News
Muturi Apokonywa Walinzi wake

Aliyekuwa Waziri wa utumishi wa umma nchini Justin Muturi amesema maisha yake yamo hatarini baada ya kupokonywa walinzi wake ambao aliyokuwa nao tangu akiwa Spika wa bunge la kitaifa.
Katika kikao na Wanahabari, Muturi amesema walinzi wake wawili waliagizwa kuondoka katika makaazi yake mwendo wa saa moja na nusu usiku, siku ya Jumatatu.
Muturi amesema walinzi hao walimwambia kwamba waliagizwa kutoendeleza majukumu yao ya ulinzi kutokana na mvutano kati yake na serikali, akisema hatua hiyo inalenga kumkandamiza kisiasa.
Muturi amehoji kwamba japo hana wasiwasi wote kuhusu swala hilo lakini usalama wake ni muhimu huku akisema serikali imegonga sipo kwani atahakikisha anawaeleza wakenya ukweli kuhusu madhila ya serikali.
Itakumbukwa kwamba Muturi alitimuliwa kazini na Rais William Ruto kutokana na msimamo wake wa kuikosoa serikali kufuatia visa vya utekaji nyara na mauaji ya kiholela, ufisadi ndani ya serikali pamoja na kudhalilishwa kwa mawaziri nchini.
News
Mombasa inaongoza kwa maambukizi ya MPOX nchini

Wizara ya afya nchini imesema kaunti ya Mombasa inaongoza kwa visa vya maambukizi ya ugonjwa wa Mpox.
Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa idara ya afya nchini Daktari Patrick Amoth, kaunti ya Mombasa imerekodi visa 139 kati ya visa 300 vilivyoripotiwa na wizara hiyo.
Amoth alidokeza kuwa serikali itatangaza siku maalum ya kutoa chanjo ya kudhibiti msambao wa ugonjwa huo wakishirikiana na shirika la afya ulimwenguni WHO.
Mkurugenzi huyo vile vile alimesema zoezi hilo litaambatana na hamasa kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na maambukizi zaidi.
“Kwa wakati huu Mombasa ndio inaongoza kwa idadi ya visa 139 kwa hivyo tuchuke tahadhari kuhakikisha kwamba tunazuia maambukizi, na tunafanya mpango pamoja na shirika la afya duniani WHO, hapa tutakuja na mpango wa chanjo na ikifika huo wakati tunaomba watu wajitokeze wapate chanjo ili wapate kinga”,alisema Daktari Amoth.
Wakati huo huo Amoth aliokeza kuwa uchunguzi wa vifo vya watu wanne walioaga dunia wiki chache zilizopita huko Migadini, eneo bunge la Changamwe kaunti ya Mombasa umebaini walifariki kutokana na magonjwa mengine na wala sio maambukizi ya ugonjwa wa MPOX kama ilivyodhaniwa na wakaazi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu.
News
Wavuvi wawili wafa maji Watamu,Kilifi

Jamii ya wavuvi katika eneo la Watamu eneo bunge la Kilifi Kaskazini inaiomba serikali ya kaunti ya Kilifi na ile ya kitaifa kununua boti za uokozi ili kusaidia kuokoa maisha wakati kunapotokea dharura baharini.
Hii ni baada ya wavuvi wawili kupotoea katika bahari hindi eneo la Watamu walipokuwa wakiendeleza shughuli zao za uvuvi siku ya Alhamisi 24, Julai 2025.
Kufikia sasa wawili hao hawajapatikana licha ya juhudi za wadau mbalimbali ikiwemo jeshi la wanamaji kuwatafuta.
Kiongozi wa vijana eneo la Watamu Bakari Shaban, alisema kuwa juhudi za kuwatafuta wavuvi hao ambao ni mandugu wanaotambulika kama Athman Lali na Huzefa Lali zinaendelea.
Shaban alisistiza haja ya serikali kuangazia suala la ununuzi wa mashua za kisasa za uokozi ili kupunguza visa vya wavuvi kuangamia baharini wakati wanapoelekea kuvua.
“Mpaka sasa juhudi zote zimefanyika lakini ndugu zetu hatujajua wako sehemu gani, serikali itusaidie mji wetu wa Watamu ni mji wa utalii, tunaomba tupate boti za kuokoa maisha baharini, popote alipo waziri Ali Joho angalau tupate boti za uokozi kama mbili hapa Watamu ni kitovu cha utalii kunamahoteli mengi, watalii wote wanaokuja Watamu mpaka leo hakuna boti za uokozi”, alisema Shaban.
Kwa upande wao wazazi wa wavuvi waliopotea baharini Lali Athman Lali na Dhurai Mohamed Ali waliiomba serikali kuweka juhudi zaidi za kuwasaidia kuwapata wana wao kwani ndio tegemeo kubwa kwa familia yao.
“Uko usaidizi unatumika, kuna vijana wanaojitolea kwa maboti wanaenda ile sehemu ambayo wavuvi wanavua, wanajaribu kuzunguka lakini toka siku hiyo hawajapata chochote: Katika Maisha yangu mimi nawategemea hawa watoto kunisomeshea hawa watoto wangu ambao ni wadogo zao mashule, kwa chakula kwa hivyo naomba serikali inisaidie kwa sababu ndio tegemeo langu hao watoto”.walisema wazazi.
Kisa hiki kinajiri miezi kadhaa baada ya mvuvi mmoja kutoka eneo la Mnarani mjini Kilifi kufariki baharini baada ya kugongwa kichwani kwa pondo na wavuvi wenzake kulipotokea mzozo kuhusu pato la samaki.
Kufikia sasa mwili wa mvuvi huyo haujapatikana
Taarifa ya Mwanahabari wetu