Business
Uhaba wa Samaki Wakumba Sekta ya Uvuvi Malindi

Sekta ya uvuvi katika mji wa Malindi kaunti ya Kilifi, inaendelea kukumbwa na changamoto kufuatia upepo mkali unaovuma baharini kwa kipindi cha wiki kadhaa sasa, hali inayosababisha uhaba mkubwa wa samaki sokoni na kuporomoka kwa mapato ya wavuvi.
Kwa mujibu wa Yunus Aboud Sahe, Mwenyekiti wa ufuo wa bahari katika eneo la Shella, upepo huo ulilazimu wavuvi wengi kusitisha shughuli zao za kila siku kutokana na hatari ya kuzama au kupata ajali baharini.
Sahe alisema kuwa hali hiyo imesababisha idadi kubwa ya wavuvi kukaa nyumbani, jambo ambalo linaathiri vibaya mapato yao na ustawi wa familia zao.
“Kwa sasa, hata wale wachache wanaothubutu kuingia baharini wanarejea na wastani wa kilo mbili pekee za samaki, licha ya kuhatarisha maisha yao. Hii ni hali ngumu kiuchumi na inahitaji suluhisho la haraka,” alisema Sahe.
Aidha, aliwasihi wavuvi hasa wanaovua katika maji ya kina kirefu kuwa waangalifu na kutoingia baharini wakati wa upepo mkali, bali wawe na subira hadi hali ya anga itakapokuwa salama.
Alisisitiza umuhimu wa kuzingatia tahadhari ili kuepuka majanga ambayo yamekuwa yakishuhudiwa mara kwa mara katika eneo hilo.
Business
Wavuvi Old Ferry Wageukia Biashara ya Mahindi Kutokana na Uhaba wa Samaki

Baadhi ya wavuvi kutoka eneo la old ferry kaunti ya kilifi wamegeukia biashara ya kuchoma mahindi machanga kutokana na kutoweza kuingia baharini.
Wavuvi hao wamesema kuwa msimu huu wa kusi hakuna samaki hali ambayo imefanya kuingilia biashara ya kuchoma mahindi ili kujiendeleza kimaisha.
Kulingana na wavuvi kutokana na uhaba wa vifaa vya kisasa hawawezi kuingia katika maji marefu ili kuvua samaki.
Hata hivyo wameitaka serikali kuwawezesha na vifaa vya kisasa ili waweze kuvua katika maji marefu.
Business
Wanawake Pwani Wataka Ushirikishwaji Zaidi Katika Uchumi wa Majini

Wanawake kutoka maeneo ya Pwani wanaitaka serikali kuu na zile za kaunti kuhakikisha wanashirikishwa kikamilifu katika sekta ya uchumi wa majini ili kujiendeleza kimaisha.
Wakiongozwa na Mercy Mghanga, wanawake hao wamesema licha ya wanawake wengi kujihusisha na uvuvi na shughuli nyingine za baharini, bado wanakosa vifaa na msaada wa kukuza biashara zao.
Kwa upande wake Linda Shuma wa shirika la Women and Girls Empowerment CBO, amesema kuna haja ya wanawake kushiriki katika michezo ya majini, utalii na usafiri wa baharini ili kuchangia katika ukuaji wa uchumi.