News
Marekani yarusha makombora Iran, Trump akionya Tehran

Marekani imerusha mabomu kwenye maeneo ya Vinu vya Nyuklia vya Iran yanavyojumuisha Fordo na kuharibu kabisa maeneo hayo hatua ambayo huenda ikachangia vita zaidi ya kimataifa.
Rais wa Marekani Donald Trump alisema maeneo hayo yanayojumuisha Fordo, yalipigwa na makombora ya jeshi la Marekani huku Marekani ikijiunga na mashambulio ya Israel dhidi ya mpango wa Nyuklia wa Tehran.
Katika hatuba yake vya vyombo vya habari, Rais Trump alisema kwamba ni lazima Iran isitishe vita na kukumbatia amani iwapo wanataka vinu vyao vya Nyuklia kutorushiwa makombora.

Picha kwa hisani
“Tayari tumevuruga na kuharibu vinu vya Nyuklia vya Iran na bado tutaendelea kurusha makombora ya kasi zaidi na kuharibu vinu vyote vya Nyuklia vya Iran iwapo makao ya Tehran hayatasalimu amri”, alisema Rais Trump katika hotuba yake.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya nje wa Iran Seyed Abbas Araghchi alilaani vikali shambulizi la Marekani na kusema kwamba ni shambulizi la kuchukiza na kwamba Tehran ina njia zote za kutetea uhuru wake.
“Matukio ya asubuhi ya leo ni ya kuchukiza na yatakuwa na matokeo ya milele. Kila Mwanachama wa Umoja wa Mataifa ni lazima ashtushwe na tabia hii hatari sana, isiyo ya kisheria bali ni tabia ya kihalifu,” alisema Seyed.
Seyed aliongeza kwamba Marekani ilifanya ukiukaji mkubwa wa Katiba ya Umoja wa Mataifa kama Mwanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Waziri Joho na Mvurya waonya wanyakuzi wa ardhi.

Waziri wa madini na uchumi wa bahari nchini Ali Hassan Joho alisema serikali haitaruhusu tena wakaazi kufurushwa katika ardhi wanayoishi.
Akizungumza katika maeneo ya Mzambarauni mjini Mtwapa eneo bunge la Kilifi Kusini kaunti ya Kilifi, Joho alionya kwamba mabwenyenye wenye hulka ya kufurusha wananchi kwenye ardhi za umma kamwe hawataruhusiwa.
Joho alisema wananchi hawafai kuhangaishwa kwenye ardhi zao huku akiwatahadharisha maafisa wa serikali dhidi ya kushirikiana na mabwenyenye kuhangaisha raia kwenye ardhi zao.
Hii ni baada ya kuibuka malalamishi ya mabwenyenye kutaka kuwafurusha wakaazi wa Utange Kaunti ya Mombasa.
Kwa upande wake Waziri wa michezo na Sanaa nchini Salim Mvurya alidokeza kuwa serikali inapanga kununua mashamba ambayo hayatumiki ili kuyakabidhi ya wananchi.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Lagat, ahojiwa na IPOA kuhusu kifo cha Ojwang’

Naibu Inspekta jenerali wa polisi Eliud Lagat aliandikisha taarifa kwa maafisa wa uchunguzi wa Mamlaka ya kuchunguza utendakazi wa maafisa wa polisi nchini IPOA.
Lagat, aliandikisha taarifa hiyo kuhusu mauaji ya mwanablogu Albert Ojwang’, baada ya kuagizwa na IPOA kufika mbele ya maafisa hao kuhojiwa kwani alikuwa kati ya maafisa waliohusishwa na kifo cha Ojwang’.
Lagat ambaye alikuwa mlalamishi kwenye kesi hiyo ambayo inasemekana kwamba Marehemu Ojwang’ alituhumiwa kwa kuchapisha taarifa zisizo za ukweli kuhusu Lagat katika mitandao ya kijamii.
Kulingana na taarifa kutoka IPOA, Lagat alihojiwa kwa masaa kadhaa na maafisa wa uchunguzi wa kesi hiyo sawa na kuandikisha taarifa kuhusu kile anachokifahamu kuhusu kukamatwa na kusafirikishwa hadi katika kituo cha polisi cha Central jijini Nairobi.
Ripoti kuhusu kuhojiwa kwa Lagat japo haijawekwa wazi masuala ya ndani kuhusu mahojiano hayo, kuna tetesi kwamba afisa huyo wa polisi aliweka wazi kuhusiana na kukamatwa kwa Albert Ojwang’ kutoka pamoja na kilichojiri katika kituo cha polisi cha Central jijini Nairobi kabla ya kifo cha Ojwang’.
Lagat hata hivyo anaongeza idadi ya watu ambao tayari walihojiwa kuhusiana na mauaji ya Ojwang’ na kwamba kufikia sasa tayari maafisa 20 walifika mbele ya Mamlaka ya IPOA kuandikisha taarifa.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi