Entertainment
Diamond Platnumz: Nilishawahi Kuoa, na Kuna Siku Nitawaambia Ikawaje
Kauli ya Diamond Platnumz kuhusu ndoa imewavuruga mashabiki mitandaoni, baada ya picha zenye taswira ya harusi kusambaa. Ingawa hajasema wazi kama ameoa, ujumbe wake wa kina kuhusu kukaa kimya na uvumilivu umeacha maswali mengi kuliko majibu. Je, Diamond ameoa kwa siri? Au ni ujanja wa kisanii?

Kauli ya msanii nyota na mfanyabiashara mashuhuri Diamond Platnumz, iliyoambatanishwa na picha zinazodaiwa kuhusiana na ndoa ya mkeka, imewaacha mashabiki wengi katika hali ya sintofahamu—wengi wakijiuliza iwapo msanii huyo maarufu ameoa au la.
Kupitia chapisho lake katika mitandao ya kijamii, Diamond alieleza kuwa amekuwa akikwepa mahojiano na vyombo vya habari kwa makusudi, akisema kufanya hivyo kumemsaidia kuepuka maneno ya upotoshaji na uzushi kutoka kwa watu.
Akiongea kwa tafakari na kina na kwa hisia, Diamond alisema kuwa kukaa kimya wakati anakumbwa na maneno ya uongo ni jambo linalohitaji ukomavu wa hali ya juu, na kumshukuru Mungu kwa kumpa hekima hiyo:
“Miongoni mwa vitu ambavyo nimejifunza ni ukomavu wa kukaa kimya… Ukomavu huu unahitaji uvumilivu wa hali ya juu, moyo wa subira, na roho ya kukaza pale ambapo mtu au watu wanapokupaka matope kwenye jamii ilhali wewe unajua ukweli, lakini unachagua kukaa kimya. Si jambo jepesi, lakini faida yake ni kubwa – unapambana vita zako kwa msaada wa Mungu, na mwisho wake unakuwa mshindi.”
Hata hivyo, katika ujumbe huo, Diamond hakuthibitisha moja kwa moja kama kweli ameoa, licha ya picha zinazomuonesha akiwa katika mazingira yanayofanana na hafla ya harusi. Kauli yake ya mwisho nayo haikufafanua jambo hilo kikamilifu:
“Anyways: Najua kila mmoja wenu ana picha tofauti kabisa kuhusu Diamond Platnumz na KUOA, ila tu nataka leo niwaambie kuwa HUYU DIAMOND PLATNUMZ ALISHAWAHI KUOA, na kuna siku nitawaambia ikawaje,” aliandika.
Kauli hiyo imeongeza maswali miongoni mwa mashabiki, huku wengine wakichukulia comment ya Juma Jux kama ushahidi wa ndoa hiyo. Jux aliandika:
“Welcome to the team my brother 🤝”
View this post on Instagram
Kumbuka kuwa mwezi huu, Diamond anatarajiwa kutangaza msanii mpya atakayesajiliwa chini ya lebo yake ya muziki WCB Wasafi, kufuatia kuondoka kwa Mbosso mapema mwaka huu.
Baadhi ya Hisia za Mashabiki:
-
Simba_Bhoy: Brother mbona ndoa ya mkeka iyoooo……………….😮
-
Msafitheswagg: HII ITAKUWA NDOTO NGOJA NIENDELEE KULALA
-
Popineshine: Sikuwahi waza kama itatokea hii miaka hii ya karibuni kwa kweli ni surprise..😱 ONGERA SIMBA🫡
-
Kimkayndo: Mimi naondoka na paragraph ya mwisho tajiri
Entertainment
Chris Brown Akanusha Shtaka la Kumshambulia Producer kwa Chupa

Msanii nyota wa Marekani, Chris Brown, amekana mashtaka mawili mahakamani yanayohusiana na madai ya shambulio kwa kutumia chupa katika kilabu cha usiku jijini London miaka miwili iliyopita.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 36 anatuhumiwa kumsababishia mtayarishaji wa muziki majeraha ya mwili katika tukio ambalo waendesha mashtaka wamelieleza kuwa “halikuwa na uchochezi wowote”.
Pia anakabiliwa na shtaka la kumiliki silaha hatari — ambayo ni chupa ya kileo.
Mashtaka haya mawili yaliongezwa mwezi uliopita kwenye shtaka la awali, kubwa zaidi, la kujaribu kumsababishia mtu majeraha mabaya ya mwili (GBH), ambalo tayari Bwana Brown alilishatupilia mbali kwa kujitetea kuwa si kweli.
Chris Brown anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa kesi hiyo mwezi Oktoba mwaka 2026.
Waendesha mashtaka wamesema kuwa mhanga wa tukio hilo, Abraham Diaw, alikuwa amesimama kwenye baa ya kilabu cha usiku kilichopo eneo la Soho mnamo tarehe 19 Februari 2023, wakati Chris Brown alimpiga kwa chupa mara kadhaa.
Mwimbaji huyo alikamatwa mwezi Mei katika hoteli ya nyota tano iliyopo Salford, Greater Manchester, baada ya kurejea Uingereza kwa ajili ya maandalizi ya ziara yake ya muziki barani Ulaya.
Alizuiliwa korokoroni kwa takriban wiki moja kabla ya kuachiliwa kwa dhamana baada ya kukubali kulipa ada ya dhamana ya pauni milioni tano (£5m) kwa mahakama.
Ada ya dhamana ni kiasi cha fedha kinachowekwa kama dhamana ya kifedha kuhakikisha mtuhumiwa atarudi mahakamani kwa kesi yake. Brown anaweza kupoteza fedha hizo endapo atakiuka masharti ya dhamana, ambayo yaliendelezwa katika kikao cha mahakama siku ya Ijumaa.
Kwa mujibu wa masharti hayo, Chris Brown anatakiwa kuishi katika anwani iliyopo Uingereza akisubiri kesi hiyo, na aliamriwa kukabidhi pasipoti yake kwa polisi.
Hata hivyo, ameruhusiwa kuendelea na ratiba ya ziara yake ya kimataifa ya Breezy Bowl XX kwa masharti kwamba atakabidhi pasipoti kila anapomaliza safari, na kuirudishiwa anapohitaji kusafiri kwa ajili ya maonesho.
Katika wiki za hivi karibuni, Brown amekuwa akitumbuiza kwenye viwanja na kumbi mbalimbali za burudani kote Uingereza na Ulaya, na kumaliza burudani mjini Paris mwishoni mwa wiki iliyopita. Sehemu ya ziara hiyo inayofanyika Marekani Kaskazini inatarajiwa kuanza baadaye mwezi huu na kufikia tamati tarehe 18 Oktoba.
Kikao kingine cha mahakama kimepangwa kufanyika tarehe 24 Oktoba.
Chris Brown ni miongoni mwa wanamuziki wakubwa zaidi wa R&B nchini Marekani, akiwa mshindi wa tuzo mbili za Grammy na nyimbo 19 zilizofika katika nafasi 10 za juu kwenye chati za Uingereza, zikiwemo Turn Up The Music, Freaky Friday, With You na Don’t Wake Me Up.
Mshitakiwa mwenza, Omololu Akinlolu, raia wa Marekani mwenye umri wa miaka 39 anayefahamika kisanii kama HoodyBaby, naye pia alikana shtaka la kumsababishia mtu majeraha ya mwili. Awali, alikana pia shtaka la kujaribu kusababisha majeraha mabaya ya mwili.
Chanzo: BBC
Entertainment
Justin Bierber Arejea na Album Mpya ‘SWAGG’

Msanii nyota wa muziki wa kimataifa, Justin Bieber, hatimaye ameachia rasmi albamu yake mpya na ya saba kwa jina “Swag”, ikiwa ni albamu yake ya kwanza tangu mwaka 2021 alipotoa Justice. Albamu hii imetoka leo na tayari imeanza kutikisa majukwaa mbalimbali ya muziki duniani.
Swag imejumuisha mastaa kadhaa akiwemo Gunna, Sexyy Red, Cash Cobain, pamoja na wasanii wengine wa kizazi kipya.
Albamu hiyo ina jumla ya nyimbo 20 na tayari baadhi ya vibao kama “Go Baby”, “Soulful” na Butterflies “zimeanza kupokelewa vizuri kwenye mitandao ya Spotify, Apple Music na YouTube.
Hii ni mara ya kwanza kwa Bieber kuachia albamu tangu alipopata matatizo ya kiafya mwaka 2022 yaliyosababisha asitishe ziara yake ya kimataifa ya Justice World Tour ambayo ilikuwa iendelee hadi mwaka 2023.
Ziara hiyo ilisitishwa mnamo Septemba 2022 baada ya Bieber kupatwa na maradhi ya Ramsay Hunt Syndrome, ugonjwa uliomsababishia kupooza upande mmoja wa uso.
Kwa kipindi cha miaka minne bila kazi mpya, mashabiki wa Justin Bieber duniani wamekuwa wakimsubiria kwa hamu ujio wa kazi mpya kutoka kwake. Kupitia Swag, msanii huyo ameonyesha kurejea kwa nguvu na ubunifu wa hali ya juu, huku akiwa katika hali nzuri kiafya na kisaikolojia.
Taarifa na Francos Mzungu