Vifo vya Wanawake wajawazito Kilifi

Vifo vya Wanawake wajawazito Kilifi

Kaunti ya ni Kilifi ni miongoni mwa kaunti ambazo ziko na Idadi kubwa ya vifo vya wanawake wajawazito wanaofariki dunia wakati wa kujifungua pamoja na vile vya watoto wachanga.

Katika kikao ambacho kiliwaleta pamoja waandishi wa habari, hafla ambayo ilfanyika katika ukumbi wa kibaoni mjini Kilifi, kupitia wakfu wa Shina ilibainika visa hivyo vinachangiwa na ukosefu wa hamasa kwa akina mama wajawazito hasa walioko mashinani kuhusu umuhimu wa kula lishe bora, kutokuhudhuria kliniki kutokana na mila na tamaduni na pia hali ya umasikini.

Akizungumzia hilo Nazi Kivutha ambaye ni mwanzilishi wa wakfu wa Shina alisema kando na ukosefu wa ufahamu huo wa akina mama kuhusu uzazi usalama kaunti ya Kilifi hamasa za kutosha hazijatolewa ipasavyo maeneo ya mashinani.

“Hapa kaunti ya Kilifi viwango vya umasikini viko juu na hilo linawafanya wanawake wengi kushindwa kumudu lishe bora na pia wengi wao bado wamekumbatia mila na tamaduni na ndio maana wanaamini kukandwa na wakunga na kupuuza kuhudhuria kliniki ili kujifungua Salama” alisema Bi Kivutha

Kwa upande wake Winnie Barawa alisema baadhi ya wanawake wajawazito wanafariki dunia kutokana ukosefu wa damu mwilini hali ambayo inachangia kwa vifo hivyo na kuwataka kuzingatia ulaji wa vyakula bora na pia kuhudhurikia kliniki mara kwa mara.

“Utapata wengi kiwango chao damu kiko chini mno hali ambayo inawaweka  mama na mtoto katika hatari ya kufariki dunia” alisema Winnie Barawa.

Hata hivyo walisema kupitia mradi wa okoa mama na mtoto chini ya wakfu wa Shina mikakati inaendelea kuwekwa ili kudhibiti vifo hivyo.

Haya yanajiri miezi michache baada ya mratibu wa huduma ya afya kaunti ya Kilifi Edward Mumbo kutoa takwimu hizo zikiwemo zile za  watoto njiti

Taarifa ya Janet Mumbi