News
Mahakama yasitisha ujenzi wa kanisa katika Ikulu ya Rais

Mahakama imesitisha ujenzi wowote wa kanisa la kudumu au hata maeneo ya ibada unaoweza kuendeshwa katika ikulu ya rais kwa sasa.
Mahakama pia ilisitisha ujenzi wa maeneo haya ya ibada kwenye ikulu ndogo zote nchini.
Jaji Chacha Mwita alitoa uamuzi huo kufuatia kesi iliyowasilishwa na mashirika ya kutetea haki za binaadam, ikiibua maswali kuhusu sheria, dini na majukumu ya serikali.
Walalamishi kwenye kesi hiyo walisema kuanzishwa kwa miundo mbinu ya kidini kwenye maeneo ya umma kama ikulu, kunaashiria ukiukaji mkubwa wa katiba.
Hatua ya kujengwa kwa kanisa katika ikulu ya rais iliibua hisia mseto nchini huku baadhi ya wananchi na viongizo wa dini wakipinga hatua hiyo.
Walidai hatua hiyo inaenda kinyume na sheria za taifa.
Kesi hiyo itatajwa tarehe 18 Novemba mwaka wa 2025.
Taarifa ya Joseph Jira
News
IEBC inaendelea kutambua vituo vya kusajili wapiga kura

Maafisa wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC wamesema wanaendelea na zoezi la kutambua sehemu za kuweka vituo vya kusajili wapiga kura hasa maeneo ya mashinani.
Afisa msimamizi wa tume ya IEBC eneo bunge la Ganze kaunti ya Kilifi, Mohammed Bahero Aboud alisema juhudi hizo ni kuhakikisha zoezi la usajili wapiga kura litakaloanza rasmi Septemba 29, mwaka huu linafaulu.
Akizungumza mjini Kilifi, Bahero alisema tume hiyo inatumia mbinu mpya ya kutambua vituo vya jadi vya usajili wapiga kura na kuweka vituo vipya kulingana na mapendekezo ya sheria.
Wakati huo huo alidokeza kwamba tume ya IEBC imekuwa ikihamashisha wakenya kutokubali kushawishiwa na wanasiasa na kujisajili katika maeneo yasiokuwa yao hasa msimu huu ambao zoezi hilo linakaribia kuanza.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Kaunti ya Mombasa kukumbatia matumizi ya mfumo wa miale ya jua

Serikali ya kaunti ya Mombasa imesema imeanza kutekeleza mpango wa kutumia nishati mbadala katika vituo vyote vya huduma za kaunti, kwa kuanza na mabadiliko ya mfumo wa taa hadi kutumia umeme wa miale ya jua.
Kwa mujibu wa waziri wa kawi, rasilimali asili na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kaunti ya Mombasa, Emily Achieng, hatua hii inalenga kupunguza gharama za matumizi ya umeme na kuhimiza matumizi ya nishati safi na rafiki kwa mazingira.
Mbali na hilo, waziri huyo alisema kaunti inaendelea kuweka vifaa maalum vya kupima ubora wa hewa katika maeneo mbalimbali ya mji na ndani ya taasisi za umma.
Lengo ni kupata ushahidi wa kisayansi kuhusu kiwango cha uchafuzi wa hewa, na kuchukuliwa kwa hatua za kisheria kwa wanaokiuka sheria.
Vifaa hivyo tayari vimewekwa katika hospitali ya rufaa ya Coast General na baadhi ya shule ikiwa ni sehemu ya mpango wa muda mrefu wa kaunti, kujenga ustahimilivu dhidi ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
Mikakati hiyo pia itasaidia kaunti katika kufanya maamuzi kuhusu maeneo yanayofaa kuwekwa biashara fulani, ili kulinda wananchi dhidi ya maradhi yanayosababishwa na uchafuzi wa hewa.
Taarifa ya Mwanahabari wetu.