News
Gavana Godhana Awataka Wakulima na Wafugaji Kudumisha Amani

Gavana wa kaunti ya Tana River Dhado Godhana amezitaka jamii za wakulima na wafugaji kuzika tofauti zao na kuishi kwa Amani na umoja ili kufungua fursa zaidi za waekezaji kuingia katika kaunti hiyo.
Godhana amesema mvutano uliopo baina ya jamii hizo mbili huenda ukaibua suala la ukosefu wa usalama huku akisema kuwa hakuna mwekezaji atakayekubali kuwekeza mahali palipo na mvutano au ukosefu wa uwiano.
Aidha ameongeza kuwa suala la ardhi ambalo limekuwa donda sugu katika kaunti hiyo wanalifahamu na kama viongozi wanatafuta mbinu za kuhakikisha mzozo huo unadhibitiwa kikamilifu.
“Hii malumbano yenu mko nayo ya ardhi tunajua mna tatizo la ardhi iwe ya malisho au ukulima, tunataka tuwahimize kwamba hayo mambo mtafute njia za kudhibiti yasipite kiwango kwa sababu hakuna mtalii atakuja akijua kuna mizozo”, alisema Godhana
News
Mwanaharakati Mwabili Mwagodi apatikana

Mwanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu Mwabili Mwagodi ambaye alidaiwa kutekwa nyara akiwa nchini Tanzania sasa amepatikana.
Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za kibinamu nchini la VOCAL Africa Hussein Khalid, alisema Mwabili alipatikana katika msitu wa Kinondo eneo bunge la Msambweni kaunti ya Kwale mwendo wa saa tisa usiku akitembea kuelekea Diani.
Khalid alisema Mwabili, anaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Pandya mjini Mombasa kisha baadaye atasafirishwa kwa ndege hadi jijini Nairobi kuungana na familia yake.
“Tunashukuru Mwabili amepatikana akiwa hai japo amedhohofika na anaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Pandya na kisha atarudi Nairobi kukutana na familia yake lakini tunaiambia serikali ya Kenya na Tanzania ni lazima wahusika kukomesha tabia hii ya kuwateka watu nyara kuna sheria kama mtu amekosea apelekwe Mahakamani”, alisema Khalid.
Hata hivyo Wanaharakati hao wa kutetea haki za kibinadamu waliishtumu serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuwanyanyasa wanaharakati wa kijamii wa taifa la Tanzania na wale wanaoingia Tanzania kutoka mataifa mengine ili kuendeleza hamasa za haki za kijamii.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Herman yahairishwa

Kesi ya mauaji ya mfanyabiashara ambaye ni raia wa Uholanzi, Rowenhorst Herman na mlinzi wake Evans Bokoro imeahirishwa hadi mwezi Oktoba mwaka huu kufuatia Mahakama kuingia kwenye mapumziko rasmi ya majaji.
Mke wa Marehemu, Riziki Cherono pamoja na mshukiwa mwenza Timothy Omondi wanakabiliwa na mashtaka ya kupanga na kutekeleza mauaji hayo yaliyotokea Juni 4 mwaka 2021 katika eneo la Shanzu kaunti ya Mombasa.
Katika kikao cha awali cha Mahakama, Afisa wa Polisi Koplo Richard Cheruiyot alieleza mbele ya Jaji Wendy Micheni kwamba Cherono alijaribu kuonekana kama mwathirika kwa madai ya kutekwa nyara na majambazi waliodaiwa kuvamia nyumba yao.
Afisa huyo alieleza kwamba walimkuta Cherono akiwa amefungwa kwenye usukani wa gari lake, huku akidai kwamba alivamiwa na kulazimishwa kuondoka nyumbani kwao akiwa chini ya tishio la bunduki.
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa ulibaini kwamba Marehemu Herman alipatikana amefariki nyumbani kwake akiwa amefungwa mikono na miguu huku mlinzi wao, Evans Bokoro, alikutwa akiwa hai kwa taabu karibu na bwawa la kuogelea lakini baadaye alifariki akipelekwa hospitalini.
Mashahidi wa upande wa mashtaka pamoja na polisi, wanaamini kwamba Cherono ndiye mshukiwa mkuu wakidai kwamba alipanga na kufanikisha mauaji hayo kwa kushirikiana na watu wengine, wakiwemo waliotajwa kuwa sehemu ya genge lililovamia nyumba hiyo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu