News
Mvuvi aliyezama baharini Watamu apatikana Tanariver

Mwili wa mvuvi Hudhefa Laly aliyepotea baharini huko Watamu eneo bunge la Kilifi Kaskazini Kaunti ya Kilifi akiwa na ndugu yake Athman Laly umepatikana eneo la Shakiko -Mathole, kaunti ya Tana River.
Ndugu hao wawili walitoweka habarini siku ya Alhamisi 24, Julai 2025 katika bahari hindi wakati wakiendelea na shughuli zao za uvuvi.
Vitengo mbali mbali vya uokozi vimekuwa vikiendesha zoezi la kutafuta miili ya wawili hao kwa ushirikiano na wavuvi eneo la Watamu.
Kufikia sasa mwili wa Athman Laly kakake Hudhefa ungali haujapatikana huku juhudi za kuutafuta zikiendelea.
Jamii ya wavuvi katika eneo la Watamu ikiongozwa na kiongozi wa vijana Bakari Shaban iliiomba serikali ya kaunti ya Kilifi na ile ya kitaifa kununua boti za uokozi ili kusaidia kuokoa maisha wakati kunapotokea dharura baharini.
“Tunaomba tupate boti za kuokoa maisha baharini, popote alipo waziri Ali Joho angalau tupate boti za uokozi kama mbili hapa Watamu ni kitovu cha utalii kunamahoteli mengi, watalii wote wanaokuja Watamu mpaka leo hakuna boti za uokozi”, alisema Shaban.
Awali wao wazazi wa wavuvi waliopotea baharini Lali Athman Lali na Dhurai Mohamed Ali waliiomba serikali kuweka juhudi zaidi za kuwasaidia kuwapata wanawao kwani ndio tegemeo kubwa kwa familia yao.
“Uko usaidizi unatumika, kuna vijana wanaojitolea kwa maboti wanaenda ile sehemu ambayo wavuvi wanavua, wanajaribu kuzunguka lakini toka siku hiyo hawajapata chochote: Katika Maisha yangu mimi nawategemea hawa watoto kunisomeshea hawa watoto wangu ambao ni wadogo zao mashule, kwa chakula kwa hivyo naomba serikali inisaidie kwa sababu ndio tegemeo langu hao watoto”.walisema wazazi.
Kisa hiki kilijiri miezi kadhaa baada ya mvuvi mmoja kutoka eneo la Mnarani mjini Kilifi kufariki baharini baada ya kugongwa kichwani kwa pondo na wavuvi wenzake kulipotokea mzozo kuhusu pato la samaki.
Kufikia sasa mwili wa mvuvi huyo haujapatikana.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Kampuni ya Simba Cement yafungwa, Kaloleni

Serikali ya kaunti ya Kilifi kwa ushirikiano na Wizara ya Madini imesitisha rasmi shughuli zote za uchimbaji madini zinazotekelezwa na kampuni ya Simba Cement eneo la Kaloleni kaunti ya Kilifi.
Agizo hilo limetolewa na Gavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Mung’aro pamoja na Waziri wa madini na raslimali za uchumi wa bahari nchini Ali Hassan Joho, wakisema kampuni hiyo imeshindwa kufuata sheria za mazingira na haiwafaidi wakaazi wa eneo hilo.
Viongozi hao walisema shughuli za uchimbaji wa kampuni hiyo zimekuwa zikiathiri mazingira na wakazi wa maeneo ya karibu, huku wakiahidi kwamba serikali haitavumilia ukosefu wa uwajibikaji unaotishia afya na maisha ya wananchi.
Walisisitiza kwamba kampuni hiyo haitaruhusiwa kuendelea na shughuli zake hadi pale itakapokidhi masharti yote ya kisheria na kuthibitisha kwamba haileti madhara kwa binadamu wala mazingira.
“Hii kampuni wacha nikuambie waziri haisadii wananchi wa Kilifi kwa chochote waziri, na leo hii watu wa kambe ribe mnisikize na mnisikize kwa makini, vile nilifanya Jaribuni ndivyo nitakavyofanya leo, kuanzia kesho asubuhi na nitawafuata na barua kesho mwelezeni mwajiri wenu kwamba hii kampuni tumeifunga na nitawafuata na barua”, alisema Gavana Mung’aro.
Hatua hii iliungwa mkono na baadhi ya viongozi wa jamii na wanaharakati wa mazingira, wakisema kuwa ni wakati wa kuwajibisha wawekezaji wanaokiuka haki za wananchi kwa msingi ya maendeleo.
Simba Cement, ambayo imekuwa ikihusishwa na miradi mikubwa ya ujenzi, sasa inalazimika kukabiliwa na masharti mapya kabla ya kurejelea shughuli zake za kawaida.
Taarifa ya Elizabeth Mwende
News
Kanja aagizwa kuwasilisha stakabadhi za Polisi kwa NPSC

Huduma ya kitaifa ya polisi nchini NPS iliagizwa kukabidhi orodha ya malipo ya polisi na kazi zote zinazohusiana na raslimali za umma kwa Tume ya kitaifa ya huduma ya polisi nchini NPSC.
Agizo hilo lilitolewa na Kamati ya bunge la kitaifa kuhusu uhasibu wa umma inayoongozwa na Mbunge wa Butere Tindi Mwale ambayo ilimuagiza Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja kutekeleza agizo hilo mara.
Kulingana na kamati hiyo, hatua hiyo itapunguza uhasama uliopo kati ya taasisi hizo mbili za umma huku ikimtaka Kanja kuhakikisha pia anawasilisha orodha ya mishahara sawa na kuruhusu tume hiyo kutekeleza majuku yake kwa mujibu wa katiba.
Hata hivyo Inspekta Jenerali wa polisi nchini Douglas Kanja aliahidi kutekelezwa kwa maagizo hayo huku mkurugenzi mkuu wa Tume ya huduma ya kitaifa ya polisi nchini NPSC Peter Lelei akiahidi kuandikia Kamati hiyo barua kuhakikisha iwapo maagizo hayo yametekelezwa.
Kanja alikuwa aliitwa mbele ya kamati hiyo kufuatia ripoti iliyotolewa na Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali Magaret Nyakang’o iliyoashiri kwamba NPSC haijaweza kutekeleza majukumu yake kwa kunyimwa stakabadhi muhimu.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi