News
Mahakama ya Kilifi imetoa hukumu kwa wanaume 6 wanaokabiliwa na mashtaka ya unajisi

Mahakama ya Kilifi imetoa hukumu kwa wanaume 6 wanaokabiliwa na mashtaka ya unajisi.
Hakimu wa Mahakama hiyo Ivy Wasike alimhukumu Lucky Munga na Hassan Daniel kifungo cha miaka 30 gerezani baada ya Mahakama kubaini kwamba walihusika kwa kuwatendea unyama watoto wa umri wa miaka 13 na 15.
Safari Karisa Lewa alihukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani kwa kumnajisi mtoto wake mwenyewe wa umri wa miaka 14 huku Eric Ruwa na Lucky Katana Kenga wakihukumiwa kifungo cha miaka 6 gerezani kwa kosa sawa na hilo.
Hata hivyo Mahakama hiyo ilimhukumu kifungo cha miaka 3 Kithi Kombe kutokana na kesi hiyo kwa mtoto wa miaka 15, japo baadaye Mahakama ikabaini kwamba mshukiwa sio baba halali wa mtoto aliyezaliwa baada ya Kithi kumnajisi mtoto huyo.
Akizungumza wakati wa vikao vya Mahakama baada ya kutoa hukumu hizo, Hakimu Wasike alisema Mahakama umezingatia ushahidi uliyotolewa Mahakamani huku akiwarai wananchi kujitenga na visawishi vibaya ili kuepuka mkono wa sheria.
Hakimu Wasike alihoji kwamba washtakiwa wa haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama lakini kwa kuzingatia taratibu zote za Mahakama na sheria.
Taarifa ya Teclar Yeri
News
Thoya: Serikali kuu iongeze mgao wa fedha kwa sekta ya Afya

Naibu gavana wa kaunti ya Mombasa Francis Thoya ametoa changamoto kwa serikali kuu kuongeza mgao wa fedha ili kufanikisha utaoji wa huduma za afya.
Akizungumza katika kaunti hiyo, Thoya alisema kuwa huduma nyingi za afya katika kaunti hiyo ya Mombasa zinakabiliwa na changamoto ya raslimali ndogo hali ambayo inakwamisha juhudi za kuwahudumia wananchi ipasavyo.
Thoya pia alitaka serikali kuhakikisha inaharakisha kuajiri wahudumu zaidi wa afya ili wenyeji wa Mombasa waweze kupata huduma bora za matibabu bila changamoto zozote.
Aidha, Thoya alisema kwamba hali ya uhaba wa wahudumu wa afya ni changamoto kuu ambayo inazuia utoaji wa huduma bora za matibabu hali inayowafanya wale wachache waliopo kufanya kazi katika mazingira magumu.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Wazee wa Kaya walaumu mgawanyiko wa maandalizi ya Chendachenda

Mungano wa Wazee wa Kaya za Mijikenda umeelezea kusikitishwa na hatua ya serikali ya kaunti ya Kilifi ya kupanga kuandaa tamasha za tamaduni za jamii ya Mijikenda za Chendachenda katika chuo kikuu cha Pwani mbali na maelewano ya kuandaa tamasha hilo kaunti ya Kwale.
Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari Muungano huo ulitaja hatua hiyo kama ya kuwakosea heshima Wazee wa Kaya.
Wazee hao walidai kwamba hatua ya serikali ya kaunti ya Kilifi chini ya gavana Gedion Mung’aro inania ya kutenganisha jamii ya Mijikenda mbali na kuwaunganisha.
Aidha walisisitiza kuchukua msimamo na kuandaa tamasha hilo katika Kaya ya Mtswakara kaunti ya Kwale na yeyote atakayeenda kinyume na maamuzi ya Wazee hao atakumbana na laana za wazee.
Waliitaka serikali ya kaunti ya Kilifi kuomba msamaha kutokana na hatua hiyo.
Taarifa ya muungano wa wazee wa Kaya kwa vyombo vya habari
Awali tamasha hiyo iliandaliwa katika kaunti ya Kilifi na ilitarajiwa kuandaliwa katika kaunti tofauti kati ya kaunti sita za Pwani, kulingana na makubaliano ya jamii ya Mijikenda.
Hatua hii imeonekana kusababisha mgawanyiko miongoni mwa viongozi wa Kaya na viongozi wa siasa eneo la Pwani
Taarifa ya Joseph Jira