Business
Vijana Kaunti ya Tana River Waanzisha Biashara ya Sambusa za Samaki kuinua Uchumi

Vijana katika Kaunti ya Tana River wameanzisha biashara ya upishi wa sambusa za samaki kwa lengo la kujikwamua kiuchumi kwa kutumia rasilimali za baharini.
Wamebuni mbinu ya kipekee ya kuandaa sambusa kwa kutumia samaki wa aina mbalimbali, wakiwemo samaki papa. Mbali na sambusa, vijana hao pia wameweza kuunda bidhaa nyingine za thamani kutokana na samaki, hatua inayochochea ubunifu na kuongeza ajira miongoni mwao.
Kulingana na vijana hao, biashara hiyo inalenga kuongeza kipato chao na kufungua milango ya kuingia katika masoko mapya, ya ndani na hata ya nje ya kaunti.
Hatua hii imesukumwa na changamoto ya uhaba wa soko la samaki katika eneo hilo, hali ambayo husababisha uharibifu wa samaki kutokana na kukosa wanunuzi. Kwa hivyo, ubunifu huu umekuwa suluhisho la kiuchumi na kiteknolojia kwa vijana wa Tana River.
Business
Wakaazi wahofia mkurupuko wa magonjwa baada ya kuuziwa nyama Malindi

Wakaazi wa mji wa Malindi kaunti ya Kilifi wanaishi kwa hofu ya mkurupuko wa magonjwa baada ya kulalamikia kuuziwa nyama ya mifugo ambayo haijakaguliwa na maafisa wa mifugo eneo hilo.
Wakielezea manung’uniko yao, wakaazi hao walioongozwa na Kensa Ondiek walisema nyama ya mifugo inayouzwa eneo hilo haijakaguliwa, akiongeza kwamba kichinjio cha kipekee mjini humo pia kina wafanyikazi ambao ni wa umri wa chini ya miaka kumi na nane.
Wakaazi hao pia walisema mazingira ya kufanya kazi katika kichinjio hicho nai ya kutatanisha huku wachuuzi wa nyama wakifanya biashara zao mahali peupe na pachafu.
Vyombo vya Habari vilidhibitisha matukio hayo kupitia picha za watoto wakifanya kazi katika kichinjio hicho na kuchinjwa kwa mifugo siku ya Jumapili.
Afisa wa mifugo eneo la Malindi Godreck Mwaringa alitetea madai hayo akisema kwamba mifugo inayochinjwa katika kichinjio hicho hukaguliwa pindi inapofika, kabla na baada ya kuchinjwa.
Aliongezea kwamba maafisa husika hufanya kazi kuanzia siku ya Jumatatu hadi Jumamosi, japo akaweka wazi kwamba huenda wanaochinjwa siku ya Jumapili huwa ni uchinjaji wa dharura ambao pia nyama yake inafaa kukaguliwa kabla ya kuuzwa.
Hata hivyo alitoa tahadhari kwa wakazi wa Malindi kuhakikisha wananunua nyama iliyokaguliwa huku akionya kuwa watakaopatikana na mifugo wala nyama ambayo hazijakaguliwa watashtakiwa.
Taarifa ya Eric Ponda
Business
Biashara ya sare za shule imedidimia Kilifi

Wafanyibiashara wa kuuza sare za shule mjini Kilifi wamesema kuwa biashara hiyo iko chini msimu huu ikilinganishwa na wakati ambapo wanafunzi wakifungua shule mwezi wa kwanza.
Wakizungumza na cocofm wafanyibiashara hao walisema kuwa kwa sasa wazazi wengi hawanunui sare za shule kwa wingi ikilinganishwa na wakati ambapo shule zilikuwa zinafunguliwa kwa muhula wa kwanza.
Hata hivyo gharama ya juu ya maisha pia imetajwa kuchangia kudorora kwa biashara hiyo kwani wengi walilalamikia ukosefu wa fedha.
Walisema wanatarajia biashara hiyo kuimarika tena msimu ujao huku wakitoa wito kwa serikali kuu kuzingatia upya swala la kupanda kwa gharama ya maisha.
Taarifa ya Pauline Mwango