News
Msithubutu Maandamano ya Sabasaba Mombasa – Polisi Yaonya

Idara ya Usalama mjini Mombasa imetoa taarifa kujibu ombi la wanaharakati wanaotaka kuandaa maandamano ya kuadhimisha siku ya SABA SABA mjini Mombasa.
Katika barua iliyotiwa Saini na Afisa mkuu wa Polisi (OCS) wa kituo Cha Central mjini Mombasa, Sylvester Wambua, ombi hilo limekataliwa kwa sababu za kiusalama, Polisi wakidai wana taarifa za kijasusi kwa maandamano hayo huenda yatatumiwa na wahuni kuvuruga amani, kusababisha maafa na uharibifu wa mali.
Ombi hilo liliwasilishwa na mwanaharakati Bradley Ouna. Maandamano hayo yanatarajiwa kufanyika katika Barabara ya SABA SABA hadi Mwembe Tayari, mzunguko wa Fountanella na kuishia Uhuru gardens eneo la Mapembe ya Ndovu kwenye Barabara ya Moi Avenue.
Siku ya SABA SABA huadhimishwa kukumbuka harakati za ukombozi wa pili nchini Kenya ulitoa nafasi ya utawala wa Vyama vingi nchini .
Charles Rubia na Kenneth Matiba wakishirikiana na Jaramogi Oginga Odinga ni miongoni mwa viongozi waliowaongoza Genz wa miaka hiyo, kama vile James Orengo, Paul Muite na wengineo kumshurutisha Rais Daniel Arap Moi kuondolea mbali kifungu 2 A cha katiba ya Kenya, na kutoa nafasi ya siasa vya Vyama vingi nchini.
News
Biwott: Polisi waendelea kuwasaka waumini wenye itikadi potovu

Kamanda wa Polisi kaunti ya Kilifi Josephat Biwott amepongeza juhudi za wakaazi wa kaunti hiyo kwa kuwa na ushirikiano mwema na asasi za usalama.
Biwott amesema ni kupitia ushirikiano huo ambapo oparesheni ya kuwanasa waumini wa dini potofu eneo la Binzaro, kilomita chache kutoka eneo la Shakahola imefanikiwa kutokana na juhudi za wakaazi kutoa taarifa kwa maafisa wa usalama.
Akizungumza na Coco Fm, Biwott alithibitisha kwamba eneo la Chakama lipo chini ya ulinzi wa polisi.
Biwott alidhitisha kuwa washukiwa 11 tayari wamekamatwa na wamefikishwa Mahakamani Jumanne 22 Julai 2025 mbele ya Hakimu Mwandamizi Joy Wesonga na wataendelea kuzuiliwa katika kituo cha Polisi mjini Malindi.
Biwott aidha alisema maafisa wa usalama wanachunguza iwapo washukiwa hao walienda msituni wakiwa na watoto.
“Nawashukuru wananchi wetu hasa wakaazi wa Binzaro, kwa kutueleza kwa mapema sana kuhusu yale mambo yalikua yanaendelea huko kwa vile wametueleza tumefaulu kuokoa wale ambao tumeokoa na wanaoendelea dini hiyo tumewakamata na wamefikishwa mahakamani”. …alisema Biwott, kwa njia ya simu.
Tarifa ya Elizabeth Mwende
News
NACADA yapendekeza sheria mpya ya kudhibiti pombe

Mamlaka ya kukabiliana na dawa za kulevya na pombe haramu nchini NACADA inaendelea kushikilia pendekezo lake la kutaka umri wa chini wa unywaji wa pombe uwe wa miaka 21.
Mratibu wa Mamlaka hiyo kaunti ya Mombasa, Wangai Gashoka alisema pendekezo hilo limetokana na ongezeko la vijana wadogo wanaotumia pombe kupindukia.
Wangai alisema kuwa utafiti wa NACADA ulionyesha wazi kwamba akili ya binadamu huendelea kukua hadi miaka 25 hivyo mtu akinywa pombe akiwa na umri mdogo huongeza hatari ya uraibu wa mapema.
NACADA sasa inashinikiza pendekezo hilo kufanywa kuwa sheria ambayo itaidhinishwa bungeni na kuanza kutekelezwa kikamilifu.
Ni hatua ambayo ilipigiwa upato na wakereketwa wa kukabiliana na utumizi wa dawa za kulevya akiwemo Famau Mohamed Famau ambaye alisisitiza haja ya mapendekezo hayo kutopuuziwa.
Taarifa ya Hamis Kombe