News
Familia ya mchuuzi aliyepigwa risasi Nairobi yalilia haki.

Familia ya Boniface Mwangi Kariuki, mchuuzi mwenye umri wa miaka 22 aliyepigwa risasi kichwani na afisa wa polisi wa kupambana na ghasia katika barabara ya Moi jijini Nairobi wakati wa maandamano sasa inaomba haki na hatua za haraka zichukuliwe.
Jonah Kariuki Nyambura babake mwathiriwa alidai hakufahamu kosa la mwanawe lililomfanya afisa wa polisi kufyatua risasi akisema alikuwa akijilinda tu kwa kuuza barakoa.
Akihutubia wanahabari Jumatano asubuhi 18 juni 2025, Nyambura alisema mwanawe yuko katika hali mahututi katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), alikopelekwa kutibiwa baada ya kupata majeraha mabaya kichwani.
Kariuki aliongeza kuwa alifarijika baada ya kumuona mtoto wake akiwa hai, kinyume na taarifa za awali kuwa alifariki baada ya kupigwa risasi.
“Nilimuona kwenye video hiyo kwenye simu yangu, na majira ya saa nane jioni nilipigiwa simu na watu wake wa karibu kuwa mwanangu amepigwa risasi, nililala hapa (KNH) na asubuhi nilimuona katika chumba cha wagonjwa mahututi- ICU, angalau sasa nina matumaini,” alisema Kaiuku.
Aidha aliomba hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya afisa wa polisi aliyempiga risasi mwanawe.
“Ningewaomba maafisa wa polisi wawajibike kwa sababu wana watoto pia. Aliyempiga risasi pia ni mtoto wa mtu. Hatua kali zichukuliwe dhidi ya afisa huyo wa polisi,” aliongeza Kariuki.
Alikuwa ameandamana na seneta wa Busia Okiya Omtatah, ambaye alilaani ukatili wa polisi, na kuongeza kwamba tukio hilo lazima lishughulikiwe haraka.
Wakati huo huo huduma ya kitaifa ya Polisi NPS ilithibitisha kukamatwa kwa afisa aliyempiga risasi Mwangi huku shinikizo la kudhibiti ukatili wa polisi nchini likiendelea kukithiri.
Kwa upande wake rais wa chama cha mawakili Faith Odhiambo ametoa wito wa kukamatwa kwa afisa mwengine wa polisi aliyeonekana kwenye video na afisa wa polisi aliyempiga risasi mchuuzi wa barakoa kichwani wakati wa maandamano ya Jumanne 17 Juni 2025 jijini Nairobi.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Mzozo kati ya Kenye na Tanzania waendelea kutokota

Serikali ya Kenya imeiandikia barua jumuiya ya afrika mashariki kupinga vikwazo vilivyowekwa na Tanzania kuhusu kufanya biashara katika taifa hilo.
Katibu mkuu katika idara ya EAC Daktari Caroline Karugu, alisema kenya imebaini kuwa agizo hilo haliambatani kamwe na masharti muhimu ya itifaki ya soko la pamoja la EAC, ambayo inahakikisha uruhu wa watu kusafiri, kuhudumu na haki ya kuanzishwa kwa biashara na raia wa mataifa ya afrika mashariki.
Aidha Kenya iliasema imeandika rasmi barua kwa EAC kuiarifu rasmi jamhuri ya muungano wa Tanzania kuangazia upya agizo hilo ili kuhakikisha inafuata kikamilifu mkataba wa EAC na sheria za Jumuia.
Maafisa wa EAC kwa sasa wanafanya uchambuzi wa hatua hiyo na itawasilisha hatua zozote zilizokiukwa pamoja na kaununi zilizopo katika mkutano ujao wa baraza la kisekta la biashara, viwanda na uekezaji.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Mradi wa Galana Kulalu kukabili uhaba wa chakula nchini

Serikali imesema inalenga kufikia ekari 3,200 za kilimo katika mradi wa uzalishaji chakula wa Galana Kulalu ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2025.
Waziri wa maji, usafi na kilimo nyunyizi Eric Mugaa alisema tayari ekari 1,060 zimepandwa mahindi kwa kutumia mifumo ya umwagiliaji ya kisasa, mazao ya kwanza yakitarajiwa kuvunwa mwezi Oktoba, huku maandalizi yakuongeza mashamba zaidi yakiendelea.
Akizungumza alipozuru mradi wa Galana Kulalu kutathmini maendeleo ya shughuli za mradi huo, waziri Mugaa pia alisema miundombinu mipya ikiwemo mabwawa ya kuhifadhi maji, mifareji ya kunyunyiza maji, na mitambo ya kusukuma maji imejengwa ilikuwezesha shughuli za unyunyizaji.
Wakati huo huo, waziri huyo alidokeza kuwa ujenzi wa Daraja la Sabaki umefikia hatua ya asilimia 50, akidokezakwamba daraja hilo linatarajiwakukamilika hivi karibuni ili kurahisisha usafirishaji wa vifaa vya kilimo na vile vilekusafirisha mazao kutoka Galana Kulalu.
Serikali kupitia Mamlaka ya unyunyizi iliahidi kuendelea kushirikiana na sekta za kibinafsi kuhakikisha mradi huo wa Galana Kulalu unakuwa suluhu ya uhaba wa chakula hapa nchini.
Taarifa ya Mwanahabari wetu