Uncategorized
Kaunti ya Mombasa Yatakiwa Kuchukua Hatua za Dharura Kusafisha Soko la Marikiti

MOMBASA – Serikali ya Kaunti ya Mombasa imetakiwa kuchukua hatua za haraka kuondoa taka zilizorundikana katika soko la Marikiti, hatua inayolenga kupunguza hatari ya kiafya na uvundo unaosababishwa na uchafu huo, hasa katika msimu huu wa mvua.
Akizungumza na wanahabari, Mwenyekiti wa soko hilo, Muhammad Ali, amesema kuwa hali ya uchafu sokoni hapo imefikia kiwango cha kutisha, huku baadhi ya wanunuzi wakikwepa kufika sokoni humo kutokana na harufu kali na mazingira yasiyovutia.
“Tumejaribu kuwasiliana na serikali ya kaunti mara kadhaa kuhusu suala hili, lakini hadi sasa hatujapata suluhisho la kudumu. Taka zimejaa kila kona ya soko, na hali hii si tu inatishia afya ya wananchi, bali pia inasababisha hasara kwa wafanyabiashara,” alisema Ali.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, mvutano kati ya serikali ya kaunti na baadhi ya wafanyabiashara kuhusu ni nani anapaswa kukusanya taka umekuwa kizingiti kikuu katika kutatua changamoto hiyo. Hata hivyo, amesisitiza kuwa ni jukumu la moja kwa moja la serikali ya kaunti kuhakikisha kuwa huduma za ukusanyaji taka zinatolewa kwa wakati katika masoko yote ya umma.
“Hili si suala la kubebana lawama. Serikali ya kaunti ina wajibu wa kuhakikisha mazingira safi na salama kwa wafanyabiashara na wateja,” aliongeza.
Wafanyabiashara sokoni Marikiti wanasema hali hiyo imeathiri sana mapato yao, huku wakiitaka kaunti kuingilia kati na kurejesha heshima ya soko hilo linalohudumia maelfu ya wakazi wa Mombasa kila siku.
News
Ujenzi wa Barabara ya Kuelekea Timbo za Jaribuni Kuanza

Kikao cha kutafuta mwafaka kuhusu mzozo uliyoshuhudiwa kati ya wakaazi wa eneo la Jaribuni kaunti ya Kilifi na wawekezaji wa timbo za eneo hilo uliyosababisha kufungwa kwa barabara, kilifanyika ramsi.
Kikao hicho kilichoongozwa na Waziri wa madini na Uchumi samawati nchini Ali Hassan Joho kilijumuisha pia wawekezaji wa timbo hizo na wenyeji kama hatua moja wapo ya kuibuka na mwafaka.
Kikao hicho ambacho pia kilihudhuriwa na Gavana wa Kilifi Gedion Mung’aro kimeshuhudia kuanzishwa kwa mradi wa ujenzi wa barabara zinazoelekea katika timbo za eneo hilo la Jaribuni.
Japo barabara hizo zimesalia kufungwa kufuatia maandamano yaliyoshuhudiwa ya wenyeji wakilalamikia uchafuzi wa mazingira, ubovu wa barabara pamoja na kupuuzwa kwa miradi ya maendeleo, huenda sasa mwafaka wa mzozo huo ukapatikana
News
Mwaura: Hakuna Mswada wa Fedha wa Mwaka 2025 uliyowasilishwa Bungeni

Serikali imejitokeza na kupinga taarifa zinazoendelea katika mitandao ya kijamii kwamba inalenga kuwasilisha mswada wa fedha wa mwaka wa 2025 bungeni ambao unalenga kuongeza ushuru kwa wakenya.
Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura amesema taarifa hizo ni propaganda zisizo na ukweli wowote na ambazo zinalenga kuwagonganisha wakenya kama ilivyoshuhudiwa mwezi Juni mwaka wa 2024 wakati wananchi walipozua vurugu kupinga mswada wa fedha.
Katika kikao na Wanahabari katika jumba la mikutano la KICC jijini Nairobi, Mwaura amesema japo serikali iko na mipango ya kutengeneza bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2025/2026, ni lazima wananchi wahusishwe kikamilifu katika vikao vya kutoa maoni ya umma.
Msemaji huyo wa serikali amebainisha kwamba serikali itahakikisha inawashikiza wakenya wanaokwepa kulipa ushuru kuwajibika huku akisema wakenya zaidi ya milioni 8.5 wamenufaika na bima ya Afya ya Taifa Care.
Wakati huo huo ameelezea hatua zilizopigwa na serikali za kimaendeleo katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili sasa, akisisitiza haja ya wakenya kuunga mkono serikali kufanikisha ajenda yake ya maendeleo kwa wananchi wote.