Entertainment
#Janjaruka254: Safari ya Omwami ya Kuchekesha Dunia
Kicheko ni dawa, lakini safari ya kumfanya mtu acheke si ya mchezo. Hii ni kauli inayomwelezea vyema Omwami Comedian, mchekeshaji anayezidi kung’aa kwenye anga la burudani humu nchini. Katika mahojiano ya kipekee na Janjaruka 254, Omwami amefunguka kuhusu safari yake ya kuwa mchekeshaji, akieleza changamoto, matumaini, na nguvu ya kutokata tamaa.
Omwami anasema kipaji chake cha ucheshi kilianza kujionyesha tangu akiwa mtoto. Alikuwa na tabia ya kunakili sauti na maneno ya wageni waliotembelea familia yao, kisha baadaye kuwaigiza mara tu walipoondoka. “Nilikuwa kama runinga ya familia. Watu walinifurahia lakini pia walikuwa makini wakija kwetu, maana walijua nitaigiza kila kitu walichosema,” Omwami alisema kwa tabasamu.
Akiwa shule ya upili, Omwami alijiunga na kundi la waigizaji. Hapo ndipo kipaji chake kilianza kung’aa rasmi. Hata hivyo, safari hiyo haikuwa rahisi kwani mama yake hakufurahishwa na ushiriki wake katika sanaa akiamini angerudi nyuma masomoni.
“Mama alikuja shule kuniambia niachane na drama club, lakini mwalimu mkuu alikataa kwa sababu aliona nina kipaji,” alisema.
Omwami anasema kupata nafasi ya kuigiza kwenye kipindi maarufu cha Churchill Show haikuwa lelemama. Alifanya auditions zaidi ya tatu kabla ya kupata nafasi ya kuonesha uwezo wake.
“Ilichukua muda na maombi. Lakini siku moja nilipofanikisha, nilijua ndoto yangu inaanza kutimia,” alisema.
Katika harakati zake, Omwami hakusahau kumtaja mchekeshaji maarufu Eric Omondi na Victor Ber kama watu waliompa moyo wa kuendelea kufanya anachokipenda. “Eric aliniambia nina uwezo mkubwa na nisikate tamaa. Hilo lilinipa nguvu kuendelea na leo hii, naona matunda ya uvumilivu,” alieleza kwa shukrani.
Omwami anahitimisha kwa kutoa wosia kwa vijana na mtu yeyote anayefuatilia ndoto yake. “Usikate tamaa. Haijalishi changamoto ni kubwa kiasi gani, ukijitahidi na kuomba, siku moja utafanikiwa.”
Safari ya Omwami ni ushuhuda kuwa mafanikio hayaji kwa urahisi. Inahitaji bidii, kujitoa, na imani. Kwa wale wanaotafuta nafasi yao kwenye sanaa au nyanja nyingine yoyote, hadithi ya Omwami ni mfano wa kuigwa – kuwa huwezi chekesha dunia kabla hujajifunza kuvumilia vizingiti vyake.
Entertainment
Mboga Imejileta; Arrow Bwoy Aitisha Pigano Dhidi ya Shakib

Msanii maarufu wa Kenya, Arrow Bwoy, amezua gumzo mtandaoni baada ya kumualika wazi wazi mfanyabiashara kutoka Uganda, Shakib Cham, kwenye pambano la ndondi.
Hii imekuja baada ya kipigo cha hadharani ambacho Shakib alipokea kutoka kwa msanii mwenzake wa Uganda, Rickman, hali iliyoacha mashabiki wengi wakisema: “Sasa ata Arrow Bwoy anaweza!”
Kupitia video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Arrow Bwoy, anayefahamika kwa vibao kama Digi Digi, hakuonyesha woga wowote. Kwa ucheshi, alisema amekuwa akisubiri nafasi kama hii kwa muda mrefu.
“Mboga imejileta,” alisema kwa kujiamini, akimaanisha kuwa Shakib amejileta mwenyewe kwenye kipigo.
“Chakula kiko tayari. Niko tayari kwa pambano hili.”
Arrow Bwoy pia hakusita kumtaja mke wa Shakib, Zari Hassan, akimtaka akae mbali na ulingo siku ya pambano hilo kwa usalama wake binafsi.
“Zari, usijisumbue kuja. Hii si sehemu ya wanawake. Usije ukazimia tukapata janga la pili,” alisema kwa kejeli.
Hata hivyo, wakosoaji wake walikumbusha jamii kuhusu video za awali zinazoonyesha Arrow Bwoy akichapwa na polisi wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha. Swali likabaki: Je, kweli ana uwezo wa kumpiga Shakib au ni porojo za mitandaoni?
Kwa jina la Zari kuingizwa kwenye sakata hili, mvutano umeongezeka na mashabiki kote Afrika Mashariki wanasubiri kuona kama Shakib atakubali changamoto hii ya kihistoria.
“Zari, kama unasikia, mtume tu kijana wako aje achukue kichapo — kichapo cha kimataifa,” Arrow Bwoy alimalizia kwa msisitizo.
Kwa sasa, macho yote yako kwa Shakib. Je, atakubali changamoto hii na kuweka historia mpya ya burudani Afrika Mashariki?
Entertainment
#CHAN2024: Savara, Zuchu na Eddy Kenzo Kutumbuiza Fainali ya CHAN 2024 Nairobi

Mashindano ya CHAN 2024 yakielekea ukingoni, mashabiki wanatarajiwa kupata burudani ya aina yake kutoka kwa baadhi ya nyota wakubwa wa muziki Afrika Mashariki.
Kenya, Uganda na Tanzania zitawakilishwa vilivyo kupitia majina makubwa matatu: Savara wa Kenya (mwanachama wa zamani wa kundi maarufu Sauti Sol), Eddy Kenzo wa Uganda, na Zuchu kutoka Tanzania, anayejulikana kwa jina halisi Zuhura Othman.
Onyesho hili la kufunga pazia litafanyika sambamba na mechi ya fainali Jumamosi, likitarajiwa kuhamasisha na kuburudisha maelfu ya mashabiki watakaofurika uwanja wa Kasarani. Shoo hiyo inalenga kumaliza mashindano haya ya kihistoria kwa upekee na kiwango cha juu cha burudani.
Mbali na kusubiriwa kwa hamu jukwaani, Savara pia amekuwa na mchango mkubwa nyuma ya pazia. Yeye ndiye mtunzi na mtayarishaji wa wimbo rasmi wa CHAN 2024 unaoitwa “Pamoja”.
Wimbo huo unashirikisha nyota kutoka kanda hii: Elijah Kitaka wa Uganda na Phina wa Tanzania. Uliimbwa kwa mara ya kwanza katika sherehe za ufunguzi na uliweka ladha na hamasa ya mashindano haya.
Ingawa wenyeji wa mashindano haya—Kenya, Uganda na Tanzania—waliishia katika hatua ya robo fainali, fainali za mwaka huu zinaahidi kuwa kilele cha msisimko.
Burudani kutoka kwa Zuchu, Savara na Eddy Kenzo itakuwa chachu ya kuhitimisha mashindano yaliyojaa matukio na hisia.
Kwa upande mwingine, kumekuwa na malumbano mitandaoni kati ya mashabiki wa Kenya na Tanzania, hususan baada ya timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, kudondoshwa nje ya michuano hiyo katika robo fainali.
Mashabiki wa Tanzania hawakusita kuchokoza wenzao kwa kejeli, jambo lililoongeza ladha ya ushindani wa nje ya uwanja.