News
Miili 7 zaidi yagunduliwa Kwa Binzaro na kufikisha idadi ya miili 32

Shughuli ya kufukuaji wa maiti katika vichaka vya Kwa Binzaro eneo la Shakahola kaunti ndogo ya Magarini inaingia wiki ya pili huku miili 7 zaidi ikifukuliwa Alhamisi Agosti 28.
Kupatikana kwa miili hiyo sasa inafikisha idadi ya maiti zilizofukuliwa katika kijiji Kwa Binzaro kuwa watu 32 waliofariki katika awamu ya pili ya sakata ya mauaji ya kinyama eneo la Shakahola.
Maafisa wa serikali wa uchunguzi wa maiti wakiongozwa na Daktari Richard Njoroge, walisema miili hiyo iliharibika kiasi cha kutombulika huku wakipata vipande vingine 54 vya miili vikiwa vikitapakaa katika eneo la tukio.
Hii inaaminika kwamba baadhi ya miili hiyo ililiwa na wanyamapori kwani ilikuwa imezikwa katika makaburi ya kina kifupi sana.
Sakata hii ya Shakahola 2 inazidisha hofu hasa miongoni mwa wakaazi wa sehemu hiyo ya Shakahola kukiwa na taarifa kwamba huenda baadhi ya miili hiyo ilisafirisha hadi eneo hilo la Kwa Binzaro.
Mapema mwezi uliopita maafisa wa usalama, kwa ushirikiano na wenyeji walifumania kundi la watu wanaoaminika kwamba ni wafuasi wa itikadi kali katika msitu huo wa Kwa Binzaro ambao baadhi yao walifanikiwa kutoroka.
Maafisa wa Polisi waliwazuilia korokoroni watu sita kuhusiana na sakata hiyo ya Kwa Binzaro, ambayo imetokea miaka michache tu tangu kisa cha kwanza na shakaola One chini ya uongozi wa Mhubiri tata Paul Mackenzie.
Waumini wa Kanisa la Mhubiri Mackenzie waaminika walilazimishwa kufunga hadi kufa kwa imani kwamba watakutana na Yesu.
Mackenzi na wenzake wako korokoroni wakisubiri uamuzi wa Mahakama kuhsu kesi ya mauaji inayowakanili.
Taarifa ya Eric Ponda
News
Wahudumu wa afya Lamu watishia kuishtaki serikali ya kaunti hiyo

Wahudumu wa Afya kaunti ya Lamu wametishia kuelekea Mahakamani kuishtaki serikali ya kaunti hiyo kwa kukaidi kutekeleza matakwa yao.
Wahudumu hao waliishtumu serikali ya kaunti ya Lamu kwa kupuuza matakwa yao na badala yake kutumia vitisho ili kuwashurutisha kurejea kazini.
Kulingana na viongozi wa wahudumu hao, licha ya mgomo wao kuendelea kwa zaidi ya wiki mbili serikali ya kaunti hiyo imekataa kata kuandaa vikao vya kusuluhisha malalamishi yao.
Baadhi ya changamoto wanazolalamikia ni pamoja na kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 10 bila ya kupandishwa vyeo, kupuuzwa kwa mkataba wa makubaliano ya nyongeza ya mishahara, kunyimwa kwa mishahara kwa baadhi ya wahudumu hao miongoni mwa matakwa mengine.
“Mkiendelea kutufinyilia itabidi tufuate njia ya sheria kwa sababu tunajua tunalilia haki yetu, haiwezekani serikali ya kaunti inashindwa kutupandisha vyeo ilhali tumefanya kazi kwa miaka 15 sasa, hatuwezi kuendelea kufanya kazi katika mazingira duni na pia mkataba wa makubaliano kuhusu nyongeza ya mishahara sharti itekelezwe” walisisitiza viongozi hao.
Wakati uo huo serikali ya kaunti ya Lamu imejibu malimishi yao kupitia barua na kutangaza kuwa mgomu huo ni kinyume cha seria na kuwataka wahudumu hao kurejea kazini mara moja.
Taarifa ya Elizabeth Mwende
News
Rais Ruto atuma KDF kusimamia ujenzi wa hospitali nchini

Rais William Ruto ametuma jeshi la KDF kusimamia ujenzi wa vituo vya afya zaidi ya 75 kote nchini katika juhudi za kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa haraka.
Akizungumza katika kaunti ya Narok wakati wa uzinduzi wa hospitali ya Sogoo Level 4, waziri wa ulinzi Patrick Mariru alifichua kuwa ujenzi wa hospitali hiyo yenye mamlaka kamili itakamilika baada ya mda wa miezi 11.
Ujenzi wa hospitali ya Sogoo Level 4 ulivutia rais Ruto alipozuru eneo hilo mwezi mei mwaka 2025, jambo lililomfanya kuagiza KDF kuipandisha hadhi.
Mariru hata hivyo alishikilia kuwa wafanyikazi wote wasio na ujuzi watatolewa kutoka kwa jamii.
“Jeshi litamsimamia mkandarasi. Hilo liwe wazi, kazi yote itafanywa na vijana wa Sogoo. Tutaweka maafisa wawili na kila jioni watanipa ripoti ya maendeleo,” alisema Mariru.
“Tuna zaidi ya miradi 75 tunayosimamia na sio kwamba tunabadilisha wakala wa serikali tunataka tu kushirikiana na ofisi tofauti miongoni mwao wizara za afya na michezo.”
Taarifa ya Joseph Jira