Mahakama ya Kilifi imemhukumu kifungo cha miaka 25 gerezani mwanaume mmoja ambaye ni mzee wa umri wa miaka 69 baada ya kupatikana na hatia ya kumnajisi mjukuu wake mwenye umri wa miaka 13.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Ivy Wasike amesema mzee huyo atatumikia kifungo hicho gerezani kwani wazee kama wao ndio wanaofaa kukemea vitendo hivyo sawa na kuelekeza vijana lakini wamekuwa wahusika wakuu wa dhulma za kijinsia dhidi ya watoto.
Hakimu Wasike ameagiza idara ya watoto na jamii kumpa ushauri nasaha mtoto huyo ili apate nafuu baada ya kutatizika kisaikolojia alipopitia dhulma hiyo.
Awali Mahakama ilielezwa kwamba kati ya tarehe tofauti mwezi Januari mwaka 2025 katika eneo la Kauma kaunti ya Kilifi, mzee huyo kwa jina Chivatsi Mundu akiwa mlevi alimnajisi mjukuu wake aliyekuwa ameenda kumsaidia kuchota maji.
Mahakama imeelezwa kwamba baada ya mzee huyo kumtendea unyama huo mjukuu wake alionya kwamba asiwahi kusimulia kitendo hicho kwa mtu yeyote tukio hilo, lakini ikabainika wazi.
Mahakama pia ikimpa mzee huyo siku 14 za kukata rufaa iwapo hajaridhishwa na uamuzi huo wa Mahakama.
Taarifa ya Teclar Yeri
