News
Rais Ruto, Amteua Ethekon kuwa Mwenyekiti wa IEBC

Rais William Ruto amemteua Erastus Edung Ethekon kuwa Mwenyekiti wa Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC na makamishna 6 wa tume hiyo ili kufanikisha shughuli za uchaguzi nchini.
Katika chapisho la gazeti rasmi la serikali, Rais Ruto amezingatia kipengele cha 250 ibara ya pili {a} ya Katiba ya Kenya na mwongozo wa uteuzi wa makamishna wa sehemu ya 5 na 7 na kutekeleza jukumu hilo.
Katika chapisho hilo lililotiwa saini na Mkuu wa utumishi wa umma nchini Felix Koskei, Rais amezingatia muongozo wa Katiba na kuwateua makamishna 6 wa tume hiyo akiwemo Ann Njeri Nderitu kutoka kaunti ya Nyandarua, Moses Alutalala Mukhwana kutoka kaunti ya Kakamega na Mary Karen Sorobit kutoka kaunti ya Uasin Gishu.
Wengine ni pamoja na Hassan Noor Hassan kutoka kaunti ya Mandera, Francis Odhiambo Aduol kutoka kaunti ya Kisumu pamoja na Fahima Araphat Abdallah kutoka kaunti ya Lamu.
Sasa majina ya makamishna hao na Mwenyekiti mpya wa IEBC yatawasilishwa bungeni kupigwa msasa na kuidhinishwa kabla ya kuapishwa ili kuanza majukumu yao ya kikazi.
News
Wazee wa Kaya wanataka bunge kupitisha sheria kudhibiti mauaji ya wazee

Muungano wa Wazee wa Kaya kaunti ya Kilifi umeitaka serikali kuu kupitia bunge la kitaifa kubadilisha sheria ya mwaka wa 1926 kuhusu uchawi ili kuwezesha utamaduni kudhibiti mauaji ya wazee yanayoendelea kushuhudiwa kaunti ya Kilifi.
Wakiongozwa na Stanley Kahindi Kiraga wamesema kuwa sheria hiyo imechangia pakubwa mauaji ya wakongwe Kilifi kutokana na swala kuwa haitambui uwepo wa uchawi na jinsi ya kuudhibiti.
Kiraga sasa anasema ni sharti sheria hiyo iondolewe au ifanyiwe ukarabati bungeni hali itayopelekea uchawi kudhibitiwa kupitia mila na utamaduni.
“Vijana wanaowaua wazee wakiwasingizia kuwa wachawi wanazidi kuongezeka na kwa sababu hakuna sheria ya moja kwa moja ya kuwashtaki na kuwafunga” amesema Kiraga akieleza kusikitishwa kwake na ongezeko la magenge ya vijana wanaolipwa kutekelezwa mauaji ya wazee kwa shutuma za uchawi.
Taarifa ya Hamis Kombe
News
Mahakama ya Kilifi yaanzisha upya kesi ya ulaghai wa pesa

Mahakama ya Kilifi imeanzisha upya kesi ya mwanaume mmoja anayekabiliwa na shtaka la ulaghai wa pesa.
Hii ni baada ya Mwanaume huyo kwa jina Samuel Ngonyo, kuachiliwa kwa dhamana hapo awali lakini alikosa kudhuhuria vikao Mahakamani hali iliyopelekea kesi hiyo kuanzishwa upya.
Hakimu mkuu wa Mahakama hiyo Charles Obulutsa aliagiza jamaa huyo kuzuliwa rumande baada ya agizo la kukamatwa kwake kuidhinishwa na Mahakama baada ya jamaa huyo kupuuza vikao vya Mahakama vya awali.
Kabla ya agizo hilo, Mahakama ilielezwa kwamba mnamo tarehe tofauti kati ya mwezi Septemba hadi Oktoba mwaka 2021 katika maeneo la Ganze kaunti ya Kilifi kwa kutumia njia ya ulaghai, mshukiwa alichukua pesa taslimu shilingi elfu 50 ya mlalamishi Grace Sidi Katana.
Mahakama ilielezwa zaidi kwamba mshukiwa alitekeleza kitendo hicho baada kumdanganya Mlalamishi kwamba yeye ni Mwandishi na afisa wa kazi za umma hivyo angemsaidia Moses Katana mtoto wa mlalamishi kupata kazi ya serikali.
Kesi hiyo itaendelea mnamo tarehe 13 mwezi Agosti mwaka huu.
Taarifa ya Mwanahabari wetu