News
Manchester United Guu Moja Fainali Europa

Miamba wa Uingereza kilabu ya manchester united imeweka guu moja fainali ya UEFA Europa Ligi baada ya ushindi wao mnono wa magoli 3-0 dhidi ya Athletic Bilbao ugani san mames uhispania.
Kiungo wa taifa la Brazil Casemiro aliwaweka uongozi Mashetani wekundu kunako dakika 30 kipindi cha kwanza kabla ya nahodha Bruno Fernandes kuongeza goli la pili dakika ya 37 huku akifunga lingine na lake la pili dakika ya 45 kupitia tuta au penalty.
Kilabu ya Bilbao walimaliza wachezaji 10 baada ya kadi nyekundu kwa beki wake Dani vivian dakika ya 35. kwenye mechi nyingine Tottenham Hotspurs walicharaza Bodo/Glimt ya Norway magoli 3-1.
Kwenye taji la Uefa Conference ligi kilabu ya Chelsea ilichapa Djugarden ya uswedi magoli 4-1 nayo Real Betis ya Uhispania ikichakaza Fiorentina ya Italia magoli 2-1 .
Mechi za mkondo wa pili utapigwa Alhamisi ijayo ugani Old Trafford ambapo Bilbao itahitaji kuwafunga United magoli 4-0 ili kufuzu kwenye fainali Mei 21.
News
Anselim, ashutumu utovu wa usalama Taita Taveta

Kaimu Spika katika bunge la kaunti ya Taita Taveta Anselim Mwadime alieleza kusikitishwa na mauaji ya mhudumu mmoja wa bodaboda aliyeuliwa na kisha pikipiki yake kuchukuliwa katika eneo la chuo kikuu cha Taita Taveta.
Mwadime alisema kuna baadhi ya abiria ambao ni wahuni hubebwa na kisha kuwashambulia wahudumu wa pikipiki hadi kuwaua au hata kutoweka na pikipiki.
Aidha, Mwadime alisema kama viongozi wa kaunti ya Taita Taveta hawataruhusu visa hivyo kuendelezwa katika kaunti hiyo.
Vilevile, Mwadime aliishinikiza idara ya usalama kwenye kaunti ya Taita Taveta kuwajibika ipasavyo ili kudhibiti visa vya utovu wa usalama katika sekta ya bodaboda na wanaohusika wakabiliwe kisheria.
“Hili jambo linafaa kufuatiliwa kwa undani. Na tunalilaani vikali sisi kama viongozi wa Taita Taveta’’ alisema Mwadime.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Viongozi wahimizwa kushirikiana kubuni ajira kwa vijana

Mwakilishi wa wadi ya Sabaki eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi Rose Baraka alitoa wito kwa viongozi wa kaunti ya Kilifi kushirikiana na mashirika ya kijamii pamoja na wawekezaji katika kaunti ya Kilifi ili kudhibiti changamoto za ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.
Rose alisema hatua hiyo itasaidia pakubwa kuwaepusha vijana kujiingiza kwenye utumizi wa mihadarati sawa na uhalifu.
Akizungumza wakati wa kikao kilichowaleta pamoja maafisa wa shirika la SHOFCO pamoja na wakaazi wa Sabaki, Rose aliahidi kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kijamii katika juhudi za kuwasadia wananchi kujiendeleza kupitia mpango wa ajira.
“Vijana ni wengi, kazi ni kidogo. Sisi kama viongozi tunastahili kutia bidii kutafuta haya mashirika ili tuangalie vijana wetu wasaidika vipi’’ alisema Rose Baraka.
Kwa upande wake Afisa wa Shirika la SHOFCO eneo la Magarini Kelvin Mtawali Karisa aliupongeza ushirikiano wa mwakilishi wa wadi huyo na shirika hilo na kuwataka vijana kujiunga kwenye makundi mbalimbali ili waweze kupata mikopo ya kujiendeleza kimaisha.
Taarifa ya Janet Mumbi