News
IEBC kufanikisha chaguzi ndogo

Taifa sasa linajiandaa kwa chaguzi ndogo hasa baada ya kuapishwa kwa mwenyekiti na makamishna wapya sita wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC hivi majuzi.
Chaguzi hizo zitatumika kutathmini ushawishi wa kisiasa kati ya rais William Ruto, waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka.
Miongoni mwa maeneo kunakotarajiwa kufanyika uchaguzi mdogo ni eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi ambako wakaazi wamekuwa bila uwakilishi bungeni baada mahakama ya upeo kubatilisha ushindi wa Harrison Kombe kama mbunge wa eneo hilo mwezi Mei mwaka 2025.
Maeneo mengine ni Kaunti ya Baringo, eneo bunge la Banisa, Ugunja, Malava, Mbeere kaskazini na Kasipul.
Maeneo 15 ya uwakilishi wadi nchini pia wananchi watashiriki uchaguzi mdogo kutafuta wawakilishi wao wa wadi.
Chaguzi hizi zinatokana na hatua ya kuteuliwa kwa wawakilishi wa baraza la mawaziri nchini, baadhi ya viongozi kufariki, na kubatilishwa kwa matokeo ya uchaguzi wa baadhi ya wabunge na wawakilishi wadi kadhaa wa mabunge ya kaunti.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Mawakili Kilifi waungana kushtumu mauaji ya Wakili Mbobu

Siku chache baada ya Wakili Kyalo Mbobu kuuawa kinyama kwa kupigwa risasi mara kadhaa akiwa kwenye gari lake barabara ya Lang’ata jijini Nairobi, mawakili mjini Kilifi kaunti ya Kilifi wameungana na mawakili wengine nchini siku ya Ijumaa Semtemba 12 mwaka huu kufanya matembezi ya amani, wakishutumu vikali mauaji hayo.
Wakiongozwa na Mwakilishi wao Sesil Mila, mawakili hao walilaani vikali mauaji ya wakili Mbobu wakiishutumu serikali kwa kutowajibikia swala la usalama wa wananchi wake.
Aidha waliitaka idara ya usalama kuhakikisha kuwa inafanikisha wajibu wake wa kuwalinda mawakili wakisisitiza haja ya haki kupatikana kwa familia ya mwendazake wakili Kyalo.

Mawakili wa Kilifi wakiongozwa na Sesil Mila, washtumu mauaji ya Wakili Kyalo Mbobu
Mawakili hao sasa waliitaka idara ya upelezi na asasi zote husika kuhakikisha kuwa uchunguzi wa kina unafanywa kubaini watuhumiwa wa mauaji hayo ili wachukuliwe hatua kali za kisheria haraka iwezekanavyo.
Taarifa ya Hamis Kombe
News
IEBC inaendelea kutambua vituo vya kusajili wapiga kura

Maafisa wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC wamesema wanaendelea na zoezi la kutambua sehemu za kuweka vituo vya kusajili wapiga kura hasa maeneo ya mashinani.
Afisa msimamizi wa tume ya IEBC eneo bunge la Ganze kaunti ya Kilifi, Mohammed Bahero Aboud alisema juhudi hizo ni kuhakikisha zoezi la usajili wapiga kura litakaloanza rasmi Septemba 29, mwaka huu linafaulu.
Akizungumza mjini Kilifi, Bahero alisema tume hiyo inatumia mbinu mpya ya kutambua vituo vya jadi vya usajili wapiga kura na kuweka vituo vipya kulingana na mapendekezo ya sheria.
Wakati huo huo alidokeza kwamba tume ya IEBC imekuwa ikihamashisha wakenya kutokubali kushawishiwa na wanasiasa na kujisajili katika maeneo yasiokuwa yao hasa msimu huu ambao zoezi hilo linakaribia kuanza.
Taarifa ya Joseph Jira