News
Kenya Yatoa ufadhili wa Asilimia 20 kwa WHO

Kenya imejitolea kuongeza ufadhili wake kwa Shirika la Afya duniani WHO kwa asilimia 20 katika kipindi cha miaka 4 ijayo.
Waziri wa Afya nchini Aden Duale ameyasema hayo wakati wa Kongamano la 78 la Afya duniani linaloendelea mjini Geneva nchini Uswizi, ambapo amesisitiza haja ya serikali ya Kenya kujitolea katika kuboresha sekta ya afya ulimwenguni.
Waziri Duale amesisitiza umuhimu wa ufadhili endelevu kwa Shirika la Afya duniani WHO, akisema licha ya bajeti kurekebishwa na kuweka ufadhili huo mdogo pia utasaidia sekta ya afya.
Waziri Duale ameangazia dhamira ya serikali ya Kenya ya kuhakikisha wananchi wananufaika na huduma za afya kwa wote UHC, kuimarishwa kwa ufadhili wa afya na kuendeleza miundombinu ya afya ya kidijitali ili kuendesha sera inayotumia data.
Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus amepongeza kujitolea kwa mataifa wanachama katika kufadhili WHO, akisema ahadi zilizotolewa na mataifa hayo zitachangia kuimarika kwa sekta ya afya duniani.
News
Serikali yaombwa kuondoa miili 400 hospitali ya Malindi

Kamati ya afya ya bunge la seneti sasa imetoa wito kwa serikali kuu kuiondoa miili zaidi ya 400 ambayo inaendelea kuhifadhiwa katika makafani ya hospitali ya Malindi kaunti ya Kilifi baada ya kufukuliwa katika msitu wa Shakahola.
Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo, seneta wa kaunti ya Bungoma David Wakoli, alisema maiti hizo zimezuia serikali ya kaunti ya Kilifi kuendeleza ujenzi wa makafani mpya katika hospitali hiyo.
Wakoli alisema ikiwa serikali itazingatia hilo basi serikali ya kaunti ya Kilifi itaweza kujenga makafani hiyo bila changamotoz zozote.
“Tunataka kuiomba serikali kuu kuruhusu serikali ya kaunti ya Kilifi kuendeleza ujenzi huo, na serikali inapaswa kutafuta eneo maalumu la kuhifadhi na kuizika miili hiyo’’ Alisema Wakoli
Hii ni baada ya serikali kutenga fedha katika bajeti ya mwaka jana ili kujenga makafani mpya kushindwa kuendeleza ujenzi huo kutokana na miili ambayo bado haijatambuliwa.
Ni kauli ambayo iliungwa mkono na seneta wa kaunti ya Kilifi Stewart Madzayo ambaye aliitaka serikali kuu kukamilisha shughuli ya uambatanishaji wa chembechembe za msimbojeni-DNA, ili kupeana miili hiyo kwa wapendwa wao kabla ya kuanza kufukua miili mingine katika eneo la Kwa Binzaro huko Shakaholo.
“Kule Shakahola tumeona watu wanaendelea kufa na wengine kuzikwa, kwahivyo tunaomba zile maita ambazo ziko hapa ziweze kuondolewa na serikali kuu maana hakuna nafasi,’’ alisisitiza Madzayo.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Rais Ruto amteua Amani Yuda Komora kuwa Mwenyekiti wa NPSC

Rais William Ruto amemteua Amani Yuda Komora kuwa Mwenyekiti wa Tume ya kitaifa ya Huduma ya Polisi (NPSC) na Angeline Yiamiton Siparo kuwa mwanachama.
Uteuzi huo unafuatia mahojiano ya hivi majuzi yaliyofanywa na Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) kati ya Julai 1 na Julai 3 2025, baada ya kuorodhesha wagombea wanane wa uwenyekiti na 11 wa wajumbe.
Wawaniaji walitakiwa kuwasilisha kitambulisho halisi cha kitaifa, hati za masomo, na idhini halali kutoka kwa mashirika ya serikali.
Stakabadhi nyingine ilikuwa ni pamoja na nyaraka za mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini (KRA), tume ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC), fomu maalum kutoka kwa mkurugenzi wa idara ya upelelezi wa jinai (DCI), bodi ya mikopo ya elimu ya juu (HELB) na ofisi yoyote iliyosajiliwa ya marejeleo ya mikopo.
Wale walio na shahadi ya digrii za mataifa ya kigeni walilazimika kuwasilisha barua za utambulisho kutoka kwa tume ya elimu ya vyuo vikuu.
Shughuli ya uteuzi ilianza mnamo mwezi Februari baada ya kujiondoa kwa tume ya awali, inayoongozwa na Eliud Kinuthia, ambaye muhula wake wa miaka sita ulimalizika mapema mwaka huu wa 2025.
Iwapo itaidhinishwa na Bunge, NPSC itajumuisha Komora kama Mwenyekiti na wanachama watano wakiwemo, Peris Muthoni Kimani, Edwin Cheluget, Benjamin Juma Imai, Collete Suda na Angeline Yiamiton Siparo
Komora ni naibu mwenyekiti wa zamani wa tume ya kutathmini mishahara na marupurupu ya wafanyakazi wa umma (SRC), na hapo awali alikuwa na majukumu ya juu ya rasilimali watu katika Mamlaka ya Bandari KPA na KRA.
Taarifa ya Joseph Jira