News
Papa Leo XIV amteua Askofu wa kwanza kutoka China

Makao makuu ya Kanisa Katoliki duniani mjini Vatican ilitangaza uteuzi wa kwanza wa Askofu mwenye asili ya China chini ya usimamizi wa Papa Leo XIV.
Hii inaashiria uungaji mkono wa Papa mpya kwa makubaliano yenye utata juu ya uteuzi uliyopingwa na mtangulizi wake na Beijing.
Ofisi ya Vatican imeeleza kuridhishwa na China kwa kutambua kuteuliwa kwa Joseph Lin Yuntuan kama Askofu msaidizi wa Fuzhou, mji mkuu wa jimbo la Fujian kusini mashariki.
Papa alifanya uteuzi huo tarehe 5 mwezi Juni mwaka huu wa 2025.
“Tukio hili linawakilisha matunda zaidi ya mazungumzo kati ya kiti kitakatifu na Mamlaka ya China na ni hatua muhimu katika safari ya Jumuiya ya dayosisi,” ilisema katika taarifa.
Uongozi wa Vatican na ule wa Kikomunisti wa China hauna uhusiano rasmi wa kidiplomasia, kwani Vatican inaitambua Taiwan huku Beijing ikidai kisiwa hicho kinachojitawala ni eneo lake.
Lakini katika makubaliano ya kihistoria, walikubaliana mwaka 2018 kuruhusu pande zote mbili kuwa na usemi katika kuwataja maaskofu nchini China, ambayo ina takriban Wakatoliki milioni 12.
Hata hivyo hayati Papa Francis alipokuwa akitafuta nafasi ya Kanisa kuingia nchini China, mkataba huo ulifanywa upya mara kadhaa, wa hivi karibuni ikiwa ni mnamo Oktoba 2024, baada ya mda wa miaka minne.
Papa Francis alifariki Aprili 21 mwaka 2025 baada ya miaka 12 ya kuhudumu kama Kiongozi wa waumini wa Kanisa katoliki duniani wapatao bilioni 1.4 na Papa Leo alichaguliwa katika kongamano la Makadinali Mei 8 mwaka 2025.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Nassir: Kaunti ya Mombasa wametenga milioni 80 za Afya

Gavana wa kaunti ya Mombasa, Abdulswamad Shariff Nassir amesema serikali ya kaunti ya Mombasa wametenga shilingi milioni 80 kugharamia sehemu ya matibabu ya wakaazi ambao hutibiwa katika hospitali za Level 4 na Level 5.
Akizungumza katika kaunti ya Mombasa, Nassir alisema fedha hizo zitagharamia bima ya afya ya SHA ya wenyeji wa kaunti hiyo kwa muda wa mwaka mmoja.
Gavana Nassir pia alisema fedha hizo zitagharamia madeni ya ziada ya matibabu kwa watoto wa chini ya umri wa miaka 5 ambao wanatibiwa kupitia bima hiyo ya SHA.
“Tumeweka dawati maalum na fedha kuweza kuwalipia ile amana ambayo ilikuwa inalipiwa SHA. Na itakuwa sio ya Public health pekee lakini kando na Public health mnakuwa mumelipiwa kwa mwaka mzima’’, alisema gavana Nassir
Wakati huo huo Gavana Nassir alieleza matumaini kwamba mpango huo utasaidia kwa asilimia kubwa kuimarisha huduma za matibabu kwa wenyeji wa kaunti hiyo.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Chibule, apendekeza adhabu kali kwa wanaoendeleza dhulma za kijinsia

Naibu gavana kaunti ya Kilifi Flora Mbetsa Chibule, amependekeza adhabu kali kwa watu wanaotekeleza visa vya dhulma za kijinsia katika jamii.
Chibule alisema visa vya dhulma za kijinsi dhidi ya watoto vimekithiri katika jamii hasa kaunti ya Kilifi, akiahidi ushirikiano wa hali ya juu na wadau mbalimbali ili kukomesha visa hivyo.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya hamasa kuhusu dhulma za kijinsia katika uwanja wa Bofa Youth mjini Kilifi, Chibule alisema ili kufanikisha ndoto ya mtoto wa kike ni lazima haki zao za kimsingi zilindwe.
“Kwa ambao wanadhulumu mtoto wa kike na kiume, kwa wale ambao wanaingia misuli kwa misuli wanafaa kuwekwa gerezani kabisa”, alisema Chibule.

Wanaharakati wa kijamii wapinga unyanyasaji wa kijinsi, Kilifi
Kwa upande wake Mwakilishi wa kike kaunti ya Kilifi Getrude Mbeyu aliyeandaa hafla hiyo kupitia hazina ya kitaifa ya NGAAF na kutoa hundi ya kima cha shilingi milioni 1.6 kwa makundi 14, alisisitiza hamasa zaidi kwa jamii kuhusu jinsi ya kukomesha visa hivyo.
“Ni jukumu letu la kuwaeleza hawa watu watambua jinsi ya kuripoti hizi kesi, yani kwa mfano umedhulumiwa ni wapi pa kuanzia na hatua hii itakomesha hizi visa”, alisema Mbeyu.
Naye Mzee wa mataa wa Kiwandani mjini Kilifi Elina Nyevu alisema visa vya dhulma za kimapenzi vimekithiri mno katika mtaa huo, akipendekeza hamasa zaidi kwa jamii.
“Hapa kwetu Kiwandani visa vya dhulma za kijinsia ni vingi sana, kuna ulevi na ukosefu wa ajira ambao umechangia utumiaji wa Mihadarati na unyanyasaji wa watoto wadogo kimapenzi, alisema Elina.
Hata hivyo katika halfa hiyo baadhi ya watoto waliopitia madhila hayo hasa ubakaji wameelezea masaibu waliopitia japo haki yao kupitia idara ya usalama walikosa kufaulu.
Taarifa ya Lolani Kalu.