Business
KPA kuekeza kwenye miradi muhimu

Mamlaka ya bandari ya nchini (KPA) imesema itaendelea kuekeza katika miradi muhimu ya miundombinu ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya usafirishaji wa mizigo kupitia reli, baharini na barabara.
Meneja mkuu wa operesheni za mizigo katika KPA, Dkt. Sudi Mwasinago, alisema kuwa uwekezaji huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi katika shughuli za bandari, hasa kufuatia uimarishaji wa mifumo ya kiutendaji na ununuzi wa vifaa vya kisasa.
Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha wadau kutoka KPA, shirika la reli nchini (KRC), na maafisa kutoka Etihad Rail ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Dkt. Mwasinago alisema kuwa ushirikiano kati ya mashirika hayo ni hatua muhimu katika kuimarisha sekta ya usafirishaji nchini.
Dkt. Mwasinago, alisema KPA inaendelea kujenga mazingira bora ya biashara kwa kuunganisha bandari na miundombinu mingine ya usafiri, ikiwa ni pamoja na reli ya kisasa ya SGR na barabara kuu, ili kuhakikisha mchakato wa usambazaji wa bidhaa unakuwa mwepesi na wenye tija.
Aidha, kampuni ya Etihad Rail, ilionyesha nia ya dhati ya kushirikiana na Kenya katika uendelezaji wa mtandao wa reli wa kisasa ili kuboresha viwango vya usafiri wa reli nchini, sambamba na kukuza biashara ya kimataifa kupitia bandari ya Mombasa.
Taarifa ya Mwanahabari
Business
Mradi wa kiuchumi wa Dongo Kundu wavutia wawekezaji zaidi

Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wanaendelea kuonyesha nia ya kuekeza katika mradi wa kiuchumi wa dongo kundu kaunti ya Mombasa.
Mradi huo unaotarajiwa kuongeza uzalishaji katika viwanda na thamani ya bidhaa ndani ya nchi na nje, unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
Kampuni ya nishati kutoka China, Ruike Energy Group Limited, ni mwekezaji wa hivi karibuni kuonyesha nia ya kupata nafasi ndani ya eneo hilo la kiuchumi la Dongo Kundu kwa ajili ya kuanzisha kiwanda cha kusafisha mafuta.
Kulingana na halmashauri ya bandari nchini KPA hatua hiyo italeta faida Zaidi ikiwemo kubuni nafasi za ajira, ikuaji wa uchumi, upatikanaji wa vifaa vya baharini, na urahisi wa kufikia masoko ya kanda na ya kimataifa.
Taarifa ya Pauline Mwango
Business
KETRACO kuimarisha usalama wa chakula nchini

Shirika la usambazaji umeme nchini, KETRACO, limethibitisha dhamira yake ya kuimarisha usalama wa chakula, ukuaji wa kijani, na ushirikiano wa kieneo kupitia uekezaji mkubwa katika miundombinu ya umeme.
Katika maonesho ya Kimataifa ya kilimo ASK yanayoendelea kaunti ya Mombasa, KETRACO imeonyesha jinsi miundombinu yake ya umeme inavyowezesha kilimo cha kisasa na uzalishaji wa viwandani.
Kwa mujibu wa kaimu mkurugenzi mkuu, mhandisi Kipkemoi Kibias, KETRACO imekamilisha miradi 43 ya njia za kusafirisha umeme, huku mingine 29 ikitarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2028.
Kibias, alisema shirika hilo tayari limejenga zaidi ya kilomita elfu sita za njia za umeme wa msongo mkubwa, likiwa pia na vituo 46 vya kusambaza umeme na upanuzi wa mitambo 33.
Katika eneo la Pwani, Kibias alisema upanuzi wa mpango wa Green Energy Backbone umewezesha usambazaji wa kawi safi kwa asilimia 93, jambo lililopunguza utegemezi wa mafuta na kuchochea maendeleo ya biashara za kilimo, utalii na uchumi wa baharini.
Kibias alisema KETRACO inaendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa na kuunganisha Kenya na nchi jirani kupitia njia za kimataifa kama zile za Ethiopia, Tanzania na Uganda hatua zitakazowezesha biashara ya umeme Afrika Mashariki.
Taarifa ya Mwanahabari wetu