News
Polisi:Mauaji ya wazee Kaloleni-Kilifi yamedhibitiwa

Naibu Kamishna wa kaunti ndogo ya Kaloleni kaunti ya Kilifi, Kyalo Kaloki amewapongeza wenyeji kwa juhudi ambazo wamekuwa wakiweka kudhibiti mauaji ya wazee kwa tuhuma za uchawi.
Kaloki ambaye alikuwa akizungumza katika eneo la Gotani, wadi ya Kayafungo, aliitaka jamii eneo hilo pia kushirikiana na afisi za machifu ili kupata mwafaka wa migogoro ya mashamba ambayo imekithiri maeneo hayo.
Kaloki pia alisema maafisa wa polisi wamekuwa wakipokea kesi za mashamba kwa wingi.
Vilevile, Kaloki alisema ni kupitia ushirikiano ndipo mizozo ya ardhi itadhibitiwa vilivyo.
“Sasa ile kesi naomba tupunguze pia ni kesi ya mashamba,mkikosana na jirani yako hapana kukimbia kwa kituo cha polisi, eti unaenda kumshtaki amekutishia maisha, Ita wazee wenzenu, kaeni chini mtatue’’, alisema Kaloki.
Eneo la pwani limekuwa kishuhudia visa vya wazee kuawa kwa tuhuma za ushirikina, huku baadhi yao wakilazimika kukimbilia usalama wao katika makao ya kuhifadhi wazee.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Philip Charo ateuliwa kaimu waziri wa barabara Kilifi

Gavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Mung’aro amefanya mabadiliko katika serikali yake na kumteua afisa mkuu mtendaji wa idara ya barabara Philip Charo kuwa kaimu waziri katika idara ya barabara.
Hii ni baada ya kuchaguliwa kwa aliyekuwa waziri wa idara hiyo Catherine Kenga kuwa spika wa bunge la kaunti ya Kilifi.
Katika taarifa kupitia msemaji wa kaunti Johnathan Mativo, afisa mkuu mtendaji wa idara ya maswala ya fedha Hezekiah Mwaruwa pia aliteuliwa kuwa afisa mkuu mtendaji katika ofisi ya gavana.
Mativo alisema kwamba mabadiliko hayo yanaanza kutekelezwa mara moja ingawa ni ya mda.
Catherine Kenga alijiunga na utumishi wa serikali ya kaunti ya Kilifi mnamo mwaka 2023 baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 uliopelekea kuchaguliwa kwa gavana Gideon Maitha Mung’aro.
Pia amewahi kuhuduma kama kaimu katibu wa kaunti baada ya kutimuliwa kwa Martin Mwaro.
Catherine Kenga alichaguliwa kuwa spika wa bunge la kaunti ya Kilifi katika kikao maalum ambacho kiliandaliwa katika bunge hilo Jumatu Julai 21 2025.
Kenga anachukua hatamu ya kuliongoza bunge hilo kutoka kwa aliyekuwa spika Teddy Mwambire ambaye alitimuliwa mapema mwezi uliopita Juni 30, 2025 kupitia kura ya maoni.
Mwambire alibanduliwa kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na ukiukaji wa katiba.
Taarifa ya Joseph Jira
News
11 wazuiliwa rumande Malindi kwa madai ya Uhalifu na ugaidi

Mahakama mjini Malindi kaunti ya Kilifi iliwaamuru washukiwa 11 waliokamatwa katika kijiji cha Kwa Binzaro kilomita sita kutoka eneo la Shakahola kuzuiliwa rumande kwa mda wa siku 30 ili kuruhusu uchunguzi zaidi.
11 hao walikamatwa baada ya kuhusishwa na madai ya uhalifu, ugaidi na kwenda msituni na watoto.
Awali polisi ilitangaza kupata mwili mmoja na mafuvu mawili ya binadam kwenye nyumba moja katika kijiji hicho.
Kulingana na polisi watu wanne waliokolewa katika oparesheni hiyo.
Kamishna wa kaunti ya Kilifi Josephat Biwot alisema oparesheni hiyo iliyohusisha wakaazi, watu watatu kati ya wanne waliookolewa walionekana wakiwa dhaifu kuliko hali yao ya kawaida.
Biwot alidokeza kuwa wahusika hawakupatikana nyumbani wakati wa oparesheni hiyo na haikubainika kilichokuwa kikiendelea.
Eneo la Shakahola kaunti ya Kilifi liligonga vichwa vya habari baada ya kugunduliwa makaburi ya halaiki yaliyomhusisha mhubiri tata Paul Mackenzi ambaye kwa sasa anaendelea kuzuiliwa rumande pamoja na washirika wake wakati kesi ikiendelea.
Mwili na mafuvu hayo yalipelekwa katika hifadhi ya maiti katika hospitali ya kaunti ndogo ya Malindi.
Taarifa ya Joseph Jira