News
Mshukiwa wa Ugaidi Azuiliwa na Polisi Mombasa

Maafisa wa Polisi mjini Mombasa wanamzuilia mwanamme mmoja baada ya kupatikana akiwa amebeba risasi na bidhaa zengine zinazokisiwa kuwa vilipuzi katika kivuko cha Feri cha Likoni.
Maafisa wa Polisi wamesema jamaa huyo anayefahamika kwa jina Shinali Amuna Komoro amekamatwa alipokuwa akivuka kivuko cha Feri cha Likoni akitokea kisiwani Mombasa.
Maafisa hao wamesema kabla ya mshukiwa huyo kukamatwa alikuwa ameabiri basi lililokuwa likivuka feri kuelekea upande wa Likoni na ametiwa nguvuni wakati maafisa wa usalama walipokuwa wakifanya ukaguzi katika kivuko hicho.
Akithibitisha kukamatwa kwake, Kamanda wa Polisi eneo la Likoni Geoffrey Ruheni amesema huenda mshukiwa alikuwa amepanga njama ya kutekeleza mashambulizi ya kigaidi ndani ya Feri.
Ruheni amesema mshukiwa huyo amekabidhiwa maafisa wa kupambana na ugaidi nchini ATPU kwa uchunguzi zaidi.
News
Ethekon: Sheria haijafafanua taratibu za kuwarudisha nyumbani wabunge

Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imeweka wazi kwamba hakuna sheria inayofafanua misingi na taratibu za kuwarudisha nyumbani wabunge ama maseneta waliokosa kuwajibikia majukumu yao ya kikazi.
IEBC, ilieleza kwamba suala hilo ni kinyume cha Katiba na ubaguzi ikilinganisha hatua hiyo na uamuzi uliyotolewa na Mahakama kuu kuhusu kesi iliyowasilishwa Mahakamani na Taasisi ya Katiba dhidi ya Ofisi ya Mwanasheria mkuu kwa kuambatana na sheria ya uchaguzi ya 2011.
Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na kutiwa saini na Mwenyekiti wa Tume hiyo Erastus Ethekon, IEBC ilisema kutokana na kwamba hakuna mfumo wa sheria wa kuwarudisha nyumbani wabunge ama maseneta waliokosa kuwajibikia majukumu yao ya kikazi, wakenya wanaweza kutumia kipengele cha 104 cha Katiba na kuwarudisha nyumbani Wawakilishi wadi.
Aidha alisema wakati bunge la kitaifa likifanya marekebisho ya sheria kuruhusu kurudishwa nyumbani Wawakilishi wadi, hakuna mwafaka wowote uliafikiwa wa kuruhusu wabunge kurudishwa nyumbani iwapo wamekosa kuwajibika.
Hata hivyo Tume hiyo imeahidi kuwajibika kikamilifu katika suala hilo huku ikisema tayari imeliandikia barua bunge la kitaifa kuibuka na sheria ya kuwarudisha nyumbani wabunge wasiowajibika.
Haya yamejiri kufuatia malalamishi yaliowasilishwa na baadhi ya wakenya wanaotaka baadhi ya wabunge na maseneta kurudishwa nyumbani wa hivi karibuni akiwa Mwakilishi wa Kike kaunti ya Nairobi Esther Passaris akituhumiwa kuvunja sheria na kukiukaji wa Katiba lakini uamuzi wa Tume ya IEBC ni afuani kwake.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Anselim, ashutumu utovu wa usalama Taita Taveta

Kaimu Spika katika bunge la kaunti ya Taita Taveta Anselim Mwadime alieleza kusikitishwa na mauaji ya mhudumu mmoja wa bodaboda aliyeuliwa na kisha pikipiki yake kuchukuliwa katika eneo la chuo kikuu cha Taita Taveta.
Mwadime alisema kuna baadhi ya abiria ambao ni wahuni hubebwa na kisha kuwashambulia wahudumu wa pikipiki hadi kuwaua au hata kutoweka na pikipiki.
Aidha, Mwadime alisema kama viongozi wa kaunti ya Taita Taveta hawataruhusu visa hivyo kuendelezwa katika kaunti hiyo.
Vilevile, Mwadime aliishinikiza idara ya usalama kwenye kaunti ya Taita Taveta kuwajibika ipasavyo ili kudhibiti visa vya utovu wa usalama katika sekta ya bodaboda na wanaohusika wakabiliwe kisheria.
“Hili jambo linafaa kufuatiliwa kwa undani. Na tunalilaani vikali sisi kama viongozi wa Taita Taveta’’ alisema Mwadime.
Taarifa ya Janet Mumbi