News
Mwanaharakati Mwabili Mwagodi apatikana

Mwanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu Mwabili Mwagodi ambaye alidaiwa kutekwa nyara akiwa nchini Tanzania sasa amepatikana.
Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za kibinamu nchini la VOCAL Africa Hussein Khalid, alisema Mwabili alipatikana katika msitu wa Kinondo eneo bunge la Msambweni kaunti ya Kwale mwendo wa saa tisa usiku akitembea kuelekea Diani.
Khalid alisema Mwabili, anaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Pandya mjini Mombasa kisha baadaye atasafirishwa kwa ndege hadi jijini Nairobi kuungana na familia yake.
“Tunashukuru Mwabili amepatikana akiwa hai japo amedhohofika na anaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Pandya na kisha atarudi Nairobi kukutana na familia yake lakini tunaiambia serikali ya Kenya na Tanzania ni lazima wahusika kukomesha tabia hii ya kuwateka watu nyara kuna sheria kama mtu amekosea apelekwe Mahakamani”, alisema Khalid.
Hata hivyo Wanaharakati hao wa kutetea haki za kibinadamu waliishtumu serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuwanyanyasa wanaharakati wa kijamii wa taifa la Tanzania na wale wanaoingia Tanzania kutoka mataifa mengine ili kuendeleza hamasa za haki za kijamii.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Mabadiliko ya tabianchi yatajwa kuchangia mapato duni ya samaki, Lamu

Wadau katika sekta ya mazingira kaunti ya Lamu wanasema mabadiliko ya hali ya anga yanayoshuhudiwa sawa na ujenzi wa bandari ya Lamu kumechangia mapato ya samaki kupungua katika bahari hindi.
Mahmoud Yusuf ambaye ni mwanazingira alisema zana za kizamani wanazotumia wavuvi kuvua samaki pia zinachangia mapato duni ya samaki.
Yusuf alisema tangu ujenzi huo wa bandari uanze, maji ya bahari chini yamekuwa na matope kutokana na kuchimbwa na kufukuliwa kwa bahari, hali iliyochangia samaki kutorokea bahari kuu.
Mwanamazingira huyo aliitaka serikali kuwapa wavuvi vifaa vya kisasa vya uvuvi sawa na meli za uvuvi zitakazowawezesha kufika maji makuu, baada ya bandari ya ndani kuharibika.
Taarifa ya Joseph Jira.
News
Gachagua atangaza azma ya kuwania urais 2027

Kinara wa chama cha DCP Rigathi Gachagua ametangaza nia ya kuwania wadhfa wa urais mwaka 2027 akilenga kumg’oa rais William Ruto mamlakani.
Gachagua amekuwa akifanya ziara katika eneo la mlima kenya pamoja na viongozi wa chama chake akitumia mikutano ya barabarani kutangaza azma yake ya kuwania urais.
Kulingana na Gachagua serikali ya sasa inatumia mikutano ya ikulu kuendeleza vitendo vya ufisadi, na ameahidi kuwa akichaguliwa atakomesha matumizi mabaya ya fedha za umma.
Katika ziara hiyo viongozi wa chama chake walieza kuwa Gachagua ndiye mgombea anayefaa kupeperusha bendera ya upinzani, wakidai eneo la mlima kenya limejiondoa katika uungwaji mkono wa serikali ya sasa.
Taarifa ya Joseph Jira.