News
David Maraga amfokea mkurugenzi wa mashtaka ya umma

Jaji mkuu mstaafu David Maraga amefokea ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma kwa kuwashtaki kwa makosa ya ugaidi vijana waliokamatwa wakati wa maandamano.
Maraga alisema hatua hiyo inawadhulumu vijana hao ambao wamesalia korokoroni wakisubiri kesi yao kuamuliwa.
Maraga pia aliaka kesi hizo zitupiliwe mbali akisema hazina msingi, akidai hatua hiyo ni utumizi mbaya wa sheria kwa madai ya kukabiliana na magaidi, ilihali walioshtakiwa walikuwa wakishinikiza uongozi bora nchini.
Maraga pamoja na wanaharakati wa kutetea haki za binadam walimtaka mkurugenzi wa mashtaka ya umma Renson Ingonga kuwajibika na kutupilia mbali kesi hizo na kuwaruhusu washukiwa kuendelea na maisha yao.
Taarifa ya Joseph Jira
News
IEBC inaendelea kutambua vituo vya kusajili wapiga kura

Maafisa wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC wamesema wanaendelea na zoezi la kutambua sehemu za kuweka vituo vya kusajili wapiga kura hasa maeneo ya mashinani.
Afisa msimamizi wa tume ya IEBC eneo bunge la Ganze kaunti ya Kilifi, Mohammed Bahero Aboud alisema juhudi hizo ni kuhakikisha zoezi la usajili wapiga kura litakaloanza rasmi Septemba 29, mwaka huu linafaulu.
Akizungumza mjini Kilifi, Bahero alisema tume hiyo inatumia mbinu mpya ya kutambua vituo vya jadi vya usajili wapiga kura na kuweka vituo vipya kulingana na mapendekezo ya sheria.
Wakati huo huo alidokeza kwamba tume ya IEBC imekuwa ikihamashisha wakenya kutokubali kushawishiwa na wanasiasa na kujisajili katika maeneo yasiokuwa yao hasa msimu huu ambao zoezi hilo linakaribia kuanza.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Kaunti ya Mombasa kukumbatia matumizi ya mfumo wa miale ya jua

Serikali ya kaunti ya Mombasa imesema imeanza kutekeleza mpango wa kutumia nishati mbadala katika vituo vyote vya huduma za kaunti, kwa kuanza na mabadiliko ya mfumo wa taa hadi kutumia umeme wa miale ya jua.
Kwa mujibu wa waziri wa kawi, rasilimali asili na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kaunti ya Mombasa, Emily Achieng, hatua hii inalenga kupunguza gharama za matumizi ya umeme na kuhimiza matumizi ya nishati safi na rafiki kwa mazingira.
Mbali na hilo, waziri huyo alisema kaunti inaendelea kuweka vifaa maalum vya kupima ubora wa hewa katika maeneo mbalimbali ya mji na ndani ya taasisi za umma.
Lengo ni kupata ushahidi wa kisayansi kuhusu kiwango cha uchafuzi wa hewa, na kuchukuliwa kwa hatua za kisheria kwa wanaokiuka sheria.
Vifaa hivyo tayari vimewekwa katika hospitali ya rufaa ya Coast General na baadhi ya shule ikiwa ni sehemu ya mpango wa muda mrefu wa kaunti, kujenga ustahimilivu dhidi ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
Mikakati hiyo pia itasaidia kaunti katika kufanya maamuzi kuhusu maeneo yanayofaa kuwekwa biashara fulani, ili kulinda wananchi dhidi ya maradhi yanayosababishwa na uchafuzi wa hewa.
Taarifa ya Mwanahabari wetu.