News
Dkt. Nzai, awahimiza vijana kujisajili kwa mpango wa elimu kwa wote

Kama njia mojawapo ya kuimarisha vijana wa Pwani kupitia elimu, Jumuiya ya kaunti za Pwani imeanzisha mpango wa elimu kwa wote unaotoa elimu ya juu kupitia mtandao.
Mkurugenzi wa Jumuiya ya kaunti za Pwani, Dkt. Emmanuel Nzai alisema wanalenga vijana elfu tano kupitia mpango huo huku idadi lengwa ya vijana wa kaunti ya Kilifi ikiwa 700.
Dkt. Nzai alitoa wito kwa vijana kujisajili kwenye mpango huo ikizingatiwa kwamba ni vijana 25 pekee katika kaunti ya Kilifi ambao tayari wamejisajili kwenye mpango huo.
Dkt. Nzai alidokeza kwamba wanashirikiana na taasisi ya kimataifa ya Regeneysis kufanikisha mpango huo.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu kaunti ya Kilifi Felkin Kaingu alisema kupitia wafadhili mbalimbali watahakikisha kuwa vijana watakaojisajili kwenye mpango huo wanafadhiliwa kuendeleza masomo yao.
Hata hivyo vijana ambao tayari walinufaika na mpango huo walisisitiza haja ya hamasa zaidi kutolewa kwa vijana hasa wa mashinani ili wapate kujua kuhusu mpango huo wa elimu kwa wote.
Taarifa ya Hamis Kombe
News
Godhana, awataka wakaazi kutoingiza siasa miradi ya maendeleo

Gavana wa kaunti ya Tana River Dhadho Godhana amewataka wenyeji wa kaunti hiyo kujiepusha na wanasiasa ambao wanaingiza siasa kwenye masuala ya maendeleo.
Godhana alisema hilo limechangia kaunti ya Tana River kusalia nyuma kimaendeleo hali ambayo itasababisha miradi mingi kuzidi kukwama.
Godhana alisema ni lazima viongozi na wenyeji wa kaunti ya Tana River washirikiane na uongozi wa kaunti ili kuafikia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Wakati huo huo Godhana aliesema mradi wa Village Cluster ambao umekuwa ukipingwa ndio utakaosaidia kudhibiti changamoto ambazo zinaikumba kaunti ya Tana River.
Naye Mahat Ali Loka ambaye ni Naibu Gavana wa kaunti ya Tana River, aliwaonya wanasiasa kutoka kaunti zingine dhidi ya kuingilia siasa za kaunti hiyo huku Spika wa bunge la kaunti hiyo Osman Noor Galole, akitoa onyo kwa wafanyikazi wa umma dhidi ya kujumu la serikali ya kaunti ya Tana River.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Mwili wapatikana baharini Shelly Beach Likoni

Polisi kaunti ya Mombasa wanachunguza kisa ambapo mwili wa mwanamme ambaye hajafahamika umepatikana ukielea katika maji ya bahari hindi kwenye ufuo wa Shelly Beach eneo bunge la Likoni.
Ripoti ya polisi ilibaini kuwa mwili huo uligunduliwa na wavuvi eneo hilo, ambao walipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Shelly Beach kuhusiana na tukio hilo.
Polisi walisema hawakubaini mara moja anakotoka mtu huyo.
Vile vile haikubainika iwapo marehemu alizama au aliuawa kabla ya mwili wake kutupwa baharini.
Polisi walisema hawajakutana na stakabadhi zozote za kumtambulisha mtu huyo huku wakiwasihi wananchi kutoa taarifa iwapo wanafahamu familia ya marehemu.
Mwili unahifadhiwa katika hifadhi ya maiti katika hospitali ya Rufaa ya Coast General Mombasa wakati uchunguzi zaidi ukiendelea.
Taarifa ya Joseph Jira