News
Karisa Ngirani: Baadhi ya wadi Ganze zimetelekezwa na Kaunti

Mwakilishi wadi ya Ganze Karisa Ngirani anadai baadhi ya wadi ndani ya eneo bunge la Ganze zimekuwa zikitelekezwa katika maswala ya ugavi wa raslimali katika kaunti ya Kilifi.
Katika mahojiano na COCO FM, Ngirani alisema wamekuwa wakishinikiza serikali kuangazia matatizo ya wakaazi maeneo hayo ili kuhakikisha wakaazi wanafaidi miradi ya maendeleo.
Ngirani aliadai aliwasilisha hoja katika bunge la kaunti kuangazia usawa wa ugavi wa raslimali, baada ya baadhi ya wawakilishi wadi kulalamikia suala hilo.
Kulingana na mwakilishi huyo wa wadi hoja hiyo ilitupiliwa mbali licha ya kukubaliwa na wananchi baada ya kuandaa vikao vya kukusanya maoni ya umma.
“Nilikuja na hoja ambayo inaitwa “equitable bill” inaangazia usawa wa raslimali vile tunazigawanya kwa kila wadi, manake nilipoingia pale wawakilishi wengi walikuwa wanalalamika, ukiangalia ni kweli, unaangalia labda kuna mwakilishi wadi ambaye yuko karibu na gavana, huyo unapata bajeti ikitengenezwa ako na asilimia kubwa sana, lakini naskia imerejeshwa na viongozi wa juu”,alidai Ngirani
Vile vile Ngirani alidokeza kuwa suala la uhaba wa maji safi ya matumizi kwa wakaazi wa Ganze limesalia changamoto licha ya pesa zilizotengewa miradi ya maji kutolewa kwenye bajeti ya ziada.
Akiangazia masuala ya mazingira Ngirani alisema wanashirikiana na mashiriki mbali mbali kufanikisha utunzaji mazingira katika kaunti ya Kilifi, na wanapanga kuwasilisha hoja bungeni itakayotoa fursa kwa wananchi ndani ya kaunti, kutenga sehemu ya ardhi ili kuwezesha upanzi wa miti.
Alidokeza kuwa idara ya mazingira imekuwa ikitengewa mgao wa chini mno wa fedha hali ambayo imekuwa vigumu kutekeleza miradi ya kuboresha mazingira ili kukabili mabadiliko ya tabia nchi.
“Saa hii tunasukuma tuweke mswada kwamba angalau kila eneo liwe na msitu, litenge sehemu kadhaa ya ardhi ili iwe inapandwa miti iwe ni kama shamba ambalo wananchi wanawezapeana”, alisema Mwakilishi huyo wa wadi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu.
News
Mombasa inaongoza kwa maambukizi ya MPOX nchini

Wizara ya afya nchini imesema kaunti ya Mombasa inaongoza kwa visa vya maambukizi ya ugonjwa wa Mpox.
Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa idara ya afya nchini Daktari Patrick Amoth, kaunti ya Mombasa imerekodi visa 139 kati ya visa 300 vilivyoripotiwa na wizara hiyo.
Amoth alidokeza kuwa serikali itatangaza siku maalum ya kutoa chanjo ya kudhibiti msambao wa ugonjwa huo wakishirikiana na shirika la afya ulimwenguni WHO.
Mkurugenzi huyo vile vile alimesema zoezi hilo litaambatana na hamasa kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na maambukizi zaidi.
“Kwa wakati huu Mombasa ndio inaongoza kwa idadi ya visa 139 kwa hivyo tuchuke tahadhari kuhakikisha kwamba tunazuia maambukizi, na tunafanya mpango pamoja na shirika la afya duniani WHO, hapa tutakuja na mpango wa chanjo na ikifika huo wakati tunaomba watu wajitokeze wapate chanjo ili wapate kinga”,alisema Daktari Amoth.
Wakati huo huo Amoth aliokeza kuwa uchunguzi wa vifo vya watu wanne walioaga dunia wiki chache zilizopita huko Migadini, eneo bunge la Changamwe kaunti ya Mombasa umebaini walifariki kutokana na magonjwa mengine na wala sio maambukizi ya ugonjwa wa MPOX kama ilivyodhaniwa na wakaazi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu.
News
Wavuvi wawili wafa maji Watamu,Kilifi

Jamii ya wavuvi katika eneo la Watamu eneo bunge la Kilifi Kaskazini inaiomba serikali ya kaunti ya Kilifi na ile ya kitaifa kununua boti za uokozi ili kusaidia kuokoa maisha wakati kunapotokea dharura baharini.
Hii ni baada ya wavuvi wawili kupotoea katika bahari hindi eneo la Watamu walipokuwa wakiendeleza shughuli zao za uvuvi siku ya Alhamisi 24, Julai 2025.
Kufikia sasa wawili hao hawajapatikana licha ya juhudi za wadau mbalimbali ikiwemo jeshi la wanamaji kuwatafuta.
Kiongozi wa vijana eneo la Watamu Bakari Shaban, alisema kuwa juhudi za kuwatafuta wavuvi hao ambao ni mandugu wanaotambulika kama Athman Lali na Huzefa Lali zinaendelea.
Shaban alisistiza haja ya serikali kuangazia suala la ununuzi wa mashua za kisasa za uokozi ili kupunguza visa vya wavuvi kuangamia baharini wakati wanapoelekea kuvua.
“Mpaka sasa juhudi zote zimefanyika lakini ndugu zetu hatujajua wako sehemu gani, serikali itusaidie mji wetu wa Watamu ni mji wa utalii, tunaomba tupate boti za kuokoa maisha baharini, popote alipo waziri Ali Joho angalau tupate boti za uokozi kama mbili hapa Watamu ni kitovu cha utalii kunamahoteli mengi, watalii wote wanaokuja Watamu mpaka leo hakuna boti za uokozi”, alisema Shaban.
Kwa upande wao wazazi wa wavuvi waliopotea baharini Lali Athman Lali na Dhurai Mohamed Ali waliiomba serikali kuweka juhudi zaidi za kuwasaidia kuwapata wana wao kwani ndio tegemeo kubwa kwa familia yao.
“Uko usaidizi unatumika, kuna vijana wanaojitolea kwa maboti wanaenda ile sehemu ambayo wavuvi wanavua, wanajaribu kuzunguka lakini toka siku hiyo hawajapata chochote: Katika Maisha yangu mimi nawategemea hawa watoto kunisomeshea hawa watoto wangu ambao ni wadogo zao mashule, kwa chakula kwa hivyo naomba serikali inisaidie kwa sababu ndio tegemeo langu hao watoto”.walisema wazazi.
Kisa hiki kinajiri miezi kadhaa baada ya mvuvi mmoja kutoka eneo la Mnarani mjini Kilifi kufariki baharini baada ya kugongwa kichwani kwa pondo na wavuvi wenzake kulipotokea mzozo kuhusu pato la samaki.
Kufikia sasa mwili wa mvuvi huyo haujapatikana
Taarifa ya Mwanahabari wetu