News
Murkomen:Dumisheni amani siku ya Sabasaba

Waziri wa usalama wa kitaifa Kipchumba Murkomen ameshinikiza amani wakati wa maandamano ya kumbukumbu ya siku ya Sabasaba ambayo inafanyika Julai 7, 2025.
Akizungumza katika kaunti ya Meru, Murkomen alieleza wasiwasi wake kuhusiana na matukio ya vurugu ambayo yameshuhudiwa wakati wa maandamano ya hivi karibuni, ambapo mali ya umma ikiwemo vituo vya polisi na majengo ya mahakama vilivamiwa na kuteketezwa moto.
Murkomen aliweka wazi kuwa majukumu ya polisi ni kulinda raia japo hawatakubali matukio ya ghasia na vurugu.
Vile vile waziri huyo alihimiza polisi kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha maandamano yaliyopangwa Julai 7 2025 yanakuwa ya amani.
Wakati huo huo huduma ya kitaifa kwa polisi nchini NPS ilionya kuhusu matukio yeyote ya kihuni wakati wa maandamano ya sabasaba.
Katika taarifa NPS iliahidi kutekeleza majukumu yake ya kuweka amani na kulinda raia huku ikitahadharisha kuwachukulia hatua kali watakaovunja sheria wakati wa maandamano hayo.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Biwott: Polisi waendelea kuwasaka waumini wenye itikadi potovu

Kamanda wa Polisi kaunti ya Kilifi Josephat Biwott amepongeza juhudi za wakaazi wa kaunti hiyo kwa kuwa na ushirikiano mwema na asasi za usalama.
Biwott amesema ni kupitia ushirikiano huo ambapo oparesheni ya kuwanasa waumini wa dini potofu eneo la Binzaro, kilomita chache kutoka eneo la Shakahola imefanikiwa kutokana na juhudi za wakaazi kutoa taarifa kwa maafisa wa usalama.
Akizungumza na Coco Fm, Biwott alithibitisha kwamba eneo la Chakama lipo chini ya ulinzi wa polisi.
Biwott alidhitisha kuwa washukiwa 11 tayari wamekamatwa na wamefikishwa Mahakamani Jumanne 22 Julai 2025 mbele ya Hakimu Mwandamizi Joy Wesonga na wataendelea kuzuiliwa katika kituo cha Polisi mjini Malindi.
Biwott aidha alisema maafisa wa usalama wanachunguza iwapo washukiwa hao walienda msituni wakiwa na watoto.
“Nawashukuru wananchi wetu hasa wakaazi wa Binzaro, kwa kutueleza kwa mapema sana kuhusu yale mambo yalikua yanaendelea huko kwa vile wametueleza tumefaulu kuokoa wale ambao tumeokoa na wanaoendelea dini hiyo tumewakamata na wamefikishwa mahakamani”. …alisema Biwott, kwa njia ya simu.
Tarifa ya Elizabeth Mwende
News
NACADA yapendekeza sheria mpya ya kudhibiti pombe

Mamlaka ya kukabiliana na dawa za kulevya na pombe haramu nchini NACADA inaendelea kushikilia pendekezo lake la kutaka umri wa chini wa unywaji wa pombe uwe wa miaka 21.
Mratibu wa Mamlaka hiyo kaunti ya Mombasa, Wangai Gashoka alisema pendekezo hilo limetokana na ongezeko la vijana wadogo wanaotumia pombe kupindukia.
Wangai alisema kuwa utafiti wa NACADA ulionyesha wazi kwamba akili ya binadamu huendelea kukua hadi miaka 25 hivyo mtu akinywa pombe akiwa na umri mdogo huongeza hatari ya uraibu wa mapema.
NACADA sasa inashinikiza pendekezo hilo kufanywa kuwa sheria ambayo itaidhinishwa bungeni na kuanza kutekelezwa kikamilifu.
Ni hatua ambayo ilipigiwa upato na wakereketwa wa kukabiliana na utumizi wa dawa za kulevya akiwemo Famau Mohamed Famau ambaye alisisitiza haja ya mapendekezo hayo kutopuuziwa.
Taarifa ya Hamis Kombe