Mahakama ya Kilifi yaagiza kuzuiliwa Washukiwa 7 wa mauaji

Mahakama ya Kilifi yaagiza kuzuiliwa Washukiwa 7 wa mauaji

Mahakama ya Kilifi imeagiza kuzuiliwa kwa siku 14 washukiwa 7 wanaotuhmiwa kuhusika katika kifo cha mwanamke mmoja aliyekuwa na umri wa miaka 65, ambaye aliuwawa kwa tuhma za uchawi katika eneo la Malomani eneo bunge la Ganze kaunti ya Kilifi.

Washukiwa hao Gilbert Karisa Changawa, Selvestar Changawa Kahindi, Elizabeth Jackson Ngala, Dhahabu Kithi Kombe, Dzendere Palu Kalama, Agness Changawa na Kadzo Ngombo Bienge watazuiliwa katika kituo cha Bamba wakati uchunguzi ukiendelea.

Kulingana na Afisa mpelelezi kutoka kitengo cha DCI ameeleza mahakama kwamba ilikuwa mnamo tarehe 27 mwezi huu ambapo walipokea tarifa kwamba dama changawa alikuwa amekatwa kichwa na kuuwawa na watu wasiojulikana usiku huo.

Afisa mpelelezi pia ameeleza kuwa washukiwa ambao ni wanafamilia,siku kabla ya tukio husika walikuwa wameandaa kikao cha kudumisha Amani baada ya kifo kilichokuwa kimetokea kwa kijana mmoja mtoto wa mmoja kati ya washukiwa aliyefariki kaunti ya Mombasa baada ya kupigwa kwa tuhma za wizi.

Kutokana na kifo cha kijana huyo wanafamilia hao walimtuhmu dama kwamba ndiye aliyekuwa amemroga kijana huyo na kusababisha kifo hicho cha gafla, ambapo usiku huo Dama aliuwawa nyumbani kwake.

Washukiwa watarudishwa mahakamani tarehe 13 mwezi Agosti mwaka huu baada ya uchunguzi kukamilika.

Taarifa ya Teclar Yeri