News
Rais Ruto: Mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu utaendelea

Rais William Ruto amesema lengo kuu la serikali ya Kenya kwanza ni kuhakikisha wakenya wananufaika kimaendeleo na wala sio siasa za vurugu na migawanyiko.
Rais Ruto alisema mpango wa kujenga nyumba za bei nafuu katika maeneo mbalimbali nchini utaendelea ili kuhakikisha wakenya wanamudu gharama ya maisha kwani watakuwa na nafasi nzuri kwenye makaazi bora.
Akizungumza jijini Nairobi, Rais Ruto alisema viongozi wengi wamebali kushirikiana na serikali akiwemo Kinara wa Chama cha ODM Raila Odinga ili kuhakikisha wakenya wanafaidi na raslimali zao.
Kiongozi wa nchi, aliweka wazi kwamba atahakikisha miradi yote ya maendeleo nchini inatekelezwa kupitia ushirikiano wa viongozi na wananchi, huku akiwakosoa wale wanajaribu kurudisha nyuma juhudi za maendeleo.
“Tuko na mpango wa kujenga nyumba za bei nafuu kwani wananchi wetu, watu wengi wanaisha katika nyumba duni na alisema hii maneno tutafanya hata wale wengine waongee maneno mengi mimi nitahakikisha natekeleza jukumu langu”, alisema rais Ruto.
Wakati uo huo aliahidi wakenya kwamba serikali itaendelea na mpango wake wa bima ya afya ya jamii SHA, ili kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini wanapata matibabu bila ya kuanganishwa huku akiwarai wakenya kujisajili na SHA.
“Kila mkenya ni lazima apate matibabu kwa gharama ya chini ndio tunasema ni vuzuri wakenya wajisajili katika SHA na tayari wale ambao waliweza kujisajili wameona manufaa ya SHA na kweli tumesajili watu zaidi ya milioni 20”, aliongeza Rais.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Godhana, awataka wakaazi kutoingiza siasa miradi ya maendeleo

Gavana wa kaunti ya Tana River Dhadho Godhana amewataka wenyeji wa kaunti hiyo kujiepusha na wanasiasa ambao wanaingiza siasa kwenye masuala ya maendeleo.
Godhana alisema hilo limechangia kaunti ya Tana River kusalia nyuma kimaendeleo hali ambayo itasababisha miradi mingi kuzidi kukwama.
Godhana alisema ni lazima viongozi na wenyeji wa kaunti ya Tana River washirikiane na uongozi wa kaunti ili kuafikia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Wakati huo huo Godhana aliesema mradi wa Village Cluster ambao umekuwa ukipingwa ndio utakaosaidia kudhibiti changamoto ambazo zinaikumba kaunti ya Tana River.
Naye Mahat Ali Loka ambaye ni Naibu Gavana wa kaunti ya Tana River, aliwaonya wanasiasa kutoka kaunti zingine dhidi ya kuingilia siasa za kaunti hiyo huku Spika wa bunge la kaunti hiyo Osman Noor Galole, akitoa onyo kwa wafanyikazi wa umma dhidi ya kujumu la serikali ya kaunti ya Tana River.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Mwili wapatikana baharini Shelly Beach Likoni

Polisi kaunti ya Mombasa wanachunguza kisa ambapo mwili wa mwanamme ambaye hajafahamika umepatikana ukielea katika maji ya bahari hindi kwenye ufuo wa Shelly Beach eneo bunge la Likoni.
Ripoti ya polisi ilibaini kuwa mwili huo uligunduliwa na wavuvi eneo hilo, ambao walipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Shelly Beach kuhusiana na tukio hilo.
Polisi walisema hawakubaini mara moja anakotoka mtu huyo.
Vile vile haikubainika iwapo marehemu alizama au aliuawa kabla ya mwili wake kutupwa baharini.
Polisi walisema hawajakutana na stakabadhi zozote za kumtambulisha mtu huyo huku wakiwasihi wananchi kutoa taarifa iwapo wanafahamu familia ya marehemu.
Mwili unahifadhiwa katika hifadhi ya maiti katika hospitali ya Rufaa ya Coast General Mombasa wakati uchunguzi zaidi ukiendelea.
Taarifa ya Joseph Jira