake Waziri wa michezo na Sanaa nchini Salim Mvurya alidokeza kuwa serikali inapanga kununua mashamba ambayo hayatumiki ili kuyakabidhi ya wananchi.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Marekani yarusha makombora Iran, Trump akionya Tehran

Marekani imerusha mabomu kwenye maeneo ya Vinu vya Nyuklia vya Iran yanavyojumuisha Fordo na kuharibu kabisa maeneo hayo hatua ambayo huenda ikachangia vita zaidi ya kimataifa.
Rais wa Marekani Donald Trump alisema maeneo hayo yanayojumuisha Fordo, yalipigwa na makombora ya jeshi la Marekani huku Marekani ikijiunga na mashambulio ya Israel dhidi ya mpango wa Nyuklia wa Tehran.
Katika hatuba yake vya vyombo vya habari, Rais Trump alisema kwamba ni lazima Iran isitishe vita na kukumbatia amani iwapo wanataka vinu vyao vya Nyuklia kutorushiwa makombora.

Picha kwa hisani
“Tayari tumevuruga na kuharibu vinu vya Nyuklia vya Iran na bado tutaendelea kurusha makombora ya kasi zaidi na kuharibu vinu vyote vya Nyuklia vya Iran iwapo makao ya Tehran hayatasalimu amri”, alisema Rais Trump katika hotuba yake.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya nje wa Iran Seyed Abbas Araghchi alilaani vikali shambulizi la Marekani na kusema kwamba ni shambulizi la kuchukiza na kwamba Tehran ina njia zote za kutetea uhuru wake.
“Matukio ya asubuhi ya leo ni ya kuchukiza na yatakuwa na matokeo ya milele. Kila Mwanachama wa Umoja wa Mataifa ni lazima ashtushwe na tabia hii hatari sana, isiyo ya kisheria bali ni tabia ya kihalifu,” alisema Seyed.
Seyed aliongeza kwamba Marekani ilifanya ukiukaji mkubwa wa Katiba ya Umoja wa Mataifa kama Mwanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi