Wakimbizi nusu milioni wakabiliwa na baa la njaa, Dadaab

Wakimbizi nusu milioni wakabiliwa na baa la njaa, Dadaab

Ripoti iliyotolewa hivi karibu na Shirika la Chakula duniani WFP ilionyesha kwamba zaidi ya wakimbizi nusu milioni wanaoishi katika kambi za wakimbizi za Kakuma na Dadaab zilizoko nchini Kenya, wako katika hatari ya kuangamia kutokana na baa la njaa.

Kambi hizi ambazo zinahifadhi wakimbizi wengi zaidi kutoka nchini Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Somalia, ziko hatari iwapo zitakosa misaada ya chakula.

Kufuatia hali hiyo ambayo pia imechangiwa na mashirika ya kimataifa kusitisha ufadhili, sasa hali huenda ikawa tofauti baada ya taifa la Korea kwa ushirikiano na Kenya kutoa ufadhili wa shehena ya nafaka ya zaidi ya tani elfu 10 ambayo inakadiriwa kuwa kima cha shilingi milioni 1.2.

Katibu katika Idara ya uhamiaji nchini Belio Kipsang, aliyepokea msaada huo wa Chakula mjini Mombasa na kuhifadhiwa katika maghala ya Shirika la WFP, ameonya kwamba iwapo Kenya itakosa kupokea msaada kutoka kwa washirika na wafadhili wengine, basi italazimika kuchukua maamuzi magumu, ikiwemo kuwaondoa baadhi ya wakimbizi.

“Nyuma ya kila takwimu kuna familia ambazo ustahimilivu wao unaendelea kujaribiwa kila siku: akina mama wanaokosa kula ili watoto wao wapate chakula, watu walio katika mazingira hatarishi wakiruka milo, na vijana wanaokabiliwa na mustakabali usio na uhakika. Hizi si takwimu za kufikirika. Zinawakilisha watu halisi ambao heshima yao, afya yao na matarajio yao ya maisha yanategemea maamuzi tunayofanya kwa pamoja,” alisema.

Wakati wa hafla hiyo ya kupokea msaada huo wa chakula kwa wakimbizi wa Kakuma na Dadaab, Mkurugenzi wa Shirika la WFP nchini Kenya Betty Ka, alisema shehena ya nafaka itasaidia kuwahudumia takribani wakimbizi nusu milioni katika miezi ijayo.

“Usafirishaji huu unaonyesha umuhimu wa ushirikiano imara katika mnyororo wa ugavi wa misaada ya kibinadamu, ambapo ushirikiano huu kati ya Kenya, Mamlaka ya bandari Kenya (KPA), Shirika la viwango la Kenya(KEBS) na mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa kuhakikisha kwamba chakula cha msaada kinafanikishwa”,alisema Betty.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi