News
Ukosefu wa vitambulisho changaoto kwa usajili wa walemavu

Ukosefu wa vitambulisho vya kitaifa pamoja na vyeti vya kuzaliwa ni changamoto inayoathiri shughuli ya usajili wa watu wanaoishi na uwezo maalum kaunti ya Kwale.
Haya yametajwa na Mshirikishi wa Shirika la Muslim Women Advancement of Rights & Protection (MWARP) Mwalimu Ali, ambaye alisema wanalenga kutatua changamoto hiyo kwa kuihusisha Ofisi ya usajili wa stakabadhi hizo muhimu.
Akizungumza wakati wa zoezi la usajili wa jamii ya walemavu katika eneo la Kilimangodo eneo bunge la Lungalunga kaunti ya Kwale, Ali alisisitiza umuhimu wa stakabadhi hizo kwa jamii za mashinani.
“Tunaendelea na hamasa mashinani kwa ushirikiano na ofisi ya usajili wa vitambulisho vya kitaifa na vyeti vya kuzaliwa ili kuhakikisha jamii ya walemavu wanapata stakabadhi hiyo na kusajiliwa rasmi ili kunufaika na huduma muhimu za serikali”, alisema Ali.
Kwa upande wao jamii ya walemavu eneo hilo wamelipongeza Shirika hilo kwa kuanzisha mpango na kusema kwamba kuna haja ya wahisani mbalimbali kujitokeza na kuwasaidia ili wajiendeleze.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Washukiwa 42 wa magenge ya uhalifu wakamatwa, Malindi

Maafisa wa polisi Malindi kaunti ya Kilifi wanasema wamewanasa washukiwa 42 wa magenge ya uhalifu katika msako kwenye mitaa ya Karima, Soweto, Milano na Mgandini.
Polisi ilisema msako huo umewawezesha kuwakamata washukiwa 11 wa genge la “Wakali Mwisho” na wanawake watano kwa visa vya utovu wa nidhamu.
Msako huo unafuatia zaira ya kamanda wa polisi ukanda wa pwani Ali Nuno katika eneo hilo na kuwataka polisi kuongeza juhudi za kukabiliana na wanachama wa magenge hayo wanaoendelea kuwahangaisha wananchi.
Simu 14 zilizoshukiwa kuwa za wizi zilinaswa kutoka kwa mshukiwa Ahmed Ali.
Magenge ya uhalifu wakiwemo wale wanaojiita mawoza ni miongoni mwa makundi ya vijana ambao wamekuwa wakitatiza amani na usalama miongoni mwa wakaazi eneo hilo.
Idara ya usalama ilikuwa mbioni kuwasaka wahalifu katika mji huo wa kitalii katika juhudi za kurejesha amani na utulivu.
Vijana hao wamekuwa wakiwavamia wakaazi na kutekeleza vitendo vya wizi.
Taarifa ya Joseph Jira.
News
Mabadiliko ya tabianchi yatajwa kuchangia mapato duni ya samaki, Lamu

Wadau katika sekta ya mazingira kaunti ya Lamu wanasema mabadiliko ya hali ya anga yanayoshuhudiwa sawa na ujenzi wa bandari ya Lamu kumechangia mapato ya samaki kupungua katika bahari hindi.
Mahmoud Yusuf ambaye ni mwanazingira alisema zana za kizamani wanazotumia wavuvi kuvua samaki pia zinachangia mapato duni ya samaki.
Yusuf alisema tangu ujenzi huo wa bandari uanze, maji ya bahari chini yamekuwa na matope kutokana na kuchimbwa na kufukuliwa kwa bahari, hali iliyochangia samaki kutorokea bahari kuu.
Mwanamazingira huyo aliitaka serikali kuwapa wavuvi vifaa vya kisasa vya uvuvi sawa na meli za uvuvi zitakazowawezesha kufika maji makuu, baada ya bandari ya ndani kuharibika.
Taarifa ya Joseph Jira.