Entertainment
Justin Bierber Arejea na Album Mpya ‘SWAGG’

Msanii nyota wa muziki wa kimataifa, Justin Bieber, hatimaye ameachia rasmi albamu yake mpya na ya saba kwa jina “Swag”, ikiwa ni albamu yake ya kwanza tangu mwaka 2021 alipotoa Justice. Albamu hii imetoka leo na tayari imeanza kutikisa majukwaa mbalimbali ya muziki duniani.
Swag imejumuisha mastaa kadhaa akiwemo Gunna, Sexyy Red, Cash Cobain, pamoja na wasanii wengine wa kizazi kipya.
Albamu hiyo ina jumla ya nyimbo 20 na tayari baadhi ya vibao kama “Go Baby”, “Soulful” na Butterflies “zimeanza kupokelewa vizuri kwenye mitandao ya Spotify, Apple Music na YouTube.
Hii ni mara ya kwanza kwa Bieber kuachia albamu tangu alipopata matatizo ya kiafya mwaka 2022 yaliyosababisha asitishe ziara yake ya kimataifa ya Justice World Tour ambayo ilikuwa iendelee hadi mwaka 2023.
Ziara hiyo ilisitishwa mnamo Septemba 2022 baada ya Bieber kupatwa na maradhi ya Ramsay Hunt Syndrome, ugonjwa uliomsababishia kupooza upande mmoja wa uso.
Kwa kipindi cha miaka minne bila kazi mpya, mashabiki wa Justin Bieber duniani wamekuwa wakimsubiria kwa hamu ujio wa kazi mpya kutoka kwake. Kupitia Swag, msanii huyo ameonyesha kurejea kwa nguvu na ubunifu wa hali ya juu, huku akiwa katika hali nzuri kiafya na kisaikolojia.
Taarifa na Francos Mzungu
Entertainment
Mboga Imejileta; Arrow Bwoy Aitisha Pigano Dhidi ya Shakib

Msanii maarufu wa Kenya, Arrow Bwoy, amezua gumzo mtandaoni baada ya kumualika wazi wazi mfanyabiashara kutoka Uganda, Shakib Cham, kwenye pambano la ndondi.
Hii imekuja baada ya kipigo cha hadharani ambacho Shakib alipokea kutoka kwa msanii mwenzake wa Uganda, Rickman, hali iliyoacha mashabiki wengi wakisema: “Sasa ata Arrow Bwoy anaweza!”
Kupitia video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Arrow Bwoy, anayefahamika kwa vibao kama Digi Digi, hakuonyesha woga wowote. Kwa ucheshi, alisema amekuwa akisubiri nafasi kama hii kwa muda mrefu.
“Mboga imejileta,” alisema kwa kujiamini, akimaanisha kuwa Shakib amejileta mwenyewe kwenye kipigo.
“Chakula kiko tayari. Niko tayari kwa pambano hili.”
Arrow Bwoy pia hakusita kumtaja mke wa Shakib, Zari Hassan, akimtaka akae mbali na ulingo siku ya pambano hilo kwa usalama wake binafsi.
“Zari, usijisumbue kuja. Hii si sehemu ya wanawake. Usije ukazimia tukapata janga la pili,” alisema kwa kejeli.
Hata hivyo, wakosoaji wake walikumbusha jamii kuhusu video za awali zinazoonyesha Arrow Bwoy akichapwa na polisi wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha. Swali likabaki: Je, kweli ana uwezo wa kumpiga Shakib au ni porojo za mitandaoni?
Kwa jina la Zari kuingizwa kwenye sakata hili, mvutano umeongezeka na mashabiki kote Afrika Mashariki wanasubiri kuona kama Shakib atakubali changamoto hii ya kihistoria.
“Zari, kama unasikia, mtume tu kijana wako aje achukue kichapo — kichapo cha kimataifa,” Arrow Bwoy alimalizia kwa msisitizo.
Kwa sasa, macho yote yako kwa Shakib. Je, atakubali changamoto hii na kuweka historia mpya ya burudani Afrika Mashariki?
Entertainment
#CHAN2024: Savara, Zuchu na Eddy Kenzo Kutumbuiza Fainali ya CHAN 2024 Nairobi

Mashindano ya CHAN 2024 yakielekea ukingoni, mashabiki wanatarajiwa kupata burudani ya aina yake kutoka kwa baadhi ya nyota wakubwa wa muziki Afrika Mashariki.
Kenya, Uganda na Tanzania zitawakilishwa vilivyo kupitia majina makubwa matatu: Savara wa Kenya (mwanachama wa zamani wa kundi maarufu Sauti Sol), Eddy Kenzo wa Uganda, na Zuchu kutoka Tanzania, anayejulikana kwa jina halisi Zuhura Othman.
Onyesho hili la kufunga pazia litafanyika sambamba na mechi ya fainali Jumamosi, likitarajiwa kuhamasisha na kuburudisha maelfu ya mashabiki watakaofurika uwanja wa Kasarani. Shoo hiyo inalenga kumaliza mashindano haya ya kihistoria kwa upekee na kiwango cha juu cha burudani.
Mbali na kusubiriwa kwa hamu jukwaani, Savara pia amekuwa na mchango mkubwa nyuma ya pazia. Yeye ndiye mtunzi na mtayarishaji wa wimbo rasmi wa CHAN 2024 unaoitwa “Pamoja”.
Wimbo huo unashirikisha nyota kutoka kanda hii: Elijah Kitaka wa Uganda na Phina wa Tanzania. Uliimbwa kwa mara ya kwanza katika sherehe za ufunguzi na uliweka ladha na hamasa ya mashindano haya.
Ingawa wenyeji wa mashindano haya—Kenya, Uganda na Tanzania—waliishia katika hatua ya robo fainali, fainali za mwaka huu zinaahidi kuwa kilele cha msisimko.
Burudani kutoka kwa Zuchu, Savara na Eddy Kenzo itakuwa chachu ya kuhitimisha mashindano yaliyojaa matukio na hisia.
Kwa upande mwingine, kumekuwa na malumbano mitandaoni kati ya mashabiki wa Kenya na Tanzania, hususan baada ya timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, kudondoshwa nje ya michuano hiyo katika robo fainali.
Mashabiki wa Tanzania hawakusita kuchokoza wenzao kwa kejeli, jambo lililoongeza ladha ya ushindani wa nje ya uwanja.