Entertainment
Ronald Fenty, Baba wa Rihanna, Afariki Dunia Akiwa na Miaka 70

Mwanamuziki maarufu duniani, Rihanna, anaomboleza kifo cha baba yake mpendwa, Ronald Fenty, aliyefariki dunia Mei 31, 2025 huko Los Angeles, Marekani, akiwa na umri wa miaka 70, baada ya kuugua kwa kipindi kifupi.
Taarifa hizo za kuhuzunisha ziliripotiwa kwa mara ya kwanza na kituo cha habari cha Starcom Network cha Barbado.
Ingawa chanzo rasmi cha kifo bado hakijatangazwa, vyanzo vya karibu vimeripoti kuwa Fenty aliaga dunia akiwa amezungukwa na familia yake, wakiwemo Rihanna pamoja na kaka yake mdogo Rajad Fenty, katika Hospitali ya Cedars-Sinai wakati wa saa zake za mwisho.
Kwa mujibu wa TMZ, Rajad alionekana akifika hospitalini mnamo Mei 28, na inadaiwa kuwa Rihanna pia alikuwa kwenye gari hilo, japokuwa hakuonekana kwenye picha.
Ronald Fenty alizaliwa mwaka 1954 huko Barbados na alikuwa msimamizi wa ghala. Alikuwa baba wa watoto sita, wakiwemo Rihanna (jina kamili Robyn Rihanna Fenty), Rajad, na Rorrey, aliowapata na aliyekuwa mke wake Monica Braithwaite, ambaye walitalikiana mwaka 2002.
Aidha, Fenty alikuwa na watoto wengine watatu—Samantha, Kandy, na Jamie—kutoka mahusiano ya awali. Familia ya Rihanna iliishi maisha ya kawaida katika nyumba ya kupangisha eneo la Bridgetown, ambalo sasa linajulikana kama Rihanna Drive. Ingawa uhusiano wa Rihanna na baba yake ulikuwa na changamoto nyingi, Fenty alihusika pakubwa katika kuhamasisha kipaji chake cha muziki tangu akiwa mdogo.
Kwa sasa, mashabiki, watu mashuhuri, na familia ya karibu wanaendelea kumpa Rihanna pole na kumfariji wakati huu wa huzuni kuu.
Entertainment
Lisemwalo Lipo, Apewe Nafasi Afunguke, Kaa la Moto Amkingia Kifua Kelechi Afrikana

Msanii nguli wa muziki Afrika Mashariki, Kaa la Moto, amekingia kifua kauli ya msanii mwenzake Kelechi Africana aliyedai kuwa “kinachowafelisha wanamuziki wa Mombasa ni ukahaba.”
Akizungumza na meza ya burudani ya Coco FM, Kaa la Moto alieleza kuwa anaamini nia ya Kelechi si ya kubeza bali ya kutaka kuona mabadiliko chanya kwenye tasnia ya muziki kutoka ukanda wa Pwani.
“Ameona ndio maana anayakemea,” alisema Kaa la Moto kwa utulivu.
“Naamini kwamba ana ufahamu sahihi, na pia naamini kuwa ni kijana ambaye anataka maendeleo ya sanaa kutoka mkoa wake. Kwa hiyo watu walipatie fikra—kwa sababu lisemwalo lipo. Labda ana kitu, akipewa nafasi atazungumza zaidi.”
Kauli ya Kelechi ilizua hisia mseto mitandaoni baada ya kupachikwa kwenye ukurasa wake wa Facebook, ambapo aliandika: “Kinacho felisha wanamuziki wa Mombasa ni ukahaba.”
Wengine waliona ni matusi kwa jumuiya ya wasanii, lakini kwa Kaa la Moto, ilikuwa ni hoja yenye mzizi wa ukweli. Alisisitiza kuwa hakuna hoja inayopaswa kupuuzwa kabla ya kueleweka kwa undani.
“Sipingi hoja yake kwa sababu kila hoja ipo huru kwa aliyeifikiria na kuiwaza. Naamini anajaribu kuinspire vijana wenzake,” aliongeza Kelechi.
Katika mazungumzo hayo, Kaa la Moto pia alitumia fursa hiyo kueleza kinachomuweka relevant kwenye muziki licha ya mabadiliko ya ladha, mitindo, na majina mapya kwenye game kila mwaka.
“Kitu ambacho kimeniweka hadi leo ni nidhamu. Nidhamu kwenye maisha, kwenye kazi, kwenye watu,” alisema kwa msisitizo.
Baadhi ya mashabiki waliopena maoni yao kwenye post ya Kelechi walisema;
Tamara Black, “Shida tu unaingililia watu hawana shughuli yako.Put that effort in Use ututolee kazi kali umbea achia watoto wa kike.”
Raisi Wakitaa, “Apo umenena nimepata mwenzangu sasa wakusema ukweli wanaboesha Sana Kwanza uyo my wife ndo kabisa simuelewi kila siku post ya mtu mmoja demu mwenyewe alishaliwa na wahuni toka enzi za shule .”
D Jay Ricious,”Wapashe adi wagutuke maana tulio chini ni huko juu ndio twaja kwa nafasi zetu. #coast music occupy kenya .”
Hamza Ahmed Lama, “Acha kutafuta Kiki’kai anapiga hela na anamadili kibao.”
Knasty Snaty, “Wew nawew wataka dera kazi yako ni umbea tu acha mziki uanze umbea.”
Entertainment
Chris Brown Akanusha Shtaka la Kumshambulia Producer kwa Chupa

Msanii nyota wa Marekani, Chris Brown, amekana mashtaka mawili mahakamani yanayohusiana na madai ya shambulio kwa kutumia chupa katika kilabu cha usiku jijini London miaka miwili iliyopita.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 36 anatuhumiwa kumsababishia mtayarishaji wa muziki majeraha ya mwili katika tukio ambalo waendesha mashtaka wamelieleza kuwa “halikuwa na uchochezi wowote”.
Pia anakabiliwa na shtaka la kumiliki silaha hatari — ambayo ni chupa ya kileo.
Mashtaka haya mawili yaliongezwa mwezi uliopita kwenye shtaka la awali, kubwa zaidi, la kujaribu kumsababishia mtu majeraha mabaya ya mwili (GBH), ambalo tayari Bwana Brown alilishatupilia mbali kwa kujitetea kuwa si kweli.
Chris Brown anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa kesi hiyo mwezi Oktoba mwaka 2026.
Waendesha mashtaka wamesema kuwa mhanga wa tukio hilo, Abraham Diaw, alikuwa amesimama kwenye baa ya kilabu cha usiku kilichopo eneo la Soho mnamo tarehe 19 Februari 2023, wakati Chris Brown alimpiga kwa chupa mara kadhaa.
Mwimbaji huyo alikamatwa mwezi Mei katika hoteli ya nyota tano iliyopo Salford, Greater Manchester, baada ya kurejea Uingereza kwa ajili ya maandalizi ya ziara yake ya muziki barani Ulaya.
Alizuiliwa korokoroni kwa takriban wiki moja kabla ya kuachiliwa kwa dhamana baada ya kukubali kulipa ada ya dhamana ya pauni milioni tano (£5m) kwa mahakama.
Ada ya dhamana ni kiasi cha fedha kinachowekwa kama dhamana ya kifedha kuhakikisha mtuhumiwa atarudi mahakamani kwa kesi yake. Brown anaweza kupoteza fedha hizo endapo atakiuka masharti ya dhamana, ambayo yaliendelezwa katika kikao cha mahakama siku ya Ijumaa.
Kwa mujibu wa masharti hayo, Chris Brown anatakiwa kuishi katika anwani iliyopo Uingereza akisubiri kesi hiyo, na aliamriwa kukabidhi pasipoti yake kwa polisi.
Hata hivyo, ameruhusiwa kuendelea na ratiba ya ziara yake ya kimataifa ya Breezy Bowl XX kwa masharti kwamba atakabidhi pasipoti kila anapomaliza safari, na kuirudishiwa anapohitaji kusafiri kwa ajili ya maonesho.
Katika wiki za hivi karibuni, Brown amekuwa akitumbuiza kwenye viwanja na kumbi mbalimbali za burudani kote Uingereza na Ulaya, na kumaliza burudani mjini Paris mwishoni mwa wiki iliyopita. Sehemu ya ziara hiyo inayofanyika Marekani Kaskazini inatarajiwa kuanza baadaye mwezi huu na kufikia tamati tarehe 18 Oktoba.
Kikao kingine cha mahakama kimepangwa kufanyika tarehe 24 Oktoba.
Chris Brown ni miongoni mwa wanamuziki wakubwa zaidi wa R&B nchini Marekani, akiwa mshindi wa tuzo mbili za Grammy na nyimbo 19 zilizofika katika nafasi 10 za juu kwenye chati za Uingereza, zikiwemo Turn Up The Music, Freaky Friday, With You na Don’t Wake Me Up.
Mshitakiwa mwenza, Omololu Akinlolu, raia wa Marekani mwenye umri wa miaka 39 anayefahamika kisanii kama HoodyBaby, naye pia alikana shtaka la kumsababishia mtu majeraha ya mwili. Awali, alikana pia shtaka la kujaribu kusababisha majeraha mabaya ya mwili.
Chanzo: BBC