News
Serikali kukabiliana na magenge ya uhalifu nchini

Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen ameonya kuhusu kuongezeka kwa magenge ya wahalifu nchini.
Akizungumza katika kongamano la Jukwaa la Usalama kaunti ya Vihiga, Waziri Murkomen alitoa wito kwa inspekta jenerali wa polisi kutuma vikosi zaidi vya dharura eneo hilo ili kuwasambaratisha wahalifu hao.
Magenge ya wahalifi yamekuwa yakiripotiwa kuhangaisha usalama na maisha ya wakaazi katika sehemu mbali mbali nchini ikiwepo kaunti za hapa Pwani.
Kwa upande wake gavana wa kaunti ya Kilifi Gedion Mung’aro aliahidi kushirikiana kwa karibu na maafisa wa usalama kukomesha magenge ya wahalifu yanayowahangaisha wakaazi maarufu mawoza.
Akizungumza mjini Malindi katika kaunti ya Kilifi kwenye mkutano na vijana wa eneo hilo, gavana Mung’aro alisema serikali yake haitawavumilia vijana waliopotoka kimaadili wanaoendelea kuwahangaisha wananchi.
Wakati huohuo aliwaonya baadhi ya maafisa wa kaunti wanaowahangaisha wakaazi hususan wahudumu wa bodaboda.
Taarifa ya Joseph Jira.
News
Waziri wa zamani Dalmas Otieno Afariki

Mbunge wa zamani wa eneo bunge la Rongo Dalmas Otieno ameaga dunia.
Kiongozi huyo shupavu na mweledi katika uzungumzaji, ameaga dunia Septemba 7, 2025 nyumbani kwake katika mtaa wa Kileleshwa jijini Nairobi.
Marehemu ambaye aliwahi shikilia Wizara mbalimbali nchini pamoja na taasisi za umma muhimu kuanzia utawala wa Rais wa pili nchini Hayati Daniel Arap Moi katika miaka ya 80 atakumbukwa na wengi kwa mchango wake nchini.
Taarifa za Kifo chake zimetolewa na mwanawe Eddy Otieno.
Otieno alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuingia bungeni na kuwaakilisha eneo bunge la Rongo mnamo mwaka 1988, na kisha baadaye kuhudumu kama Waziri wa ustawi wa viwanda kati ya 1988-1991.
Mwaka wa 1991 aliteuliwa kuwa Waziri wa Leba, lakini pia akahudumu kama Waziri uchukuzi na mawasiliano chini ya utawala wa Rais Daniel Toroitich Arap Moi.
Viongozi mbalimbali wakiongozwa na Spika wa bunge la kitaifa Moses Wetangula wametaka Mwendazake kama kiongozi alichagia mengi nchini hasa suala zima la maendeleo na miswada muhimu bungeni.
Mungu ailaze roho yake pema Peponi.
Taarifa ya Eric Ponda
News
Baraza la vyombo vya habari MCK lakerwa na baadhi ya vyombo habari

Baraza la vyombo vya habari nchini MCK limeeleza kusikitishwa na hatua ya baadhi ya vyombo vya habari nchini kumwingilia rais wa chama cha mawakili LSK Faith Odhiambo baada ya kukubali kujumuishwa kwenye kamati ya kuangazia fidia kwa waathiriwa wa maandamano nchini.
MCK ilisema hatua ya Odhiambo kujumuishwa katika kamati hiyo kuhakikisha waathiriwa wa maandamano hayo wanapata haki kwa mujibu wa sheria.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, baraza hilo lilipongeza juhudi za vyombo vya habari kwa kuangazia kwa undani maandamano yaliyofanyika nchini na hata baadhi ya wanabari kujitokeza kutoa ushahidi mahakamani.
MCK ilisema hatua ya baadhi vyombo vya habari kukosoa mwelekeo wa Odhiambo kunaiweka LSK katika hatari ya ukosoaji zaidi, katika juhudi za kuangazia usawa kwenye maswala ya uongozi dhabiti nchini.
Taarifa ya baraza la vyombo vya habari nchini MCK.
Ilieshinikiza wakenya kufahamu kuwa chama cha LSK kinaongozwa na taasisi muhimu za umma ikiwepo idara ya mahakama, ofisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma, ofisi ya mkuu wa sheria nchini vile vile tume ya malalamishi kwa vyombo vya habari.
MCK ilivitaka vyombo vya habari kumruhusu Odhiambo kuendelea kutekeleza majukumu yake bila muingilio katika kamati hiyo.
Taarifa ya Joseph Jira