News
Mchawi anaswa na wenyeji, Mavueni

Kulikuwa na kizaazaa Julai mosi 2025 katika kijiji cha Mabirikani eneo la Eureka Mitangoni karibu na Mavueni kaunti ya Kilifi baada ya mwanamume anayedaiwa katumia nguvu za uchawi kupatikana ndani ya nyumba, kitandani.
Mwanamme huyo alipatikana akiwa amevalia shati na kikoi cha mwenye nyumba ambaye anaishi jijini Mombasa na mkewe.
Ilisemekana wawili hao hakuweko ndani ya nyumba yako wakati wa tukio hilo lililowashangaza wengi.
Umati wa watu uliwasili katika jumba hilo la ghorofa wakiwa na ghadhabu wakitaka kumshambulia mshukiwa anayedaiwa kuwa mchawi.
Maafisa wa polisi walidumisha usalama wakati walipokuwa wakimsubiri mwenye nyumba kuwasili eneo la tukio kutoka jijini Mombasa.
Alipowasili Japhet Mumba, mwenye nyumba iliyonaswa mshukiwa wa mchawi, alithibitishia umati kuwa mshukiwa alikuwa ndani yanyumba yake na alikuwa amevalia baadhi ya nguo zake.
Kulingana na mtoto wa mzee mwenye nyumba, mtuhumiwa kwa jina Samson ambaye alikuwa na kitambaa chekundu mkononi, inadaiwa alipenya nyumbani akiwa uchi na akashindwa kutembea.
Aliongeza kuwa alipofika mlangoni alisimama hapo hadi mwenye nyumba alipofika na kumhoji.
Ilibainika nguo za mshukiwa alizozivua zilikuwa zingali nje ya nyumba alimokamatwa.
” Mimi niliona hii nyumba ina matatizo makubwa. Nisameheni”, alisema mshukiwa huyo wa ushirikina.
Ililazimu polisi waondoke na mtuhumiwa huyo ili kumnusuru kutoka kwa umati uliojawa na hasira.
Taarifa ya Lolani Kalu
News
Serikali yaombwa kuondoa miili 400 hospitali ya Malindi

Kamati ya afya ya bunge la seneti sasa imetoa wito kwa serikali kuu kuiondoa miili zaidi ya 400 ambayo inaendelea kuhifadhiwa katika makafani ya hospitali ya Malindi kaunti ya Kilifi baada ya kufukuliwa katika msitu wa Shakahola.
Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo, seneta wa kaunti ya Bungoma David Wakoli, alisema maiti hizo zimezuia serikali ya kaunti ya Kilifi kuendeleza ujenzi wa makafani mpya katika hospitali hiyo.
Wakoli alisema ikiwa serikali itazingatia hilo basi serikali ya kaunti ya Kilifi itaweza kujenga makafani hiyo bila changamotoz zozote.
“Tunataka kuiomba serikali kuu kuruhusu serikali ya kaunti ya Kilifi kuendeleza ujenzi huo, na serikali inapaswa kutafuta eneo maalumu la kuhifadhi na kuizika miili hiyo’’ Alisema Wakoli
Hii ni baada ya serikali kutenga fedha katika bajeti ya mwaka jana ili kujenga makafani mpya kushindwa kuendeleza ujenzi huo kutokana na miili ambayo bado haijatambuliwa.
Ni kauli ambayo iliungwa mkono na seneta wa kaunti ya Kilifi Stewart Madzayo ambaye aliitaka serikali kuu kukamilisha shughuli ya uambatanishaji wa chembechembe za msimbojeni-DNA, ili kupeana miili hiyo kwa wapendwa wao kabla ya kuanza kufukua miili mingine katika eneo la Kwa Binzaro huko Shakaholo.
“Kule Shakahola tumeona watu wanaendelea kufa na wengine kuzikwa, kwahivyo tunaomba zile maita ambazo ziko hapa ziweze kuondolewa na serikali kuu maana hakuna nafasi,’’ alisisitiza Madzayo.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Rais Ruto amteua Amani Yuda Komora kuwa Mwenyekiti wa NPSC

Rais William Ruto amemteua Amani Yuda Komora kuwa Mwenyekiti wa Tume ya kitaifa ya Huduma ya Polisi (NPSC) na Angeline Yiamiton Siparo kuwa mwanachama.
Uteuzi huo unafuatia mahojiano ya hivi majuzi yaliyofanywa na Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) kati ya Julai 1 na Julai 3 2025, baada ya kuorodhesha wagombea wanane wa uwenyekiti na 11 wa wajumbe.
Wawaniaji walitakiwa kuwasilisha kitambulisho halisi cha kitaifa, hati za masomo, na idhini halali kutoka kwa mashirika ya serikali.
Stakabadhi nyingine ilikuwa ni pamoja na nyaraka za mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini (KRA), tume ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC), fomu maalum kutoka kwa mkurugenzi wa idara ya upelelezi wa jinai (DCI), bodi ya mikopo ya elimu ya juu (HELB) na ofisi yoyote iliyosajiliwa ya marejeleo ya mikopo.
Wale walio na shahadi ya digrii za mataifa ya kigeni walilazimika kuwasilisha barua za utambulisho kutoka kwa tume ya elimu ya vyuo vikuu.
Shughuli ya uteuzi ilianza mnamo mwezi Februari baada ya kujiondoa kwa tume ya awali, inayoongozwa na Eliud Kinuthia, ambaye muhula wake wa miaka sita ulimalizika mapema mwaka huu wa 2025.
Iwapo itaidhinishwa na Bunge, NPSC itajumuisha Komora kama Mwenyekiti na wanachama watano wakiwemo, Peris Muthoni Kimani, Edwin Cheluget, Benjamin Juma Imai, Collete Suda na Angeline Yiamiton Siparo
Komora ni naibu mwenyekiti wa zamani wa tume ya kutathmini mishahara na marupurupu ya wafanyakazi wa umma (SRC), na hapo awali alikuwa na majukumu ya juu ya rasilimali watu katika Mamlaka ya Bandari KPA na KRA.
Taarifa ya Joseph Jira