News
UEFA:Inter Ndaani Ya Fainali

Miamba wa Italia kilabu ya Inter Milan imekua ya kwanza kutinga awamu ya fainali kilabu bingwa Ulaya baada ya kunyuka FC Barcelona kichapo cha magoli 4-3 na jumla ya magoli 7-6 uwanjani San Siro jana usiku.
Inter walitangulia kucheka na wavu kunako dakika ya 21 kupitia kwa mshambulizi Lautaro Martinez dakika ya 21 kabla ya kiungo Hakan Çalhanoğlu kuweka kambani goli la pili dakika ya 46 kipindi cha kwanza.
Hata hivyo Barcelona walirejea kwa moto wa radi kipindi cha pili na kusawazisha la kwanza kunako dakika ya 54 kupitia beki Erick Garcia naye mshambulizi Dani Olmo akiweka la pili dakika ya 60.
Licha ya Barcelona kuchukua uongozi dakika ya 87 kupitia kwa mahambulizi Raphinha, Inter walisawazisha kupitia kwa beki Fransisco Acerbi dakika ya 93 na kupeka mechi hiyo kwenye muda wa ziada ama extra time ukipenda.
Kiungo mshambulizi na nguvu mpya Davide Fratessi alifunga goli la ushindi la Inter dakika ya 99 na kupeleka kilabu hiyo kwenye fainali Alianz Arena Mei 31.
Hii leo ni zamu ya mabingwa wa ufaransaPSG kutifua kivumbi na Arsenal uwanjani Parc de prince.
News
Mahakama kuu yatupilia mbali ombi la Gachagua

Mahakama kuu imetupilia mbali ombi la pili la aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua la kutaka jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi ya kupinga kubanduliwa wake mamlakani kuzuiliwa kuskiza kesi hiyo.
Gachagua alisema kwamba majaji hao watatu akiwemo Jaji Eric Ogola, Anthony Mrima na Fridah Mugambi wanafaa kuondolewa kwenye kesi hiyo kwa misingi kwamba uteuzi wao haujazingatia sheria.
Mahakama hiyo ilitupilia mbali ombi hilo, na kusema kwamba jopo hilo la majaji watatu liliteuliwa na Jaji mkuu Martha Koome kwa kuambatana na sheria na kanuni za idara ya Mahakama.
Mahakama imeshikilia kwamba jopo hilo la majaji wa Mahakama kuu litaendelea kusikiliza kesi hiyo hadi wakati wa kutoa uamuzi kwa kuzingatia sheria, na kanuni za idara ya Mahakama pamoja na Katiba ya Kenya.
Mahakama hiyo pia ilitupilia mbali ombi la Mwanaharakati Fredrick Mula ambaye alitaka kubadilishwa kuwa mlalamishi katika kesi nne za kuondolewa mashtaka dhidi ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ambazo alikuwa amewasilisha awali na kisha kutaka kujiondoa.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Wazee wa Kaya wanataka bunge kupitisha sheria kudhibiti mauaji ya wazee

Muungano wa Wazee wa Kaya kaunti ya Kilifi umeitaka serikali kuu kupitia bunge la kitaifa kubadilisha sheria ya mwaka wa 1926 kuhusu uchawi ili kuwezesha utamaduni kudhibiti mauaji ya wazee yanayoendelea kushuhudiwa kaunti ya Kilifi.
Wakiongozwa na Stanley Kahindi Kiraga wamesema kuwa sheria hiyo imechangia pakubwa mauaji ya wakongwe Kilifi kutokana na swala kuwa haitambui uwepo wa uchawi na jinsi ya kuudhibiti.
Kiraga sasa anasema ni sharti sheria hiyo iondolewe au ifanyiwe ukarabati bungeni hali itayopelekea uchawi kudhibitiwa kupitia mila na utamaduni.
“Vijana wanaowaua wazee wakiwasingizia kuwa wachawi wanazidi kuongezeka na kwa sababu hakuna sheria ya moja kwa moja ya kuwashtaki na kuwafunga” amesema Kiraga akieleza kusikitishwa kwake na ongezeko la magenge ya vijana wanaolipwa kutekelezwa mauaji ya wazee kwa shutuma za uchawi.
Taarifa ya Hamis Kombe