News
Serikali kutumia AI katika utoaji wa huduma kwa umma

Waziri wa utumishi wa Umma nchini Geoffrey Ruku anasema serikali inaangazia kuwianisha mishahara ya watumishi wa umma na kukumbatia mageuzi ya kidijitali, ikiwa ni pamoja na matumizi ya mfumo wa akili mnemba (AI), ili kuboresha ufanisi katika utoaji huduma.
Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga toleo la 44 la michezo ya shirika la michezo ya huduma za kiraia nchini (KECOSO) katika uwanja wa Moi mjini Embu, Ruku aliekiri kuwepo tofauti za malipo katika sekta ya umma na kusema mageuzi yanaendelea.
Waziri huyo aliwapongeza watumishi wa umma kwa kujitolea katika utendakazi wa, akisema Kenya ina mojawapo ya wafanyakazi wenye nguvu zaidi katika utumishi wa umma barani afrika.
Ruku pia aliangazia mkakati wa serikali wa kidijitali-kwanza unaoongozwa na wizara ya mawasiliano, akisema mfumo wa AI na zana za kidijitali zitakuwa muhimu katika kubadilisha utendakazi.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Mahakama ya Kilifi imetoa hukumu kwa wanaume 6 wanaokabiliwa na mashtaka ya unajisi

Mahakama ya Kilifi imetoa hukumu kwa wanaume 6 wanaokabiliwa na mashtaka ya unajisi.
Hakimu wa Mahakama hiyo Ivy Wasike alimhukumu Lucky Munga na Hassan Daniel kifungo cha miaka 30 gerezani baada ya Mahakama kubaini kwamba walihusika kwa kuwatendea unyama watoto wa umri wa miaka 13 na 15.
Safari Karisa Lewa alihukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani kwa kumnajisi mtoto wake mwenyewe wa umri wa miaka 14 huku Eric Ruwa na Lucky Katana Kenga wakihukumiwa kifungo cha miaka 6 gerezani kwa kosa sawa na hilo.
Hata hivyo Mahakama hiyo ilimhukumu kifungo cha miaka 3 Kithi Kombe kutokana na kesi hiyo kwa mtoto wa miaka 15, japo baadaye Mahakama ikabaini kwamba mshukiwa sio baba halali wa mtoto aliyezaliwa baada ya Kithi kumnajisi mtoto huyo.
Akizungumza wakati wa vikao vya Mahakama baada ya kutoa hukumu hizo, Hakimu Wasike alisema Mahakama umezingatia ushahidi uliyotolewa Mahakamani huku akiwarai wananchi kujitenga na visawishi vibaya ili kuepuka mkono wa sheria.
Hakimu Wasike alihoji kwamba washtakiwa wa haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama lakini kwa kuzingatia taratibu zote za Mahakama na sheria.
Taarifa ya Teclar Yeri
News
Thoya: Serikali kuu iongeze mgao wa fedha kwa sekta ya Afya

Naibu gavana wa kaunti ya Mombasa Francis Thoya ametoa changamoto kwa serikali kuu kuongeza mgao wa fedha ili kufanikisha utaoji wa huduma za afya.
Akizungumza katika kaunti hiyo, Thoya alisema kuwa huduma nyingi za afya katika kaunti hiyo ya Mombasa zinakabiliwa na changamoto ya raslimali ndogo hali ambayo inakwamisha juhudi za kuwahudumia wananchi ipasavyo.
Thoya pia alitaka serikali kuhakikisha inaharakisha kuajiri wahudumu zaidi wa afya ili wenyeji wa Mombasa waweze kupata huduma bora za matibabu bila changamoto zozote.
Aidha, Thoya alisema kwamba hali ya uhaba wa wahudumu wa afya ni changamoto kuu ambayo inazuia utoaji wa huduma bora za matibabu hali inayowafanya wale wachache waliopo kufanya kazi katika mazingira magumu.
Taarifa ya Janet Mumbi