News
Mahakama ya Kisutu nchini Tanzania imeahirisha kesi Lissu

Mahakama ya Kisutu nchini Tanzania imeahirisha kesi ya jinai inayomkabili Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu hadi Juni 16, 2025.
Mahakama imeagiza Lissu kuendelea kuzuiliwa rumande.
Uamuzi huo umetolewa baada ya kesi yake kutajwa Mahakamani ambapo upande wa serikali imeomba Mahakama kuupa muda zaidi ili kukamilisha uchunguzi dhidi ya mashtaka yanayomkabili Lissu.
Lissu anakabiliwa na mashtaka mbalimbali ikiwemo kosa la uhaini huku kesi hiyo ikifuatiliwa kwa karibu na umma kupitia matangazo ya moja kwa moja.
Mwenyekiti wa chama cha CHADEMA Tundu Lissu
Lissu ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA alikamatwa mwezi Aprili mwaka huu mkoani Ruvuma na kushtakiwa kwa tuhuma za uhaini na kuchapisha taarifa za uongo.
Mawakili wa Lissu wamewasilisha malalamiko kwa Umoja wa Mataifa wakitaka kutangazwa kwa kukamatwa na kuzuiliwa kwa Lissu kuwa kinyume cha sheria, wakisema mashtaka hayo yamechochewa kisiasa na yanalenga kumzuia Lissu kushiriki uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka 2025.
Taarifa ya Elizabeth Mwende
News
Godhana, awataka wakaazi kutoingiza siasa miradi ya maendeleo

Gavana wa kaunti ya Tana River Dhadho Godhana amewataka wenyeji wa kaunti hiyo kujiepusha na wanasiasa ambao wanaingiza siasa kwenye masuala ya maendeleo.
Godhana alisema hilo limechangia kaunti ya Tana River kusalia nyuma kimaendeleo hali ambayo itasababisha miradi mingi kuzidi kukwama.
Godhana alisema ni lazima viongozi na wenyeji wa kaunti ya Tana River washirikiane na uongozi wa kaunti ili kuafikia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Wakati huo huo Godhana aliesema mradi wa Village Cluster ambao umekuwa ukipingwa ndio utakaosaidia kudhibiti changamoto ambazo zinaikumba kaunti ya Tana River.
Naye Mahat Ali Loka ambaye ni Naibu Gavana wa kaunti ya Tana River, aliwaonya wanasiasa kutoka kaunti zingine dhidi ya kuingilia siasa za kaunti hiyo huku Spika wa bunge la kaunti hiyo Osman Noor Galole, akitoa onyo kwa wafanyikazi wa umma dhidi ya kujumu la serikali ya kaunti ya Tana River.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Mwili wapatikana baharini Shelly Beach Likoni

Polisi kaunti ya Mombasa wanachunguza kisa ambapo mwili wa mwanamme ambaye hajafahamika umepatikana ukielea katika maji ya bahari hindi kwenye ufuo wa Shelly Beach eneo bunge la Likoni.
Ripoti ya polisi ilibaini kuwa mwili huo uligunduliwa na wavuvi eneo hilo, ambao walipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Shelly Beach kuhusiana na tukio hilo.
Polisi walisema hawakubaini mara moja anakotoka mtu huyo.
Vile vile haikubainika iwapo marehemu alizama au aliuawa kabla ya mwili wake kutupwa baharini.
Polisi walisema hawajakutana na stakabadhi zozote za kumtambulisha mtu huyo huku wakiwasihi wananchi kutoa taarifa iwapo wanafahamu familia ya marehemu.
Mwili unahifadhiwa katika hifadhi ya maiti katika hospitali ya Rufaa ya Coast General Mombasa wakati uchunguzi zaidi ukiendelea.
Taarifa ya Joseph Jira