National News
Shahidi wa 28 na 29 Waelezea Mahakama Masaibu Waliyopitia Shakahola

Kesi inayomhusu Mhubiri tata Paul Mackenzie na wenzake 92 imesikizwa katika Mahakama ya Mombasa, ambapo shahidi wa 28 na 29 wameeleza ushahidi wao Mahakamani.
Shahidi wa 28, ambaye ni mtoto ametoa ushahidi wake katika chumba cha faraga ambapo amesema kwamba alikamatwa na maafisa wa polisi pamoja na familia yake baada ya wazazi wake kuwaachisha shule kutokana na mafunzo ya Mackenzie.
Mtoto huyo ameeleza kwamba baba yake alikuwa akipinga mafunzo ya Mackenzie lakini baadaye alijiunga na kisha kuhamia Shakahola na familia yake ambapo alishuhudia Mackenzie akikusanya watu na kuwaagiza kufunga kula na kunywa, kabla ya kufanikiwa kutoroka hadi kituo cha watoto huko Watamu.
Kwa upande wake Shahidi wa 29, ameiambia Mahakama hiyo kwamba alipoteza watoto wake 7 kutokana na kufunga kula na kunywa, akisema walinzi waliokuwa wakilinda eneo hilo walichukua chakula chake chote kilichokuwa nyumbani kwao.
Shahidi huyo amesema wakati huo alikuwa mjamzito na alilazimika kufunga ili kuua mtoto aliyekuwa tumboni na wafuasi wa Mackenzie walikuwa hawaruhusiwi kuomboleza kifo chochote katika eneo hilo la Shakahola.
Mackenzie na wenzake 92 wanakabiliwa na mashtaka 238 ikiwemo mauaji ya halaiki, ugaidi, mafunzo ya itikadi kali miongoni mwa mashtaka mengine yanayodaiwa kuyatekeleza kati ya mwaka 2020 na 2023 katika msitu wa Shakahola kaunti ya Kilifi.
Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa mbele ya Hakimu mkuu Alex Ithuku.
National News
Kesi ya Lissu kusikilizwa katika Mahakama ya Masjala Ndogo

Kiongozi wa upinzini nchini Tanzania Tundu Lissu, anapandishwa kizimbani katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo mjini Dar es Salaam, kwa ajili ya kesi ya uhaini inayomkabili kwa ajili ya usikilizwaji wa awali (preliminary hearing – PH).
Kesi ya Lissu ambaye pia ni kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ilipangwa kusikilizwa siku Jumatatu Agosti 8, 2025 katika Mahakama hiyo na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru lakini ilihairishwa
Lissu, alikamatwa mwezi Aprili na kushtakiwa kwa uhaini, shtaka ambalo iwapo akikutwa na hatia hukumu yake ni kifo, kutokana na kudaiwa kutoa wito kwa wafuasi wake kuzuia uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Kesi ya Lissu imekuwa ikifuatiliwa na mataifa ya kigeni zikiwemo nchi za Ulaya.
Taarifa Ya Elizabeth Mwende
National News
Maafisa 8 wa polisi wajeruhiwa Garissa

Takriban maafisa wanane wa polisi wamejeruhiwa kwenye shambulizi la kigaidi ambapo gari walilokuwa wakisafiria kukanyaga kilipuzi katika barabara ya Banabs-Yumbis kaunti ya Garissa.
Duru kutoka idara ya polisi zilisema kundi la maafisa hao walikuwa wakisafiri kutumia gari la kijeshi lenye uwezo wa kuhimizi mabomu- Mine Resistant Ambush Protected (MRAP) wakati wa tukio hilo.
Hii ni baada ya kikosi cha maafisa wa kuweka usalama mipakani kukabiliana kwa risasi na washukiwa wa ugaidi wanaoaminika kuwa wanamgambo wa kundi la alshabab.
Magaidi hao wanaaminika waliweka bomu la kutegwa ardhini.
Taarifa hiyo ilisema gari la polisi aina ya Land Cruiser lililokuwa na maafisa zaidi limefika eneo la tukio kuwaokoa maafisa wenzao ambao walikuwa wamekwama ndani ya gari hilo la MRAP.
Maafisa hao wamepata majeraha mabaya na kupelekwa katika hospitali iliyokaribu kwa matibabu ya dharura ambapo baadaye watafasirishwa kwa ndege hadi jijini Nairobi.
Polisi eneo hilo wamesema magaidi wamefanikiwa kutoroka eneo la tukio japo wakiibua hofu kuwa huenda wako karibu na eneo hilo linalokabiliwa na tishio la usalama.
Mpaka wa Kenya na Somalia unasalia kuwa hatari na imekuwa rahisi kwa magaidi kupenya nchini.
Taarifa ya Joseph Jira